Home Makala EDO KUMWEMBE: KOCHA MPYA SIMBA ANAMITIHANI MINGI…ANAWEZA KUFUKUZWA…

EDO KUMWEMBE: KOCHA MPYA SIMBA ANAMITIHANI MINGI…ANAWEZA KUFUKUZWA…


PABLO Franco ndiye kocha mpya wa Simba. Kwanza inabidi uwasifu Simba kwa namna wanavyojua kuficha karata. Namna ambavyo ghafla wanaibuka na jina fulani la mchezaji au kocha bila ya mashabiki kutarajia. Bila ya vyombo vya habari kutarajia.

Jina limekuja la kocha kutoka Hispania. Pablo Franco. Anaingia Simba akiwa na mitihani mingi. Mtihani wa kwanza mkubwa unamhusu mwenyewe kabla ya mtu mwingine. Ataweza kumudu maisha ya Afrika? Hii ni kazi yake ya kwanza Bara la Afrika.

Amefanya kazi kwao katika wasifu mrefu. Ameshafanya kazi Asia. Na sasa ana mtihani wa kwanza barani Afrika. Anahitaji kuzoea haraka maisha ya Afrika ndani na nje ya uwanja. Bahati mbaya anakuwa kocha wa pili kutoka Hispania kufundisha nchini. Azam iliwahi kuleta benchi zima la ufundi kutoka Hispania lakini hata hivyo mambo hayakwenda poa.

Afrika na Tanzania imezoea makocha kutoka Ufaransa, Serbia, Brazil, Ujerumani na Ubelgiji. Haijazoea makocha kutoka Hispania. Pablo atajaribu kutuonyesha kile ambacho makocha wa Hispania wanacho. Anahitaji kuzoea kwa haraka. Hispania hapo mbali na Afrika lakini sio kwa ukanda huu. Ipo karibu na Morocco ambao nao ni kama wazungu tu. Pablo inabidi azoee kwa haraka mazingira ya Afrika. Hakuna siri tunaweza kumwambia kwamba ni mazingira magumu ndani na nje ya uwanja.

Kuna makocha wetu wazungu kina Micho, Kosta Papic, Henry Kasperczak ambao wameizoea Afrika na ndio maana wanazurura sana bara hili. Wamezoea matatizo yetu na wamegundua kwamba Afrika ina mpira wake ndani na nje ya uwanja. Pablo atakuwa na mtihani wa kwanza wa kupunguza uzungu ili aenda sambamba na wachezaji, viongozi na mashabiki wa Simba. Kila kitu hakitakwenda sawa kama anavyodhani. Awe tayari kumudu maisha yetu haraka ili kazi yake iende vyema.

Mtihani wa pili ambao inabidi aushinde ni matarajio makubwa ya aina mbili ya mashabiki. Tarajio la kwanza ni kwamba kocha anatoka Hispania kwa hiyo atakuwa ana uwezo mkubwa wa kufundisha soka kama lile la Pep Guardiola au Luis Enrique.

Hispania imejichongea katika miaka ya karibuni. Kuanzia kwa wachezaji hadi makocha. Popote walipo, wachezaji wa Hispania inabidi wacheze kama Xavi Hernandez. Na popote walipo makocha wa Hispania inabidi wafundishe mpira wa tiktak kama Pep Guardiola.

Wakati huu wapinzani wao Yanga wakiwa wanacheza soka safi la kitabuni, Pablo itabidi aifundishe timu yake kucheza zaidi ya vile ambacho kina Khalid Aucho wanacheza. Utaifa wake ni mtihani mkubwa. Mashabiki lazima wataweka matarajio makubwa kwake. Hapohapo kuna tarajio jingine kubwa. Wasifu wa Pablo unatisha. Amefundisha Getafe? Klabu ya Ligi Kuu ya Hispania. Nadhani hakujawahi kuwa na kocha mwenye wasifu mkubwa katika nchi yetu kama yeye. Amefundisha timu ya Ligi Kuu ya Hispania na sio jambo dogo. Labda kocha ambaye anaweza kufanana naye katika wasifu wa kufundisha timu ya ligi kubwa Ulaya ni wa zamani wa Yanga, Ernie Brandts. Aliwahi kufundisha Roda JC ya Ligi Kuu ya Uholanzi. Wasifu huu wa Pablo unamuweka katika nongwa nzito. Mashabiki watatarajia makubwa kutoka kwake na wala hawatampa muda mrefu wa kukisuka kikosi. Mashabiki wa pande zote mbili watakuwa wanampa presha. Wale watani watataka kumzomea na kuishawishi Simba kwamba ‘wamepigwa’. Wakati wale wa Simba watakuwa wanamtazama kwa jicho la kumtaka athibitishe ubora wake.

