Home Makala EDO KUMWEMBE ATUPA DONGO YANGA…AWATAJA MAKAMBO NA DJUMA SHABANI

EDO KUMWEMBE ATUPA DONGO YANGA…AWATAJA MAKAMBO NA DJUMA SHABANI


HERITIER Makambo juzi aliwaonyesha Yanga kile ambacho anaweza kufanya. Hapana, tuseme aliwakumbusha. Tangu alipoondoka Jangwani miaka miwili iliyopita Yanga haikuweza kupata mshambuliaji wa aina yake mpaka hivi sasa amerudi tena.

Alifunga bao maridadi katika jioni ambayo Yanga walitaka kuhitimisha siku yao ya Wananchi vyema, lakini baadaye mambo yakageuka. Wakafungwa mabao mawili katika kipindi cha pili na Zanaco. Siku yao haikuisha kwa mbwembwe kama ilivyoanza.

Ni kitu nilichokitegemea. Kile alichoonyesha Makambo ni uwezo binafsi. Na walichoonyesha wachezaji wengi wa Yanga ni uwezo binafsi. Zanaco walionyesha mambo mawili au matatu. Uwezo binafsi, uwezo wa kitimu na ubora wa matumizi ya nguvu na stamina.

Hili la tatu halikuwepo Yanga. Nilikuwepo katika kambi yao ya Morocco hivi karibuni na nilifahamu kwamba ingechukua muda kwao kufikia kiwango cha matumizi ya nguvu na stamina kama ilivyo kwa wapinzani wao wa juzi kutoka Zambia.

Yanga haikuwa na kocha wa viungo pale Morocco. Aliyekuwepo awali amemaliza mkataba wake. Walitaka kuchukua kocha kutoka Tunisia, lakini alishindwa kuingia nchini Morocco kwa sababu mbalimbali. Baadaye wakaajiri kocha wa muda katika jiji la Marrakech akawasaidia kiasi.

Kabla hajawasaidia vizuri Yanga wakakatisha ziara Morocco baada ya kupata changamoto. Likarudi kundi la kwanza kisha likarudi kundi la pili. Hili la pili lililoongozwa na Djuma Shabani liliwasili Jumamosi mchana. Saa chache kabla ya pambano la Jumapili. Nilishangaa kumuona Djuma uwanjani ingawa alicheza vyema.

Na sasa wamempata huyo kocha wa Tunisia. ‘Fitness’ ya wachezaji wa Yanga bado ipo chini. Ungeweza kuona katika pambano la juzi. Lakini hapohapo ongeza kwamba kocha wao, Mohamed Nabi ana kazi ya kuiunganisha timu iwe kitu kimoja. Sina wasiwasi sana na hili kwa sababu tayari ana wachezaji bora. Kuunganisha wachezaji bora sio kazi ngumu.

Tatizo ni kwamba Nabi ana muda mfupi mkononi. Ana bahati kwamba karibu wachezaji wote wa DR Congo kasoro Tonombe Mukoko hawatakuwepo katika kikosi cha timu ya taifa. Na ana bahati pia kwamba ana kundi kubwa la wachezaji ambao hawapo katika vikosi vya timu ya taifa.

SOMA NA HII  YANGA YAPIGA HESABU YA KUTWAA MAKOMBE

Kabla ya kucheza na Wanigeria Yanga wanahitaji kucheza mechi walau mbili za kirafiki za kujifungia. Wanaweza kwenda Chamazi na kuwa-omba Azam uwanja walau wacheze mechi za kujifungia zisizo na mashabiki wala kamera.

Sikuwepo katika kambi ya Simba lakini wana faida mkononi. Wamecheza mechi mbili za kirafiki wakiwa nchini Morocco na ingawa matokeo hayakuwa muhimu kwao lakini moja kwa moja wameanza kujua shepu ya timu yao.

Yanga wamecheza mechi ya pili ya kirafiki na ilikuwa ngumu haswa. Ile ya awali ya mazoezini baada ya kurejea kutoka Morocco, Yanga walishinda 3-1 dhidi ya timu ya Daraja la Kwanza ya DTB ya kina Amisi Tambwe.

Yanga Kama wangekuwa na muda kabla ya kwenda hadharani walipaswa kucheza mechi za kujifungia. Hawakuwa na muda. Lakini sasa kabla ya kucheza na Wanigeria wanapaswa kujifungia mahala na kucheza na timu tofauti zinazojiandaa na Ligi Kuu. Pambano lao dhidi ya watani wa jadi Simba lipo mbali na halina umuhimu zaidi ya kulinda heshima. Kufikia hapo watakuwa wamecheza mechi mbili dhidi ya Wanigeria. Watakuwa wame-pasha miili yao moto vya kutosha. Tatizo ni hili pambano lao la kwanza dhidi ya Nigeria.

Makala haya yameandikwa na Edo Kumwembe na kuchapishwa kwenye gazeti la Mwanaspoti