BEKI wa kati wa Yanga, Bakari Mwamnyeto amefunguka na kuelezea mipango yao kuelekea Dabi ya Kariakoo dhidi ya watani zao,mnyama Simba itayopigwa wikiendi hii Uwanja wa Mkapa mkoani Dar.
Watani hawa wa jadi Yanga na Simba wamekutana mara nne kwa mwaka huu na hii ya Ngao ya Jamii itakuwa ya tano huku Yanga akiwa na rekodi nzuri kwa kushinda mara mbili na Simba moja pia wametoka sare mara moja.
Akizungumza na Championi Jumatano Mwamnyeto alisema: “Tumejipanga kama tunavyojipanga siku zote katika kila mechi ila tunajua mchezo huu utakuwa ni mgumu na siku zote haijawahi kuwa rahisi tukikutana na mtani.
“Imetuuma sana sisi kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa ila haina budi tumekubali matokeo tunaangalia mbele maana yameshapita tayari.”
Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi iliondolewa hatua ya awali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufungwa jumla ya mabao 2-0 na Rivers United ya Nigeria.
Inakutana na Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes ambaye yeye anakumbuka kwamba mchezo wake uliopita alipoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya TP Mazembe ila ulikuwa ni mchezo wa kirafiki.