ZIKIWA zimebaki siku tatu kwa sasa mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Simba v Yanga uchezwe Uwanja wa Mkapa habari zinaeleza kuwa bado mwamuzi wa mchezo huo ni pasua kichwa.
Habari kutoka chanzo cha kuaminika zimeliambia Spoti Xtra kuwa mpaka sasa haijajulikana siku ya kufanya kikao kwa ajili ya kujadili waamuzi ambao watachezesha mchezo huo.
“Mchezo upo ila mpaka sasa bado haijaamuliwa ni nani atakuwa mwamuzi wa mchezo huo pia haijafahamika siku ya kukutana kuweza kujadili kuhusu mwamuzi kwani mambo bado,” ilieleza taarifa hiyo.
Ikumbukwe kuwa Agosti 30,2020 katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mwamuzi wa kati alikuwa ni Ramadhan Kayoko, alishirikiana na Mohamed Mkono, Ahmed Arajiga, Ramadhani Mwinyimkuu na Abubakari Mturo waliweza kuamua mchezo uliopita.
Katika mchezo huo ni Simba ilishinda kwa mabao 2-0 mbele ya Namungo iliyokuwa chini ya Kocha Mkuu, Hitimana Thiery ambaye kwa sasa yupo ndani ya Simba.
Hivi karibuni, Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania,(TFF), Cliford Ndimbo aliliambia Spoti Xtra kuwa maandalizi yanakwenda vizuri kuelekea mchezo huo jambo ambalo lilisababisha mpaka tarehe ya mchezo huo kutangazwa mapema.