Home Habari za michezo ISHU YA NANI ‘MWAMBA’ KATI YA CHAMA NA PACOME KUAMULIWA NA CAF….ISHUU...

ISHU YA NANI ‘MWAMBA’ KATI YA CHAMA NA PACOME KUAMULIWA NA CAF….ISHUU IKO HIVI…

Habari za Michezo leo

Ilianza mvua ya kawaida alfajiri ya juzi Jumamosi na ilipofika usiku kukawa na mvua ya mabao kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa pale Temeke. Ndio, historia iliwekwa tena na Mnyama wakati alipokuwa akiisaka robo fainali yake kwa mara nyingine.

Lakini historia zaidi ikawekwa pale kwa mara ya kwanza Tanzania ilipopeleka timu mbili kwa mpigo katika hatua ya robo fainali. Wababe wa Kaskazini wameshindwa kufanya hivyo. Mafarao wameshindwa kufanya hivyo. Wamorocco wameshindwa kufanya hivyo. Tanzania inayopatikana huku Afrika Mashariki imeweza.

Ni siku ambayo Clatous Chama alikwenda uwanjani huku akijua ambacho kitamkabili. Sawa kila mchezaji aling’ara lakini Chama kama kawaida yake katika hatua hizi aliiweka Simba katika mabega na kuendesha shoo kabambe ambayo Wanasimba waliitarajia. Aliendesha shoo ambayo ilimziba mdomo kocha wa Jwaneng Galaxy, Morena Ramoreboli ambaye siku tatu zilizopita aliongea maneno machafu dhidi ya Simba.

Chama alihusika karibu katika kila bao ambalo Simba waliuweka mpira katika wavu wa Jwaneng. Sidhani kama kuna mchezaji mtulivu katika eneo la mwisho Ligi ya Mabingwa wa Afrika anayeweza kumfikia Chama. Anajua namna ya kutengeneza nafasi kwa wenzake. Anajua. Anaweza. Ni fundi haswa.

Hakukuwa na namna ambayo Jwaneng wangeweza kunusurika Taifa. Wiki moja kabla mtani Yanga alikuwa ametangulia robo fainali, huku akiwa na mechi moja mkononi ambayo aliicheza kirafiki dhidi ya Al Ahly pale Cairo saa 24 kabla Mnyama hajaingia uwanjani. Lakini kulikuwa na kesi ya kisasi dhidi ya Makhirikhiri hawa kutoka Botswana.

Simba ikiongozwa na Chama ilifanya kila kitu kwa usahihi. Haikutaka kurudia makosa iliyofanya dhidi ya Jwaneng miaka michache iliyopita. Iliongoza mabao 2-0 pale Gaborone halafu ikafungwa mabao 3-1 hapa hapa Temeke. Tena katika kichapo hicho wao ndio walipata bao la kuongoza.

Safari hii Simba hawakufanya makosa. Walijihami kwa usahihi, walimiliki mpira kwa usahihi, walitengeneza nafasi zao kwa usahihi, na wakazitumia kwa usahihi. Kama Wydad walikuwa wanasubiri kitu chochote kutoka kwa Jwaneng basi walikuwa wanajidanganya. Walikutana na Mnyama mkali. Ndani ya dakika 14 tu Mnyama alikuwa anaongoza kwa mabao mawili.

Wakati watani wao wakiongozwa na mtu anayeitwa Pacome Zouzoua kufika robi fainali, Simba wamefika wakiwa na mtu anayeitwa Clatous Chama. Na sasa ni wakati wa kujua nani atakuwa mwanaume zaidi wa kuipeleka timu yake katika hatua ya nusu fainali. Mara ya mwisho kwa timu ya Tanzania kufanya hivi ilikuwa mwaka 1974 na walikuwa ni Simba wenyewe.

