BAADA ya Soka la Bongo kuripoti kuwa kiungo wa Simba, Ibrahim Ajibu amesaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuwatumikia wekundu hao wa Msimbazi, nyota huyo jana amesafiri kuelekea Morocco kujiunga na wachezaji wengine wa timu hiyo waliosafiri juzi.
Imemshuhudiwa Ajibu mida ya saa saba hivi akiwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam, na kuendelea na taratibu zote kwaajili ya kupaa na ndege ya Emirates kwenda Morocco.
Hata hivyo, Ajibu hakuwa peke yake kwani aliongozana na wachezaji wengine wa Simba wakiwemo nyota wapya na wengine wazoefu kikosini hapo.
Israel Patrick Mwenda, Abdul Samad Kassim na Yusuph Mhilu ni miongoni mwa nyota wapya walioongozana na Ajibu sambamba na nahodha wa timu hiyo John Bocco, Chriss Mugalu na Ally Salim.
Simba imeweka kambi katika jiji la Rabat nchini morocco ambapo itajifua kwa siku 15 kwaajili ya msimu ujao kabla ya kurudi nchini Agosti 26, 2021.