Home kimataifa NI SUALA LA MUDA TU…CONTE, ZIDANE NA BRENDAN RODGERS KUCHUKUA NAFASI YA...

NI SUALA LA MUDA TU…CONTE, ZIDANE NA BRENDAN RODGERS KUCHUKUA NAFASI YA OLE MAN UNITED


NI suala la muda tu unaambiwa. Kila kitu kitaeleweka. Manchester United imeweka tayari orodha ya makocha wanne kwa ajili ya mmoja wao kumbadili Ole Gunnar Solskjaer huko Old Trafford, huku akiwamo kocha wa zamani wa Liverpool, Brendan Rodgers.

Zinedine Zidane na Antonio Conte wanaimbwa kama warithi wa kocha ambaye yupo kwenye presha kubwa sasa huko Man United juu ya usalama wa kibarua chake.

Wasiwasi wa mabosi wa Old Trafford ni kwamba wanataka kufahamu kama kocha wa zamani wa Real Madrid, Zidane na wa zamani Chelsea, Conte – wote kwa sasa hawana kazi na wanavutiwa na kibarua hicho. Kampuni moja ya uwakala imepewa kazi ya kuwasiliana na makocha wenye majina makubwa kwenye soka, ikiwamo wa Ajax, Erik Ten Hag na Leicester City, Brendan Rodgers – aliyewahi kuinoa Liverpool ambao ni mahasimu wakubwa wa Man United.

Wakati mabosi wa Man United wanavuta muda kumfuta kazi Solskjaer, lakini kwa sasa hawapuuzii tena kuporomoka kiwango kwa timu kunakoendana na matokeo ya mabovu.

Hali ilikuwa mbaya zaidi Jumapili iliyopita walipochapwa 5-0 na mahasimu wao wakubwa, Liverpool.

Kampuni hiyo ya uwakala imetakiwa kuwasiliana na kupata mipango ya kila kocha kwa kile anachopanga kwenda kufanya kwenye timu hiyo na mahitaji yao binafsi ya kimkataba.

Kocha Solskjaer ameshapoteza imani na mabosi wakubwa kwenye klabu hiyo baada baada ya udhalilishaji uliofanyika Jumapili Old Trafford.

Makamu mwenyekiti mtendaji mkuu, Ed Woodward amekuwa akimuunga mkono Solskjaer akiweka mipango ya muda mrefu kwenye kikosi hicho baada ya kupewa kazi aliporithi mikoba ya Jose Mourinho.

Timu hiyo baada ya kuwekeza kwa mastaa wa nguvu kama Cristiano Ronaldo, Jadon Sancho na Raphael Varane na kisha timu inashindwa kupata matokeo mazuri jambo hilo ndilo linalofanya kibarua cha kocha huyo raia wa Norway kuwa na mashaka makubwa.

Kikosi hicho kinashika nafasi ya saba kwenye msimamo Ligi Kuu England, pointi nane nyuma ya vinara Chelsea – baada ya Solskjaer kuisaidia Man United kupata pointi moja tu kati ya 12 ilizopaswa.

SOMA NA HII  KIPA WA LIVERPOOL AONGEZEA KASI VITA YA NNE BORA LIGI KUU ENGLAND

Kocha wa zamani wa Real Madrid, Zidane alikuwa wa kwanza kushinda mataji matatu mfululizo Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku la mwisho lilikuwa 2018 siku tano kabla ya kujiuzulu. Mfaransa huyo aliyebeba ubingwa wa Kombe la Dunia akiwa mchezaji alirudi Bernabeu kufanya kazi kwa awamu yake ya pili na kushinda taji la La Liga kabla ya kuachana na miamba hiyo mwishoni mwa msimu uliopita.

Aliwanoa Ronaldo na Varane huko Los Blancos na sasa anasubiriwa kwa hamu kwamba huenda akabamba uteuzi wa kutua Old Trafford.

Kocha wa zamani wa Juventus na Inter Milan, Conte aliongoza Chelsea kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 2016-17, alipoweka rekodi ya kushinda mechi 30 za ligi ndani ya msimu mmoja na kwenye msimu wake wa pili alishinda ubingwa wa Kombe la FA.