Home Makala UCHAGUZI UMEISHA, TUMUUNGE MKONO WALLACE KARIA

UCHAGUZI UMEISHA, TUMUUNGE MKONO WALLACE KARIA


WIKIENDI hii kulikuwa na tukio kubwa kwenye tasnia ya soka, na tukio hilo ulikuwa ni uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF), ambao ulihusisha nafasi ya Urais pamoja na nafasi za Wajumbe wa Kamati Tendaji ambao walikuwa wanapambana kupata nafasi ya kuziwakilisha kanda zao.

Kabla ya uchaguzi wenyewe kufanyika ni wazi ilikuwa imeshajulikana kuwa Wallace Karia alikuwa anasubiri kuthibitishwa tu kama Rais wa  TFF kutokana na kuwa mgombea pekee aliyekidhi vigezo vyote kwenye nafasi ya Urais.

Kulikuwa na vigingi vingi kuelekea uchaguzi huu, wapo ambao walidiriki kutinga mahakamani kuzuia mchakato mzima wa uchaguzi kwa kile walichoeleza kuwa ulikiuka baadhi ya kanuni lakini jambo la kheri ni kuwa yote yaliisha na ratiba ya uchaguzi ikabaki palepale na tayari Wallace Karia alifanikiwa kutetea kiti chake kwa muhula wa pili ambapo atadumu madarakani kwa miaka minne akiliongoza Shirikisho hilo.

Kwa sasa uchaguzi umeisha hivyo ni wazi tunapaswa kujikita katika kupambania maendeleo ya mpira wetu ambao kwa kiasi kikubwa unaendelea kukua kadri siku zinavyozidi kusogea. Masuala ya migogoro ambayo haina afya na mustakabali wa maendeleo ya mpira wetu kwa sasa hayana nafasi kinachopaswa kufanyika ni kumuunga mkono Rais Karia ili mpira wetu uzidi kusonga mbele.

Rais Karia ni miongoni mwa viongozi pekee waliofanya makubwa kwenye miaka minne ya kwanza akiwa Rais wa shirikisho, kuanzia ngazi ya klabu hadi kwenye timu za taifa, chini ya utawala wake tumeshuhudia mafanikio makubwa kwenye timu za taifa za wakubwa, vijana na timu za wanawake.

Chini ya uongozi wake ameinyanyua na kuipa thamani Ligi ya Wanawake haya ni miongoni mwa machache ambayo Rais Karia alianza nayo na kwa kiasi kikubwa amefanikiwa. Hivyo basi tuungane kwa pamoja kuendeleza safari hii ambayo aliianzisha kwenye muhula wa kwanza kwenye uongozi wake.

Wajumbe wa kamati tendaji kutoka kanda mbalimbali ambao pia mmepata nafasi ya kushinda kwenye kinyang’anyiro ni muda wenu kuwa wasaidizi bora kwa Rais Karia kwenye kanda mnazotoka mnapaswa kuwa mstari wa mbele kuhakikisha soka linakuwa kutoka kila kona ya nchi.

SOMA NA HII  BAADA YA 'KUWASHIKA HASWA' YANGA...AUCHO ASHINDWA KUJIZUIA..UFUNGUKA KUHUSU DILI LAKE NA SIMBA

Kwa wale ambao walikwazika kwenye kipindi cha mchakato wa uchaguzi, ni muda wa kuungana pamoja kwani lengo lenu lilikuwa ni moja nalo ni kuhakikisha mpira wetu unasonga mbele, haina haja ya kuendeleza malumbano ambayo hayatakuwa na tija yoyote kwenye mpira wetu, kama hukufanikiwa kuubadilisha mpira ukiwa ndani ya shirikisho unaweza kuubadilisha hata ukiwa nje ya shirikisho kupitia maoni na ushauri wenye tija.

Leo tunashuhudia Ligi Kuu Bara ikishika nafasi ya nane kwa ubora barani Afrika, hili ni la kujivunia kwani siyo rahisi kwa ligi yetu kufikia hapo kama kusingekuwa na utawala bora kwenye shirikisho letu. Kila la heri Rais Karia.