Home news BAADA YA SIKU YA WANANCHI NA SIMBA DAY..MASAU BWIRE AIBUKA NA USIKU...

BAADA YA SIKU YA WANANCHI NA SIMBA DAY..MASAU BWIRE AIBUKA NA USIKU WA RUVU SHOOTING

 


KLABU ya Ruvu Shooting imezindua tamasha maalumu lijulikanalo kama ‘Usiku Wa Ruvu Shooting’ litakalofanyika usiku wa Septemba 25, Mkoani Pwani.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Ruvu Shooting, Masau Bwire amesema lengo kuu la tamasha hilo ni kutambulisha wachezaji wote watakaoitumikia timu hiyo na kutoa misaada mbalimbali kwa watu wenye uhitaji maalumu.

“Wengi wanaweza kusema tumeiga kwa hizi klabu za Kariakoo lakini tulishaandaa mpango huo tangu Ligi ilipoisha hivyo tunatimiza kile tulichokiahidi kwa mashabiki na wadau wetu,” amesema.

Kabla ya tamasha hilo Masau amesema Klabu hiyo itatembelea hospitali mbalimbali nchini kwa lengo la kutoa misaada kwa wagonjwa.

“Sisi kama viongozi tunajua changamoto zinazowakabili wagonjwa, hivyo tumejipanga kutoa misaada kidogo kwa tulichobarikiwa na Mwenyezi Mungu, ” amesema.

Aliendelea kuwa baada ya hapo kutakuwa na mchezo wa kirafiki ili kutoa fursa kwa wakazi wa Mkoani Pwani kuiona timu yao ilivyojiandaa  kwa msimu ujao.

“Tunatarajia kucheza na Mlandizi Kombaini kama mapendekezo ya benchi letu la ufundi likiongozwa na Kocha wetu mkuu Mkwasa ili kujiandaa vyema kabla ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuanza,” amesema.

Katika tamasha hilo Ruvu Shooting itatambulisha wachezaji wote 29, watakaoitumikia Klabu hiyo kwa msimu ujao.

“Utambulisho wetu utakuwa wa tofauti kidogo na wengine maana sisi tutaelezea historia ya kila mchezaji alipotoka mpaka kufikia hapa kwetu, tofauti na wengine wanaotambulisha wachezaji ki ujanja ujanja tu “amesema.

Masau aliwasihi viongozi na wadau wa michezo nchini kujitokeza kwa wingi ili kujifunza namna ya kuendesha tamasha hilo na kuzitaka timu nyingine kuiga kutoka kwao.

“Tutakuwa na viongozi mbalimbali kutoka TFF, na Bodi ya Ligi lakini niwaombe pia viongozi wa Klabu hapa nchini kujitokeza ili kujumuika nasi katika siku yetu muhimu,” amesema.

Katika hafla hiyo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu Wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.

DOGO ASLAY, DULLY SYKES KUNOGESHA

Katika tamasha hilo wasanii mbalimbali wa kizazi kipya watatumbuiza wakiongozwa na Dully Sykes, Dogo Aslay, Nikki Mbishi, Tunda Man na Dullah Makabila.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI CHAMPIONI JUMATATU