Home Makala ‘NEXT LEVEL’ YA SIMBA IACHANE NA ‘UJANJAUJANJA

‘NEXT LEVEL’ YA SIMBA IACHANE NA ‘UJANJAUJANJA


JULAI 29, mwaka 2019 kutoka katika kinywa cha msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara yalitamkwa maneno yafuatao: “Tukio letu la wiki ya Simba limeigwa maeneo mbalimbali, lakini sisi tutataka kulifanya kwa ubora zaidi, na kauli mbiu yetu itaitwa ‘Iga Ufe, this is Next Level.”

Hii ilikuwa ni katika maandalizi ya tamasha lao kubwa la Simba Day.

Hapa Manara alitaka kuonyesha kuwa kuna utofauti wa wazi na mkubwa uliopo kati ya klabu ya Simba na klabu nyingine hasa za Ligi Kuu Bara. Kwangu hii ni moja kati ya kauli mbiu ‘Slogan’ bora zaidi ambazo zimewahi kutolewa na Manara kuihusu Simba.

Katika miaka ya hivi karibuni ni kweli Simba wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuiweka kauli mbiu hii katika utekelezaji, na ndiyo maana leo hii tunaizungumzia klabu ambayo imefanikiwa kutawala soka la Tanzania kwa kutwaa ubingwa kwa misimu minne mfululizo.

Simba wanastahili pongezi kwa mafanikio haya makubwa kwani mpaka sasa imepita miaka 41 tangu mara ya mwisho klabu moja kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa angalau misimu minne mfululizo.

Mara ya mwisho kufanya hivyo ilikuwa mwaka 1980, ambapo Simba walitwaa ubingwa kwa misimu mitano mfululizo.

Lakini Simba pia wameonyesha ukuaji mkubwa katika uthubutu wa kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa ambapo ndani ya misimu mitatu, wamefanikiwa kufika katika hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili.

Mafanikio haya makubwa ya Simba uwanjani, bila shaka yamechagizwa sana na usajili wa wachezaji bora ambao wengi wamefanikiwa kufikia matarajio ya viongozi waliowasajili.

Simba hawajatawala soka la uwanjani pekee bali hata katika mitandao ya kijamii ambapo mwishoni mwa mwaka jana, kwa mujibu wa mtandao wa Transfer Market unaoaminika kwa kuelezea takwimu za soka, uliutaja ukurasa wa soka wa Simba kwenye akaunti ya mtandao wa kijamii wa Instagram kuwa ukurasa namba moja kwa ukuaji miongoni kurasa za klabu duniani.

Kupitia mafanikio ambayo Simba imeyapata, ni wazi klabu nyingine za Tanzania zimepata nafasi ya kujifunza, jambo ambalo linazidi kuamsha ari ya kupambana na kufanya mabadiliko muhimu ya uendeshaji wa klabu hizo ili kufanya vizuri zaidi.

SOMA NA HII  BAADA YA KUSIKIA MAYELE NDIYE MFALME BONGO...BALEKE KAKUNA KICHWA WEE..KISHA AKASEMA HILI..

Lakini licha ya mafanikio hayo makubwa ya Simba, bado kuna baadhi ya changamoto za ‘kiujanjaujanja’ wa baadhi ya viongozi wa klabu hiyo, ambao unaonekana kutaka kutia doa jitihada za makusudi zinazofanywa kufikia malengo yao ya kuwa miongoni mwa klabu bora Afrika na duniani kwa ujumla.

Kwanini nazungumza hili? Hivi karibuni gumzo kubwa lilikuwa ni sauti ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Dokta. Arnold Kashembe ambaye kupitia kituo kimoja cha habari alisikika akizungumzia makosa makubwa yaliyofanywa na viongozi wa juu wa klabu hiyo katika maamuzi ya mambo nyeti.

Kwa mujibu wa Kashembe kumekuwa na madudu makubwa yaliyofanyika kwenye baadhi ya maeneo

kama vile; mikataba ya haki za matangazo ya televisheni, ubinafsi wa baadhi ya viongozi wanaotaka kuitumia klabu hiyo kwa faida zao, na hata ishu ya mabadiliko ya uendeshaji wa klabu.

Ukimya wa uongozi wa Simba baada ya shutuma hizi unaleta taswira mbili kubwa moja shutuma hizi ni za ukweli, na hakuna namna ya kutumia nguvu kuzipinga.

Au mbili shutuma hizi si za kweli na labda klabu imeona hakuna haja ya kutumia nguvu kubwa kushindana nazo wakati wana kazi kubwa ya kutimiza malengo yao ya kushinda kombe la Shirikisho kwenye fainali dhidi ya Yanga, baada ya kutetea ndoo ya Ligi Kuu Bara.

Katika hili nadhani tuache wakati utatupa majibu sahihi ya kipi ni pumba na lipi ni la ukweli, lakini nadhani kama klabu ambayo ina malengo ya kufikia daraja A la klabu bora za Afrika, na labda duniani ni lazima wahakikishe wanahusianisha malengo yaliyo kwenye mipango ya karatasi na uhalisia wa mabadiliko yanayohitajika.

Ni lazima wakubali kutoa sadaka kubwa ya kuachana na baadhi ya watu, ambao wanaonekana kuwa kikwazo katika mpango huo wa mafanikio.