Home Azam FC DUBE HATIHATI KUIKOSA SIMBA SC

DUBE HATIHATI KUIKOSA SIMBA SC


STRAIKA wa Azam, Prince Dube anatarajiwa kufanyiwa vipimo zaidi vya Afya baada ya mchezaji huyo kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara hali inayompelekea kukosa michezo kadhaa ya timu hiyo.

Mchezaji huyo alikosa mechi ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Simba katika hatua ya nusu fainali ambapo timu yake ilipoteza kwa bao 1-0 katika uwanja wa Majimaji Mkoani Songea.

Azam inashikilia nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 64 katika michezo 32 huku timu hiyo ikikabiliwa na kibarua kizito katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba Julai 14 kisha wakihitimisha msimu ugenini kwa kumenyana na Ruvu Shooting Julai 18.

Akizungumza hali ya Dube Daktari wa Azam, Mwanandi Swedi Mwankemwa, alisema kuwa mchezaji huyo alikuwa akilalamika kutokana na maumivu ya nyonga mara kwa mara ila walipochukua hatua za kumpeleka hospitalini alikutwa hana tatizo lolote linalomsumbua katika mwili wake.

“Baada ya kuona ana maumivu makali tulimpeleka katika Hospitali ya Saifee kisha kuchukuliwa vipimo vya (MRI) ila kwa bahati mbaya hakuweza kuonekana na tatizo lolote katika mwili wake yaani alionekana yupo kawaida tu” alisema

Aidha Mwankemwa, alisema kuwa kwa sasa wanajiandaa kumfanyia vipimo zaidi na kama itashindikana kugundulika tatizo lake wataamua kuchukua hatua zaidi ya kumpeleka mchezaji huyo nje ya nchi kwa ajili ya kufanyiwa matibabu ya kiuchunguzi zaidi.

Mchezaji huyo alianza kusumbuliwa na matatizo hayo ya ghafla kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Rhino Rangers baada ya kushindwa kuendelea na mchezo.

SOMA NA HII  LWANDAMINA: TUNAITAKA NAFASI YA YANGA