NDANI ya saa chache, kila kitu kimebadilika ghafla sana, nyota wa Juventus, Cristiano Ronaldo amebadili maamuzi akiachana na mpango wa kujiunga na Klabu ya Manchester City na kutua kwa waajiri wake wa zamani, Manchester United.
Imeelezwa kuwa kilichofanyika ni umafia wa kiwango cha Phd kumfanya CR7 akatae ofa ya kwenda City na kukubali kurejea Man U.
Inaelezwa kuwa kocha wake wa zamani ambaye Ronaldo mwenyewe amekuwa akisema huyu ni kama baba yake wa pili, Sir Alex Ferguson alidaiwa kuzungumza na nyota huyo kwa njia ya simu na kumfanya abadili kabisa mawazo yake. Nini alimwambia? Ni siri yao wawili.
Lakini saa chache baadaye Man City walitangaza kujitoa kwenye dili hilo la kumuwania nyota huyo mwenye mataji matano ya Ballon d’or.
Aidha, Kocha wa Man U, Ole Gunnar Solskjaer ambaye aliwahi kucheza na Ronaldo miaka ya nyuma kabla ya kustaafu soka amesema:“Sidhani kama Cristiano ataondoka Juventus. Lakini, kama atakuwa anaondoka Juventus, anafahamu sisi tupo. Siku zote tumekuwa na mawasiliano mazuri sana, Bruno Fernandes amekuwa akizungumza naye pia. Anafahamu hisia zetu kwake. Ni gwiji kwenye klabu, ni mchezaji bora wa nyakati zote, hivyo subiri tuone kitakachotokea.”
Kwa upande wake, beki wa kati wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand amethibitisha kuzungumza na CR7 kwa simu, akimuuliza Mreno huyo kipi kinaendelea kabla ya kutumia ukurasa wake wa Twitter kudai dili la kwenda Etihad limekufa na mchezaji huyo anatua Man U.
Kocha wa Man City, Pep Guardiola alisema: “Ninachoweza kusema zimebaki siku tatu au nne, chochote kinaweza kutokea. Lakini, kwa mtazamo wangu ni wachezaji wachache sana, Ronaldo na Messi ndio wanaoamua wapi wakacheze.”
Tayari Juve wamethibitisha kupokea ofa ya Man U huku Man U wakisema tayari wameshakamilisha mazungumzo na Juventus na kinachosubiriwa ni CR7 kutua Man U na kufanya vipimo tu ili ajiunge nao rasmi.
Cristiano ametua Man United kwa ada ya Pauni milioni 25 huku akiripotiwa kusaini mkataba wa miaka miwili hadi mwaka 2023 na mshahara wa Pauni 480,000 kwa wiki.