LICHA ya kumshuhudia kiungo mpya wa Simba, Msenegal Pape Ousmane Sakho, akiichezea timu yake ya Simba kwa mara ya kwanza katika mechi ya kirafiki dhidi ya FAR Rabat juzi, Kocha Mkuu wa miamba hiyo ya Morocco, Sven Vandenbroeck, amesifu ubora wa mchezaji huyo na kumtabiria makubwa ndani ya kikosi .
FAR Rabat, inayonolewa na kocha huyo wa zamani wa Simba, ilicheza mechi ya kirafiki ya kujiandaa na msimu mpya dhidi ya mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara na kulazimishwa sare ya mabao 2-2 juzi nchini Morocco.
Simba ambayo imeweka kambi nchini humo ikijiandaa na msimu mpya, kwa sasa kikosi chake kimeongeza nyota 10 wapya katika dirisha hili la usajili na wote wapo kambini nchini Morocco wakiendelea kujifua na kikosi hicho kitakachopeperusha bendera ya Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Tayari Simba ambayo imewapoteza viungo wake wawili, Luis Miquissone anayetarajiwa kutua Al Ahly ya Misri na Clatous Chama aliyejiunga na RS Berkane ya Morocco, imesajili wachezaji wapya watano wakigeni ambao ni viungo Wamalawi wawili, Peter Banda na Daucan Nyoni, kiungo raia wa Mali, Sadio Kanoute, Sakho na beki Mkongomani Henock Inonga Baka ‘Varane’.
Wachezaji wengine wapya waliosajiliwa katika kikosi hicho ni Watanzania; mshambuliaji Yusuph Mhilu, beki wa pembeni Israel Mwenda, kiungo Jimmyson Mwanuke na Abdulsamad Rabiu.
Akizungumzia mchezo huo baada ya mechi hiyo ya kirafiki, Sven ambaye ni raia wa Ubelgiji, alisifu ubora wa wachezaji wapya waliosajiliwa na timu hiyo kwamba ni wenye morali ya kupambana uwanjani.
“Nimeiona Simba yenye mabadiliko kwenye kikosi, wachezaji wenye umri mdogo na wenye morali ya kupambania timu, kuna mfungaji wa bao la pili (Papa Ousmane Sakho) ni mchezaji bora sana, nadhani atakuwa na mchango mkubwa kwenye timu,” alisema Sven.
Kwa upande wa Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa Didier Gomes, aliwataka mashabiki wa klabu hiyo kuwa wavumilivu kwa kuwa bado kikosi chake kinahitaji kuendelea kuimarika na anaamini kinaweza kufanya vizuri zaidi kadri anavyokiandaa.
“Tunahitaji kuendelea kuimarika na naamini kikosi hiki kinaweza kufanya vizuri zaidi. Tunapaswa kuwa wavumilivu, bado tuna mwezi mmoja wa kujiandaa na nina uhakika timu itakuwa tofauti kabisa baada ya wiki mbili, naiamini timu yangu,” alisema.
Kwa upande wa Meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu, alisema wanafanya mazoezi mara mbili kwa siku na katika mchezo wao wa kirafiki wa juzi ulikuwa ni kama mechi ya kujifua kwa sababu haukuhusisha sana mashabiki.
Alisema walichotaka kukiona katika mchezo huo ni kutazama zaidi kile wachowafundisha wachezaji mazoezini kama wanaweza kukifanyia kazi uwanjani.
Aidha, Rweyemamu alisema mazoezi yanaendelea vizuri na kumeanza kuwa na mabadiliko makubwa kikosini ingawa sasa kumeanza kujitokeza changamoto ya kuwakosa baadhi ya wachezaji wao walioitwa timu zao za taifa.
“Kwa sasa changamoto kubwa tunayoendelea nayo ni kikosi kupungua, timu yetu ina wachezaji wengi wa timu ya taifa, tayari wameanza kupungua kurudi timu zao za taifa, lakini tunaendelea kujipanga kuona tunaweza vipi kulihimili hilo ili tuweze kuendelea na mazoezi na kila kitu kiende vizuri,” alisema Rweyemamu ambaye kitaaluma ni kocha.