Home news BAADA YA KUIBUKA NA USHINDI WA MBINDE DHIDI YA POLISI TZ…HITIMANA AIBUKA...

BAADA YA KUIBUKA NA USHINDI WA MBINDE DHIDI YA POLISI TZ…HITIMANA AIBUKA NA HILI KWA WACHEZAJI WA SIMBA

 


Kaimu Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Hitimana Thierry amesema haikuwa kazi rahisi kuifunga Polisi Tanzania katika mchezo wa jana Jumatano (Oktoba 27), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Hitimana ambaye amekabidhiwa jukumu la kukaimu nafasi ya Kocha Mkuu baada ya kuondoka kwa Kocha Didier Gomes, amesema suala kubwa lililokua mbele yao katika mchezo huo ni kupata ushindi, lakini walikabiliwa na upinzani mkubwa.

Kocha huyo kutoka nchini Rwanda amesema mpinzani mkubwa wa Simba SC katika mchezo huo uliomalizika kwa ushindi wa bao 1-0, alikua ni wao wenyewe, kwani wachezaji wake walicheza kwa Presha kubwa, kutokana na hitaji la ushindi.

Amesema hatua ya kuondoshwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kufungwa mabao 3-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy, ilichochea Presha kwa wachezaji wake, lakini hana budi kumshukuru Mungu kwa kupata ushindi huo.

“Mpinzani wetu wa kwanza alikuwa sisi wenyewe, tumecheza kwa presha kubwa kwakua tulihitaji sana ushindi. Tumetoka kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika pia tumefanya mabadiliko makubwa katika benchi la ufundi kwa muda mfupi ndiyo maana tulikuwa na Presha lakini kikubwa tumepata alama tatu muhimu,” Amesema Hitimana Thierry.

Bao la Simba SC katika mchezo huo lilipachikwa wavuni na kiungo kutoka nchini Zambia Larry Bwalya kwa mkwaju wa Penati iliyosababishwa na Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison dakika ya 86.

Ushindi huo umeipeleka Simba SC hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2021/22, kwa kufikisha alama 7, ikitanguliwa na Polisi Tanzania na Young Africans zenye alama 9.

Simba SC itacheza tena mchezo wa Ligi Kuu Jumapili (Oktoba 31) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam dhidi ya Coastal Union kutoka jijini Tanga.

SOMA NA HII  EDO KUMWEMBE: NILISHANGAA SIMBA WALIPOMSAJILI KISUBI...AFUNGUKA ISHU YA NKANE NA YANGA...