Sawa ulikuwa ni katika mfumo tofauti na huu lakini walifika nusu. Sawa, walicheza mechi chache kufika nusu fainali lakini bado walifika nusu fainali. Ni kama ambavyo mwaka 1998 Yanga walitinga hatua ya robo fainali kwa kutinga tu katika makundi. Mfumo ulikuwa tofauti na huu.

Na sasa mwanaume zaidi ni yule ambaye ataipeleka timu yake nusu fainali. Ni miaka 50 sasa. Na tangu tuingie katika mfumo mpya hakuna timu ya Tanzania ambayo imewahi kutinga hatua ya nusu fainali. Nani ataenda, Simba au Yanga au wote? Natamani iwe wote.

Kama Yanga atakwenda na Simba atabakia basi utakuwa wakati mgumu kwa Simba. Kwa miaka mingi mfululizo wamecheza robo fainali. Iweje Yanga waende robo fainali yao ya kwanza ya zama hizi na wapitilize mpaka nusu fainali kitu ambacho wao wameshindwa kukifanya kila uchao katika miaka ya karibuni?

Litakuwa tusi jingine kwa Simba baada ya mtani kupitilizs moja kwa moja fainali za Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita licha ya wao kujitanabaisha kwamba ni Wakimataifa zaidi kuliko Yanga. Ni kitu ambacho kiliwaumiza Wanasimba licha ya kwamba walijaribu kukejeli kwamba ilikuwa michuano midogo tofauti na ile waliyokuwa wanashiriki.

Lakini hapo hapo, kama Simba akienda na Yanga akaishia robo basi kwa mara nyingine watakuwa wamejitanabaisha kwamba kwamba wao wapo katika viwango totauti na Yanga na hawataki kukaa nao katika viwango sawa. Kwamba ‘ukinisogelea napanda ngazi zaidi.’

Kama wote wanataka kwenda nusu fainali basi waombee bahati ya kutopangwa na Mamelodi Sundowns ambao wameongoza katika kundi A. Kila mmoja anaweza kupewa Mamelodi. Yanga wana bahati kwamba wanaweza kupewa ASEC Mimosas. Lakini wanaweza kupewa Petro Atletico ya Angola.

Bahati nzuri kwao ni kwamba hawawezi kupewa Al Ahly ambao walikuwa nao kundi moja. Bahati mbaya kwa Simba ni kwamba anaweza kupewa Al Ahly au Mamelodi. Bahati nzuri kwao ni kama ikipewa Petro Atletico. Hawa kina Al Ahly na Mamelodi sio watu wazuri sana katika hatua za robo fainali. Kwao inakuwa kama vile michuano ndio imeanza.

Kwa Mnyama kama itatokea nafasi ya kupewa Al Ahly au Mamelodi basi ni bora wapewe Al Ahly. Hawaonekani kuwa sawa kama walivyokuwa katika miaka ya nyuma. Simba anaweza kupambana nao kama alivyofanya katika michuano ya Super League. Mamelodi ni ndoto ya kutisha. Sio Yanga wala Simba ambao wanaweza kupambana nao kwa sasa.

Petro hawana historia ya kutisha katika michuano hii na kwa upande wa ASEC itashangaza kama wanaweza kuwa timu ya kwanza ya Afrika Magharibi kufika nusu fainali tangu Enyimba walipofanya hivyo kwa mara ya mwisho mwaka 2003 ambapo walikwenda moja kwa moja kuchukua taji hilo na kuwa timu ya mwisho ya Afrika Magharibi kufanya hivyo.

Kazi nzuri imefanywa na kina Chama na Pacoume na wenzao. Na sasa tukutane pale Cairo katika kikao cha kupanga ratiba. Tunasubiri tu kuona nani atapangwa na nani lakini mwisho wa siku mwanaume ni yule ambaye ataifikisha Tanzania nusu fainali. Robo tumeiona.

SOMA NA HII  MASHABIKI WAYDAD WAFUATA NYAYO ZA SIMBA WAMEKIWASHA HUKO HATARI