TUNAZUNGUMZIA zaidi kuhusu pesa ambazo Simba na Yanga wamepata katika mauzo ya Clatous Chama, Jose Louis Miquissone na Tuisila Kisinda. Nasikia pia sehemu ya dili hizi ndizo ambazo hawa wakubwa wamepewa ofa ya kufanya mazoezi Morocco.
Klabu zinacheka. Wachezaji wenyewe wanacheka. Nadhani Chama anacheka zaidi. Majuzi hapa alikuwa anasumbuana na Simba na akapewa pesa ndefu ya kusaini mkataba mpya (signing fee). Halafu sasa atakuwa amepewa signing fee nyingine kwa kusaini Morocco. Waarabu huwa wanatoa signing fee kwa wachezaji.
Baada ya hapo mishahara ni minono. Wote watatu kila mmoja lazima atakuwa analipwa zaidi ya Sh25 milioni kwa mwezi. Pesa ndefu lakini kumbuka kwamba pesa hii itakwenda kutumika DR Congo, Msumbiji na Zambia ambako tayari Chama alishapeleka pesa ya Simba.
Wachezaji wetu wazawa wanakodoa macho. Hakuna hata mmoja aliyetakiwa. Wachezaji wenyewe ndio hawa hawa ambao wanasumbua kwa matatizo ya utovu wa nidhamu kila kukicha. Wanakausha mzunguko wa pesa nchini kwa kuendelea kuwa hapa na kuchukua mishahara ya kawaida.
Mpaka sasa ni Saimon Msuva pekee ambaye anachukua pesa ya uhakika ya Waarabu pale Morocco. Msuva lazima atakuwa analipwa pesa ndefu kwa aina ya klabu ambayo anaichezea kwa sasa. Hauwezi kucheza Waydad Casablanca halafu ukalipwa chini ya Sh10 milioni kwa mwezi. Lazima atakuwa analipwa zaidi ya hapo.
Msuva alikwenda Waydad akiwa staa ambaye alitamba katika ligi hiyo akiwa na Difaa El Jadida ya hapo. Ina maana uhamisho wake umekuwa ghali kuanzia kwake mwenyewe. Sitaki kuzungumzia bonasi za kutwaa ubingwa wa Morocco msimu ulioisha. Maisha yanataka nini kwake?
Sijui ambacho Himid Mao atakuwa anapata katika timu yake ya Mafarao pale Misri lakini lazima atakuwa anavuta pesa ndefu kuliko kama angekuwa anacheza Namungo. Bahati nzuri kwake ni kwamba mpaka sasa anapambana vyema.
Kipi kinaendelea kwa wazawa wetu? Nilishasema hapa tofauti ya wazawa na wageni wanaokuja ni kujituma tu. Matumizi mengi ya nguvu, uwezo mkubwa wa stamina na machache mengineyo ndio yanayomtofautisha mchezaji wa Tanzania na mchezaji wa kigeni.
Leo tunao wengi na sasa tunaleta wageni wenye ubora ambao wanaitumia ligi yetu kupita. Sio jambo baya kwa klabu zetu. Zinapata pesa. Tatizo ni hawa wazawa wetu ambao wanapishana na magari ya mishahara ya Waarabu. Sijui wanajisikiaje.
Inaanzia katika vikosi vyao. Kwanza kabisa hawapati nafasi lakini hata wanaopata nafasi huwa wanacheza katika nafasi ngumu. Kwa mfano, kule kwa Waarabu sioni sawa wakinunua walinzi wa pembeni. Hapa ndipo ambapo rafiki zangu kina Mohammed Hussein Tshabalala na Shomari Kapombe wameendelea kusota nchini.
Waarabu wanapenda wageni wanaofanya kazi za punda kama vile mlinzi wa kati, kiungo na mfungaji au washambuliaji wa pembeni hawa kina Miquissone na Tuisila. Rafiki zangu wa pembeni watasubiri sana na ni bahati mbaya kwetu hilo ndilo eneo ambalo tunatawala sana pale Msimbazi.
Maeneo ya mbele wapo wakali wa kigeni. Kando ya John Bocco hakuna mshambuliaji wa ndani ambaye anajitutumua. Na kama Bocco mwenyewe hajaondoka sijui mzawa gani wa eneo la mbele anaweza kutuletea mishahara ya Waarabu.
Kina Ditram Nchimbi, Charles Ilamfya, Waziri Junior na wengineo wapo hoi. Na hata kwa usajili ambao umefanywa na Yanga na Simba dirisha hili unaweza kusikia kina Peter Banda au Fiston Mayele wakaondoka kabla ya wazawa wetu. Wao ndio ambao watapata nafasi ya kucheza mara nyingi.
Kitu cha kwanza kinachohitajika ni wazawa kulazimisha nafasi zao klabuni. Wakishamaliza hapo ndio wataonekana. Hauwezi kuonekana wakati upo benchi. Bahati mbaya kuna wachezaji wetu wameridhika kukaa benchi. Hawana hofu. Tunawaona tu wakitamba Instagram wakati wenzao wanatamba uwanjani.
Tulikosea wapi? Bado ni kitu ambacho najiuliza. Ubora wa wachezaji wetu umepigwa na shoti gani ya umeme? Dhana zimekuwa nyingi. Kwamba hawajitumi mazoezini. Kwamba hawana mazoezi binafsi. Tujiulize wachezaji wa zamani walikuwa wanafanya nini hasa kilichowafanya kuwa bora?
Nafasi ya Chris Mugalu angecheza Edward Chumilla, nafasi ya Fiston Mayele au Michael Sarpong angecheza Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ kwa ufasaha. Tatizo ni kwamba wachezaji wa zamani walikuwa mahiri lakini wagumu kutoka. Wachezaji wa siku hizi wanaweza kutoka lakini wanaishia benchi.
Ninekumbuka jinsi ambavyo Mmachinga na James Tungaraza ‘Boli Zozo’ walikuwa wanamsugulisha benchi Nonda Shabani ‘Papii’ lakini Nonda akachomoka na kwenda kutamba Ulaya. Wao wakabakia katika ardhi yetu. Leo hadithi ni tofauti. Wazawa hata nafasi hawapati.
Wadogo zetu waamke na kupambana. Maisha sio lelemama. Sioni namna yoyote ambayo Simba na Yanga zitaacha kusaka wageni. Wana nafasi za wageni 10 na ndio kwanza wanataka idadi iongezeke kufikia wachezaji 12. Kitu kizuri kwao ni kwamba pesa wanayo.
Tazama ambavyo Metacha Mnata amelichezea lango la Yanga. Alipoondolewa yeye ambaye tulikuwa tunamchukulia kama kipa namba moja, Yanga wakaangukia kwa kipa nambari moja wa Mali. Hii ni jeuri ya pesa. Hatujui mwisho wa Metacha utakuwa vipi.
Kama akienda KMC au Polisi Tanzania unatazamia Waarabu watamuona wapi? Hili ndio tatizo letu. Hata wakati Jonas Mkude alipoleta matatizo ya kinidhamu Simba, basi Waarabu wangemuona kwa urahisi Thadeo Lwanga wakati yeye yuko nyumbani.
Makala haya yameandikwa na Edo Kumwembe na kuchapishwa awali na Mwanaspoti