Home Makala ISHU YA UPANGAJI MATOKEO HAIFAI, MZEE MPILI ASIWATOE SIMBA KWENYE RELI

ISHU YA UPANGAJI MATOKEO HAIFAI, MZEE MPILI ASIWATOE SIMBA KWENYE RELI

 


MZUNGUKO wa pili umekuwa ukigubikwa na matokeo mengi ya ajabu ambayo yanashangaza wengi. Hili lipo wazi rejea mchezo uliopita ambao uliwakutanisha Simba v Yanga.

Kila mmoja alikuwa anavutia kwake na mwisho wa siku ubao wa Uwanja wa Mkapa ulisoma Simba 0-1 Yanga. Pongezi kwa washindi na pongezi kwa wale ambao walishindwa kupata matokeo.

Kikubwa ambacho kinatakiwa kwa kila timu kuwa na nidhamu kwa kuwa hapa tulipokutana niliweka wazi kwamba hakuna haja ya kwenda na matokeo mfukuni.

Dunia imeshuhudia namna matokeo yalivyowashangaza wengi na inatakiwa kuwa hivyo wakati wote. Ligi ni ushindani na unahitajika kila wakati kwenye soka.


Mara nyingi kwenye mzunguko wa pili kumekuwa na ishu ya upangaji wa matokeo hili sio sawa na halipaswi kupewa nafasi kwa namna yoyote ile.


Jambo la msingi ambalo linahitajika ni kuona kwamba kila timu inashinda kwa kupambana kwenye kusaka ushindi bila kutegemea kubebwa na mwamuzi ama kununua matokeo.


Mamlaka husika ambayo inasimamia masuala ya mpira namaanisha Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) ina jukumu la kulitazama hili na kufuatilia kwa ukaribu.

Hapa kuna maswali ya kujiuliza kwamba ikiwa timu fulani inatoa maelekezo kwa timu moja kushinda mchezo wao dhidi ya timu fulani ni nini ambacho kinatokea kwenye mechi nyingine?

Ngumu sana kufikia mafanikio ya soka ikiwa kunamambo ambayo yanakwenda tofauti na hesabu ambazo zipo kwa kuwa kuna timu hazipendi maendeleo ya mtu mwingine.


Hakuna weledi ambao unatumika kwa timu kuamua kwamba timu fulani ishinde tena ni timu kubwa ambayo inashiriki nayo Ligi Kuu Bara katika hili sio jambo la kukaa kimya .


Kuanzia timu husika ni lazima ichukue hatua kwa wahusika ambao wamefanya jambo hilo na kueleza sababu ya wao kufanya hivyo kisha adhabu ikatolewa.


Nilipata nafasi ya kumsikiliza Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli aliweka wazi kwamba kuna timu ambazo zinategemea kubebwa. Kwa namna yoyote ile kubebwa pia sio jambo la msingi ni lazima kila timu ipambane kupata matokeo chanya.


Kwa namna yoyote ile ikiwa kuna timu ambayo inategemea kubebwa haiwezi kuleta ushindani wa kweli katika mechi ambazo watakuwa wanacheza.

Kwa sasa kila kitu kipo wazi na kila mmoja anajua kile ambacho kinaendelea kwenye ligi ya Bongo kwamba ushindani sio wa kitoto hili ni jambo jema na linapaswa kuendelea kupewa nafasi siku zote.

Lakini inapokuja masuala ya kubebwa, masuala ya upangaji wa matokeo katika hili hapana kwani kila timu inahitaji kufanya vizuri ili kufikia malengo ambayo imejiwekea.

Ikiwa timu moja haipendi kuona matokeo mazuri ya timu nyingine inakuwa imetoka kwenye ulimwengu wa mpira ni furaha bali inakuwa ni vita.

Hilo sio sawa mpira sio vita mpira ni burudani na wapinzani huwa inakuwa ndani ya dakika 90 ila baada ya hapo maisha yanaendelea na kila mmoja anaongea na mshikaji wake kwa kuwa kazi yao imekamilika.

SOMA NA HII  U 23 MNASTAHILI PONGEZI, KAZI INAENDELEA KWA WAKUBWA


Sasa kama inatokea vita inaanza nje ya uwanja kwa timu fulani kuishambulia timu moja, ama timu fulani kuzungumza vibaya kuhusu timu nyingine hili halijakaa sawa.


Tunapenda kuona kwamba uimara wa timu uonekane uwanjani kwani mchezo wa mpira sio suala la kuweza kufichika linaonekana na kila mmoja anaona namna ambavyo watu wanapambana kupata matokeo.

Kwa nyakati hizi za lala salama suala la upangaji matokeo lisipewe nafasi na kila timu ipambane kwa nguvu zake kupata kile ambacho inastahili baada ya dakima 90.

Iwe ni kwenye mechi za ligi hata zile Ligi Daraja la Kwanza hakuna umuhimu wa kuwa na upangaji wa matokeo kwa kufanya hivyo kunayeyusha ushindani.

Masuala haya hayaleti afya kwenye soka letu ni lazima yaachwe na sheria 17 zifuatwe. Yule atakayefanya maandalizi mazuri ana nafasi ya kushinda bila matatizo.

Tunahitaji kuona kwamba ligi inapata bingwa bora ambaye hana makandokando na hilo litawezekana ikiwa hakutakuwa na masuala ya michongo pamoja na upangaji wa matokeo.

Kikubwa ni maandalizi nakupanga mipango makini kwa ajili ya mechi ambazo zimebaki kwa sasa hatua hii ya mwisho.

Zile ambazo zitapata nafasi ya kushuka zinapaswa zikumbukwe kwamba jukumu lao ni kusaka ushindi kwenye mechi zao ili waweze kurudi tena kwenye ushindani wa Ligi Kuu Bara.

Wakati huu ni wa kuchanga karata upya na kupata matokeo mazuri ambayo yatawafanya waweze kurudi kwenye ligi muda mwingine.

Kurudi kwenye ligi kwa timu ambazo zitashuka ni jukumu lao kufanya maandalizi. Inabidi watambue kuwa kurudi kutoka Ligi Daraja la Kwanza mpaka Ligi Kuu Bara sio kazi nyepesi.

Kazi kubwa kwa wachezaji iwe kutafuta ushindi katika mechi zao zijazo na kupambana kwa hali na mali kupata wanachostahili.

Pia imekuwa gumzo kubwa kwa sasa kuhusu mwanachama wa Yanga, Omar Mpili maarufu kama Mzee Mpili kuzungumza kuhusu mechi yao dhidi ya Simba ambayo inatarajiwa kuchezwa Kigoma.

Tambo ni muhimu na tunaona kwamba kumekuwa na hamasa kubwa kwa wachezaji pamoja na mashabiki wa Yanga lakini wachezaji wa Simba wanapaswa waelewe kwamba kazi yao ni kucheza.

Maneno na tambo zisiwatoe mchezoni jukumu lao ni kutimiza majukumu bila kuogopa mpira uwanjani, nje ni tambo kama tambo na inaruhusiwa kabisa hasa ukiongeza na utani wa jadi.

Naona kwamba tayari Mbeya Kwanza ina uhakika wa kushiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao hapa tunawaamba kwamba karibuni huku maisha yanaendelea.

 Ninapenda kuwakumbusha kwamba zile jitihada ambazo zilitumika kwenu kupanda ligi basi huku pia ziendelee kwa kasi.

Kila kitu kinawezekana kikubwa mipango na kufanya vizuri bila kuchoka kwa wakati huu uliopo bila kubadili gia ambayo walianza nayo.