Home Makala ACHANA NA BILIONI 20..,HAPA TU NDIPO MO DEWJI ALIPOWASHIKA SIMBA SC

ACHANA NA BILIONI 20..,HAPA TU NDIPO MO DEWJI ALIPOWASHIKA SIMBA SC


MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ ameeleza katika miaka minne tangu ameingia Simba ametumia sio chini ya Sh21.3 bilioni. Mo Dewji ameeleza pia amekuwa akikerwa na maneno mengi mitandaoni kwamba hana pesa na uwezo wa kuweka Sh20 bilioni za uwekezaji Simba. Hakuishia hapo alieleza katika kila mwaka amekuwa akitumia si chini ya Sh5.3 bilioni kuhakikisha timu inafanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali.

Katika kuhakikisha anawafunga midomo waliokuwa wakimbeza majuzi alitoa hudi ya Sh20 bilioni mbele ya waandishi wa habari.

Baada ya kumaliza jambo lake hilo Mwanaspoti limefanya uchambuzi wa Sh21 bilioni vitu vilivyomfanya Mo kutumia pesa hiyo ndefu.

BENCHI LA UFUNDI

Wakati Mo Dewji anaingia Simba ilikuwa chini ya kocha Joseph Omog aliyeondolewa siku moja mbele baada ya timu hiyo kufungwa mechi ya Kombe la Shirikisho (ASFC).

Katika mechi hiyo iliyochezwa Desemba 21, 2017, Simba ilifungwa na Green Worriors kwa penati huku wakiwa na kumbukumbu ya kutoka kuchukua ubingwa msimu uliopita.

Baada ya kuachana na Omog ambaye alilipwa kila stahiki na Mo aliajiriwa Mfaransa Pierre Lechantre aliyefanya kazi na msaidizi Masoud Djuma. Baada ya msimu mmoja kwisha Simba wakiwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza baada ya misimu minne nyuma Yanga na Azam wakipishana waliachana na Lechantre.

Simba walishindwa kuendelea na Lechantre kutokana na mahitaji yake si chini ya Sh100 milioni jambo ambalo hawakuwa tayari kumpatia.

Alipoondoka Mo Dewji alimuajiri Patrick Aussems ambaye alifanya kazi na msaidizi wake Denis Kitambi baada ya kushindwa kuishi na Djuma.

Aussems na Kitambi walidumu mwaka mmoja na zaidi, kisha waliondolewa timu hiyo ilipoishia hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mo alimwajiri Sven Vandenbroeck aliyefanya kazi mwaka mmoja ambali aliivusha timu hiyo hatua ya makundi na aliondoka bila kutarajiwa. Sven alifanya kazi na msaidizi Selemani Matola na licha ya mafanikio hayo aliondoka kwa kushtukiza na kwenda kufanya kazi nchini Morocco.

Katika kuhakikisha Simba inafanya vizuri Mo alimwaga mkwanja kumwajiri Didier Gomes ambaye yupo mpaka sasa. Ingia toka ya makocha katika kikosi cha Simba Mo amekuwa akitumia pesa ndefu.

USAJILI

Tangu ameingia Mo Dewji miaka minne Simba imeshuhudiwa ikisajili wachezaji bora katika viwango bora ndani na nje.

Wachezaji waliosajiliwa ni wengi, lakini baadhi niJohn Bocco, Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohamed Hussein, Clatous Chama, Meddie Kagere, Luis Miquissone na Joash Onyango

Mo Dewji ameweka rekodi ya kutoa zaidi ya Sh230 milioni kuwapata kina Chama, Luis, Chriss, Mugalu, Rally Bwalya, Taddeo Lwanga na wengineo wengi.

Wachezaji hao wamekuwa msaada mkubwa kuhakikisha Simba inafikia lengo la kuchukua mataji nchini – Ligi Kuu mara nne mfululizo na ASFC mara mbili.

