Home Yanga SC NABI ATAKA KIUNGO HUYU KUTOKA MISRI

NABI ATAKA KIUNGO HUYU KUTOKA MISRI


IMETHIBITISHWA kuwa uongozi wa Yanga upo kwenye mazungumzo na kiungo wa kimataifa wa Ghana anayecheza soka la kulipwa kwenye Klabu ya Cleopatra inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri, Kwame Bonsu ili kumsajili kwa ajili ya msimu ujao wa 2021/22.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Yanga kimelitonya Championi Ijumaa, kuwa tayari mabosi wa klabu hiyo wamekubali kuliweka jina la kiungo huyo wa Ghana ambaye amesaliwa na mwaka mmoja tu kwenye mkataba wake wa Cleopatra, katika listi ya nyota wapya wanaotarajiwa kusajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

“Ni kweli uongozi kwa kupitia kamati yetu ya usajili umekubaliana na maamuzi ya kujumuisha jina la kiungo wa Ghana, Kwame Bonsu kwenye listi ya nyota wapya ambao wanatarajiwa kusajiliwa kwa msimu ujao.

“Hii ni baada ya kumfuatilia na kugundua kuwa ni miongoni mwa viungo bora Afrika, lakini pia ni kiungo mwenye uzoefu mkubwa na michuano mikubwa, akiwa tayari ameshacheza kwenye timu kubwa kama Esperance ya Tunisia na Asante Kotoko ya Ghana.”

Akizungumzia kuhusu usajili wa kiungo huyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Thabit Kandoro, alisema: “Kwa sasa tumesitisha kwa muda kuzungumzia masuala ya usajili, kwa kuwa bado tuna kibarua cha

mchezo wetu wa fainali ya Kombe la FA dhidi ya Simba Julai 25, mwaka huu na tutazungumzia masuala ya usajili baada ya mchezo huo kukamilika.”

Nyota huyo anakuja kuiimarisha Yanga baada ya timu hiyo kufanikiwa kusuka safu imara ya ushambuliaji ambayo inaelezwa itaongozwa na Wacongo, Heritier Makambo, Fiston Mayele na Kazadi Kasengu.

Atakuja kufanya kazi na Nasreddine Nabi ambaye ni Kocha Mkuu wa timu hiyo.

SOMA NA HII  MOLOKO AANZA KUCHEKELEA YANGA...CHICO USHINDI PAMOJA NA YOTE NDIO BASI TENA...AJIPANGE...