Home Azam FC KISA KAGAME CUP, AZAM WASHUSHA VIKOSI VIWILI

KISA KAGAME CUP, AZAM WASHUSHA VIKOSI VIWILI

 


KUFUATIA ushiriki wao kwenye michuano ya kombe la Kagame mwaka huu, Uongozi wa klabu ya Azam umeweka wazi kuwa utalazimika kukigawa kikosi chao mara mbili, ili kupata timu itakayoshiriki Kagame Cup huku sehemu ya kikosi iliyosalia ikiendelea na programu za maandalizi ya msimu ‘Pre Season’.

Azam ni miongoni mwa timu tisa ambazo tayari zimethibitisha ushiriki wao kwenye michuano ya Kagame Cup inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti Mosi, mwaka huu, ambapo kwa Tanzania timu tatu zitawakilisha.

Katika michuano hiyo Azam wamepangwa kwenye kundi B sambamba na klabu za Atlabara ya Sudani Kusini, na Tusker ya Kenya, na wanatarajia kucheza mchezo wao wa kwanza Jumatatu dhidi ya Tusker ya Kenya kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Akizungumzia kuhusu mipango yao kwenye kombe la Kagame, kocha msaidizi wa klabu ya Azam, Vivier Bahati amesema: “Tumeanza vizuri maandalizi ya kikosi chetu kuelekea michuano ya kombe la Kagame, kutokana na ushiriki wetu katika michuano hii tumelazimika kugawa kikosi chetu katika makundi mawili.

“Tumepanga kuwatumia wachezaji wa kikosi cha vijana U20 pamoja na wachezaji waliorejea kutoka kwenye klabu ambazo walienda kwa mkopo kwenye michuano ya Kagame Cup, halafu kundi lile la pili litakuwa na programu maalum ya maandalizi ya msimu mpya.”

SOMA NA HII  JAMBO LA AZAM FC BADO HALIJABADILIKA KABISA