Kama haitoshi mchezaji kama Kagere ameibuka mfungaji bora mara mbili, ilhali Bocco amechukua tuzo hiyo msimu huu huku Chama akifunga mabao muhimu katika mashindano ya kimataifa – yaani rekodi kibao ambazo kama si pesa za Mo Dewji basi Simba wasingekuwa na wachezaji daraja hilo. Katika usajili Simba imewapora wachezaji wazuri wapinzani wao Yanga kutokana na jeuri ya pesa.

SOMA NA HII  UKWASI WA MO DEWJI NI BALAA...ANAWEZA KUJENGA UWANJA NA KUINUNUA YANGA YOTE NA CHENJI IKABAKI...

PRE – SEASON

Kabla ya Mo Dewji kuingia Simba wakati wa maandalizi ya msimu (pre Season), walikuwa wanaenda Lushoto – Tanga au maeneo mengine ya ndani ya nchi, lakini baada ya kuingia wamekuwa wakibadilisha tu anga – wameenda Afrika Kusini mara mbili na msimu wa 2018-19 walikwenda Uturuki.

Kama haitoshi Jana Simba SC wameenda nchini Morocco kuweka kambi kwa maandalizi ya msimu ujao.

KAMBI

Kabla ya kuingia Mo kikosi cha Simba kilikuwa kinaishi na kukaa katika kambi zenye hadhi ya kawaida, lakini chini ya tajiri huyo ni tofauti.

Simba wakienda nje ya nchi kucheza mechi za kimataifa au kuwa maandalizi ya msimu wanaweka kambi hoteli ambayo chumba kimoja kinalipiwa si chini ya Sh230,000.

Ukiangalia kambi ambayo Simba wanaishi sasa ni ya maana, wakienda kucheza mechi nje ya Dar wanaishi katika hoteli ya maana na yote hiyo ni jeuri ya Moi.

BONASI

Kabla ya kuingia Mo kikosi cha Simba hakikuwa na bonasi kubwa za maana ambazo wachezaji walikuwa wanachukua baada ya kushinda mechi au kufanya vizuri.

Chini ya Mo kila wanaposhinda mechi ukiondoa zile za Yanga na Azam kunakuwa na Sh10 milioni ambayo wachezaji hugawana.

Katika mechi za Azam kama wakishinda hupewa Sh50 milioni wakati zile za Yanga si chini ya Sh200 milioni. Kwenye mechi za kimataifa kama wakifanya vizuri kila mmoja anaweza kuchukua Sh10 milioni kama ilivyokuwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Ahly msimu huu.

VIWANJA VYA MAZOEZI

Kabla ya Mo kikosi cha Simba walikuwa kilkuwa kinafanya mazoezi viwanja vya kulipia kama Klabu ya Gymkhana na kwa dakika 90 si chini ya Sh2.5 milioni ambazo alikuwa akilipa.

Simba walikuwa wanafanya mazoezi Uwanja wa Boko Veterans ambao kwa awamu moja Mo alikuwa akilipa Sh300,000. Mbali ya gharama hizo wachezaji walifanya mazoezi katika viwanja vya kawaida kama Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDS), Kinesi, TTC Chang’ombe na Bandari.

USAFIRI

Kwa nyakati tofauti kabla ya Mo Dewji kuingia Simba walikuwa wanasafiri kwa basi kutoka Dar mpaka Mbeya kucheza mechi ya mashindano. Tangu ameingia Simba kusafiri kwa basi mwisho ni Morogoro na maeneo mengine yote amekuwa akimwaga mkwanja mrefu wachezaji na viongozi wanapanda ndege kwenda na kurudi.

MISHAHARA

Eneo lingine ambalo Mo Dewji amekuwa akitoa pesa ndefu kila mwisho wa mwezi ni katika mishahara ya waajiriwa na amekuwa akimwaga mkwanja wa maana.

Ni ukweli usiopingika mnyonge mnyongeni, lakini haki yake Mo Dewji anastahili kupewa ndani ya Simba mpaka inakuwa moja ya timu kubwa na inayozungumziwa Afrika barani Afrika.