SOMA NA HII  SARE DHIDI YA KAGERA SUGAR YAMFANYA AHMED ALLY KUIBUKA NA HILI SIMBA...

Halafu tarajio jingine linakuja katika ubinadamu wa kawaida kwamba kocha yeyote ambaye angefuata, hata kama sio yeye alipaswa kuirudisha Simba katika lile soka la pira biriani. Mashabiki wa Simba wanachokiona sasa hawajakizoea kwa takribani mwaka wa nne. Walizoeshwa pasi nyingi na nafasi nyingi za kufunga. Mtihani mwingine ambao unamkabili rafiki yangu Pablo ni namna ya kuziba pengo la Clatious Chama na Jose Luis Miquissone. Hawajui na wala hajawahi kuwasikia lakini akifika tu katika uwanja wa mazoezi wa Simba kwa mara ya kwanza ataambiwa habari zao.

Akitazama mikanda ya zamani ya Simba ataona ubora wao. Najua kuna viongozi na mashabiki wengi ambao watamwambia timu haina ubora kwa sababu kuna wachezaji wawili muhimu wameondoka. Yeye hatajali sana hilo kwa sababu usajili wa wachezaji umeshafanyika na atalazimika kufanya kazi na wachezaji waliopo.

Kitu kibaya zaidi kwake ni kwamba halijui soka la Afrika na wala hafahamu wachezaji walio nje ya Simba ambao wanaweza kuimarisha kikosi chake katika dirisha dogo au mwishoni mwa msimu. Atalazimika tu kufanya kazi na wachezaji waliopo kina Jonas Mkude na mastaa wenzake.

Pablo atalazimishwa kuifikisha Simba katika ubora uleule wa kina Chama bila kujali sana wachezaji ambao anawatumia. Katika kundi hilo kuna wachezaji wapya walioingia ambao amepishana nao miezi miwili tu. Hawa ndio kina Peter Banda. Bado hawajaonyesha ubora wao mpaka sasa tofauti na mastaa wapya wa klabu nyingine.

Vyovyote ilivyo Pablo anaingia katika kikosi cha Simba akiwa na mitihani mingi. Macho na masikio pia yatakuwa kwake katika pambano la tatu la ligi dhidi ya watani wao Yanga. Nadhani ataambiwa umuhimu wa mechi hii. Mashabiki watataka abadilishe hali ya hewa kwa haraka zaidi ya kuwasili kwa mechi hiyo Desemba 11.

Mashabiki wengi wa Simba wanakubali nikisema timu yao inabidi ibadilike kwa haraka kabla ya mechi hiyo ngumu. Yanga wapo vizuri. Kabla hata hawajawa vizuri tayari walikuwa wanaisumbua Simba huku wakiwa na timu mbovu ya kina Yikpe.

Na sasa Yanga wana timu nzuri huku Simba wakionekana kusuasua kwa kiwango licha ya kuendelea kuwa na kundi kubwa la wachezaji kasoro mastaa wa zamani waliouzwa Morocco na Misri. Mashabiki watataka abadilishe upepo haraka kabla ya mechi hiyo. Wakati mwingine unaweza kudhani mzaha lakini kuna mambo mawili ambayo yanageuza akili za mashabiki na viongozi kwa haraka. Kwanza kuna mechi ya Simba na Yanga na pili kuna suala la ubingwa. Unaweza kuchukua ubingwa, lakini kama umenyanyaswa sana na mpinzani – basi unaweza kujikuta uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ukielekea nyumbani.

Credit: Edo Kumwembe/Mwanaspoti