KASI ya kusaka pointi tatu inaendelea ndani ya Ligi Kuu Bara ambapo tayari mzunguko wa pili umekamilika na sasa ni hesabu kuufuata ule mzunguko wa tatu ili kujua nani atazidi kuwa nani kwa kuwa mpaka sasa picha linaonyesha kwamba ushindani ni mkubwa na kila dakika rekodi tamu zinaandikwa.
Ikumbukwe kwamba katika mzunguko wa kwanza yalikusanywa jumla ya mabao 10 pekee katika viwanja nane tofauti na timu mbili zilishinda mabao mengi ambazo ilikuwa ni Namungo 2-0 Geita Gold na Polisi Tanzania 2-0 KMC.
Sasa kwa upande wa mzunguko wa pili jumla mabao 12 yamekusanywa kwenye viwanja nane tofauti ambavyo vimetumika huku ile rekodi ya timu kufunga mabao mengi ikiwa haijavunjwa kwa sasa ikibaki kuwa vilevile mabao 2-1 ambayo ni Polisi Tanzania iliwatungua Azam FC.
Kwa upande wa mechi iliyokusanya mabao mengi ni ile Dabi ya Mbeya iliyowakutanisha Mbeya City v Mbeya Kwanza Uwanja wa Sokoine baada ya dakika 90 kukamilika ubao ulisoma Mbeya City 2-2 Mbeya Kwanza na kufanya jumla yafungwa mabao manne kwenye mchezo mmoja.
Pia mchezo huo kwa msimu wa 2021/22 umetoa bao bora la mzunguko wa pili ambalo ni la mtindo wa tikitaka wengi hupenda kuita Acrobatic lilifungwa na Crispine Ngushi dakika ya 86 na kufanya timu hizo kugawana pointi mojamoja.
Ngushi aliweza kukimbizwa hospitali kupewa huduma ya kwanza baada ya kuzimia kutokana na kuonekana kupata mtikisiko kwenye ubongo kwa sababu alibinuka wakati wa kufunga na aliweza kufanya hivyo wakati wa kushangilia.
Taarifa rasmi kutoka Mbeya Kwanza kupitia kwa daktari wa timu imeeleza kuwa tayari nyota huyo ameungana na timu kambini kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa 2021/22.
Pia ni Eliud Ambokile kwenye mzunguko wa pili aliweza kukosa penalti dakika ya tatu baada ya kipa wa Mbeya Kwanza Hamad aliyeweza kuikoa penalti hiyo na kuliweka lango la Mbeya Kwanza salama.
Kwa mzunguko wa kwanza ilikuwa ni John Bocco wa Simba alikosa penalti mbele ya Biashara United na iliokolewa na kipa James Ssetuba ilikuwa Uwanja wa Karume, Mara.
Kwa upande wa mabingwa watetezi, Simba waliweza kupata ushindi wa kwanza mbele ya Dodoma Jiji baada ya ushindi wa bao 1-0 ambalo lilifungwa na Meddie Kagere dakika ya 69 kwa pasi ya Chris Mugalu.
Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Jamhuri,Dodoma ilishuhudiwa kadi ya kwanza nyekundu ikitolewa na mwamuzi Joseph Akamba kwa kijana Anuary Jabir wa Dodoma Jiji baada ya kuonekana akimpiga kiwiko beki Kened Juma.
Yanga mabingwa mara 27 waliendelea ushindi mbele ya Geita Gold kwa ushindi wa bao 1-0 Uwanja wa Mkapa na ikumbukwe kwamba mzunguko wa kwanza walishinda bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, Uwanja wa Kaitaba.
Mtibwa Sugar ya Morogoro, KMC ya Kinondoni, Azam FC ya Dar, Biashara United ya Mara, Coastal Union ya Tanga,Geita Gold ya Mwanza, Kagera Sugar ya Bukoba na Tanzania Prisons kutoka Songea mpaka sasa hazijaonja ladha ya kusepa na pointi tatu mazima kwenye mechi zao ambazo wamecheza.
Matokeo yalikuwa namna hii:-Dodoma Jiji 0-1 Simba, Biashara United 0-1 Ruvu Shooting,Coastal Union 0-0 KMC, Polisi Tanzania 2-1 Azam FC,Yanga 1-0 Geita Gold,Mtibwa Sugar 0-0 Prisons, Mbeya City 2-2 Mbeya Kwanza na Namungo 1-1 Kagera Sugar