Home Yanga SC USAJILI WA YANGA NA TAFSIRI YA ALBERT EINSTEIN KUHUSU WENDAWAZIMU

USAJILI WA YANGA NA TAFSIRI YA ALBERT EINSTEIN KUHUSU WENDAWAZIMU


DUNIA imewahi kushuhudia watu wengi maarufu waliopata kuibukia katika taaluma mbalimbali. Katika ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia mwaka 1879 alizaliwa mtu mmoja maarufu aitwaye Albert Einstein.

Einstein amekuwa maarufu sana hata baada ya kifo chake kilichotokea mwaka 1955, hii ni kutokana na kuwahi kufanya mambo mengi yaliyowashangaza watu. Kuna wakati mtu huyu maarufu aliwahi kusema “Wendawazimu ni kufanya kitu kilekile kila wakati, huku ukitegemea matokeo tofauti.”

Bila shaka unaweza kujiuliza ni kwanini nimeanza na stori hii? Subiri nitakuelewesha, kwa sasa kwenye Ulimwengu wa soka maeneo mbalimbali, ligi zimeshamaliza na kinachoendelea ni maandalizi ya kabla ya msimu ‘Pre-season’, pamoja na masuala ya usajili ambayo ndiyo habari ya mjini.

Kwetu hapa Tanzania unapozungumzia usajili basi huwezi kuacha kuzitaja klabu za Simba, Yanga na Azam ambazo mara zote zimekuwa zikivuta hisia za wadau wengi wa soka.

Kama ilivyokuwa msimu uliopita, msimu huu pia Mabingwa wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara klabu ya Yanga, wameteka stori za usajili kutokana na kushusha majembe yenye majina makubwa kuelekea msimu ujao.

Mpaka sasa Yanga wametambulisha mastaa watano wapya ambapo wanne kati ya hao ni wachezaji wa Kimataifa ambao ni; Fiston Mayele, Heritier Makambo, Khalid Aucho, Djigui Diarra na mshambuliaji mzawa Rajab Athuman.

Yanga pia wametangaza kuachana rasmi na makipa wao wawili Faroukh Shikalo na Metacha Mnata, huku wakijiandaa kutangaza kuachana na nyota wengine zaidi ya watano wa kimataifa.

Ukumbuke pia katika hili wapo nyota wengi wazawa ambao wanatarajiwa kupewa mkono wa kwaheri, kutokana na kushindwa kuonyesha kiwango kilichotarajiwa.

Kitu wanachokifanya Yanga kwa sasa ni kama marudio ya kile ambacho kilifanyika msimu uliopita, ambapo Yanga waliachana na rundo la mastaa ambao kwa idadi walikuwa wanafika wachezaji 17.

Umegundua kitu? Kama hujagundua basi hapa ndipo tunaporejea maneno ya Mwanasayansi, Einstein kuhusiana na tafsiri ya Uwendawazimu.

Kuna kitu hakipo sawa kwenye Kamati ya usajili ya Yanga, haiwezekani kwa misimu miwili tu waachane na zaidi ya wachezaji 17, ambao hawakumaliza mikataba yao, kutokana na kushindwa kuthibitisha ubora wao.

SOMA NA HII  DOUMBIA NA YANGA MPAKA KIELEWEKE ISHU IKO HIVI

Yanga kwa matumaini makubwa waliuanza msimu uliopita wa 2020/21, hii ni baada ya kuwa na safari nyingi za kwenda pale Terminal 3 ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere kwa lengo moja kubwa la kuwapokea wachezaji wao wapya.

Baadhi ya mashabiki hawa walidiriki hata kukubali kutengeneza mistari kama vile Wanajeshi wanaojiandaa na Gwaride, ili wachezaji hao wapya wapite.

Mwezi Agosti ulipoisha na kelele za mapokezi ya wachezaji kusahaulika, mwezi Septemba ukafika na Ligi ikaanza, hapo ndipo kasheshe ikaanza kwani mchezo wa kwanza tu Yanga wakatoa sare kwenye dimba la Benjamin Mkapa dhidi ya Tanzania Prisons, Wananchi wakajipa moyo kuwa kuteleza si kuanguka.

Baada ya hapo Yanga wakacheza michezo mitatu, ya ushindi ambao kwa jicho la tatu ulikuwa haupendezi kwani timu ilikuwa ikicheza bila kuwa na plani inayoeleweka na kuonekana wazi wamekosa muunganiko, hivyo kusababisha malalamiko kuanza.

Mchezo wa tano tu ukatosha kumfungulia njia ya kutokea kocha Mserbia, Zlatko Krimpotic na nafasi yake kuchukuliwa na Cedric Kaze. Kaze akaibadilisha Yanga na kurudisha muunganiko wa kitimu licha ya kupata shida kupata matokeo ya ushindi.

Kaze akaipa Yanga kombe la Mapinduzi tena kwa kuwafunga Simba kwenye fainali januari 13, mwaka huu, huku akipoteza mchezo mmoja pekee, lakini ushindi mmoja katika michezo sita iliyopita kumewaibua viongozi wa Yanga na kuamua kuwaondoa.

Lakini unaweza kujiuliza tatizo la Yanga liko wapi? Ni kweli kulikuwa na shida ya benchi la ufundi? Au shida ipo kwa madaraja ya wachezaji walionao? Na vipi kuhusu uthabiti wa Uongozi?

Bila shaka hapa ndipo tunabaki na swali gumu zaidi, juu uthabiti wa mbinu za usajili zinazotumiwa na Yanga kuleta wachezaji wapya, bila shaka ligi itakapoanza Yanga itakuwa na deni kubwa la kutuonyesha utofauti wa kilichofanyika kwenye usajili wa mwaka jana na wa mwaka huu.

Ikiwa watarudia makosa yaleyale basi sisi tutarudi kwa Mwanasayansi, Einstein na tafsiri yake ya Wendawazimu.