Home Yanga SC WASOMALI, WAGHANA WAPEWA MFUPA WA YANGA KIMATAIFA

WASOMALI, WAGHANA WAPEWA MFUPA WA YANGA KIMATAIFA


Marefa nane kutoka nchi za Somalia na Ghana wamepangwa kuchezesha mechi mbili za raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu zitakazokutanisha wawakilishi wa Tanzania, Yanga na Rivers United mwezi ujao.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limepanga waamuzi wanne kutoka Somalia kuchezesha mechi ya kwanza baina ya timu hizo itakayochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Septemba 12, kuanzia saa 11 jioni

Refa Hassan Mohamed Hagi ndiye atakayesimama katikati na atasaidiwa na Suleiman Bashir na Ali Mohamud Mahad huku refa wa akiba akiwa ni Ahmed Hassan Ahmed wote wakitoka huko Somalia

Kamishna wa mchezo huo atakuwa ni Lewis Madeleine kutoka Shelisheli huku Ofisa Vipimo wa Uviko-19 akipangwa Violet Michael Lupondo wa Tanzania.

Katika mchezo wa marudiano baina ya timu hizo mbili utakaochezwa Septemba 19 huko Port Harcourt, Nigeria, refa wa kati atakuwa ni Adaari Abdul Latif ambaye atasaidiwa na Waghana wenzake Paul Atimaka, Patrick Papala na Kwame Sefah atakayekuwa mezani.

Sullay Kamara kutoka Sierra Leone ndiye amepangwa kuwa kamishna wa mchezo na ofisa wa vipimo vya Uviko-19 atakuwa ni Ozi Salami Onimisi  wa Nigeria.

Timu itakayopata matokeo mazuri katika mechi mbili baina ya Yanga na Rivers United, itasonga mbele na kutinga katika hatua ya kwanza ambako itapambana na mshindi kati ya Fasil Kenema na Al Hilal

Wakati huohuo marefa wanne wa Tanzania wamepangwa kuchezesha mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya Mogadishu City ya Somalia na APR ya Rwanda utakaochezwa Septemba  12 huko Djibouti

Ramadhan Kayoko ndiye atakuwa mwamuzi wa kati ambapo atasaidiwa na Frank Komba na Soud Lila huku refa wa akiba akiwa ni Mfaume Ali Nassoro.

Katika hatua nyingine Watanzania wawili wameteuliwa kuwa maofisa wa mechi mbili tofauti za mashindano hayo

Msafiri Mgoyi amepangwa kuwa kamishna wa mechi kati ya Zesco United ya Zambia na Royal Leopards ya Eswatini, Septemba 18 wakati Hamid Al-Busaidy atakuwa ofisa wa vipimo vya Uviko-19 katika mchezo baina ya KMKM na Al Ittihad utakaochezwa Septemba 19 kwenye Uwanja wa Amaan huko Zanzibar.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI NA WANIGERIA....EDO KUMWEMBE AIPASUKIA UKWELI YANGA...ATAJA YA TAIFA STARS...