Home news HITIMANA: KUNA MAKOSA TULIFANYA..KUONGOZA SIMBA SI KAZI RAHISI..NILISHINDWA KULALA WALA KULA..

HITIMANA: KUNA MAKOSA TULIFANYA..KUONGOZA SIMBA SI KAZI RAHISI..NILISHINDWA KULALA WALA KULA..


KWENYE mahojiano maalum na Kocha Msaidizi wa Simba, Thiey Hitimana alizungumzia mambo mengi ikiwemo lile la kuweka wazi kwamba ndiye aliyependekeza kwa uongozi walete Kocha mpya ambaye watasaidiana nae yeye na Seleman Matola. Lakini akaongeza pia kwamba ujio wake Simba ulitokana na uswahiba wake na Didier Gomes ambaye alikuwa anajua uwezo wake kiufundi.

 Hitimana anasema aliwahi kufanya kazi na Gomes nje ya Tanzania, hivyo alivyomtaka awe msaidizi wake hakuona shida ingawa kabla ya kupendekezwa na Gomes aliwahi kutuma maombi Simba lakini viongozi hawakuwa na uharaka wa kukamilisha dili lake. “Baada ya Simba kuona nimekuja Mtibwa Sugar, kufanya nao kazi, wakanitafuta na kilichofanya dili lao likamilike bila shida nilikuwa sijasaini mkabata, hivyo nikawalipa gharama zao zote za kunileta Tanzania,”anasema Hitimana na kuongeza;

“Basi maisha yangu na Simba yalianzia hapo katika nafasi ya usaidizi chini ya Gomes ambaye alikuwa ananihitaji na CV yangu iliwashinda makocha wengine waliomba nafasi hiyo kwa wakati huo,” anasema.

KOCHA MKUU

Anasema wakati anakuja Simba hakuwa anatarajia kama angekutana na mabadiliko ambayo yangembadili nafasi ya msaidizi hadi kocha mkuu, Ligi ya Mabingwa Afrika, ingawa kila kitu alifanya chini ya uangalizi wa Gomes.

“Kama tulishinda ugenini dhidi ya Jwaneng Galaxy, tulishinda pamoja na kama kutolewa tulitolewa pamoja, ingawa mechi ya pili ndio ilitibua mambo mengi sana, baada ya kufungwa nyumbani,”anasema na anaongeza kuwa;

“Kuna makosa tuliyafanya ambayo yalichangia kufungwa na kupoteza mechi hiyo, jambo ambalo hakuna aliyetegemea ila tumejifunza na kazi iliyobaki sasa ni kuandaa timu kwa ajili ya Kombe la Shirikisho Afrika.”

MECHI TATU ZA LIGI

Simba baada ya kuamua kuachana na Gomes, siku tatu mbele Hitimana alikiongoza kikosi hicho kama kaimu kocha mkuu na katika mechi tatu, alishinda mbili na alitoka sare moja.

Anakiri haikuwa kazi rahisi, kukaa benchi peke yake, wakati huo Matola alikuwa masomoni, lakini alikabiliana na ari na timu ikapata pointi saba.

“Kuongoza wachezaji 30 Simba si kazi rahisi, tena kipindi cha presha kubwa, sikuwa na wakushauriana naye kwenye benchi kwasababu Matola alikuwa kwenye kozi, ila nashukuru Mungu mambo yalienda.

“Nakumbuka presha ilikuwa tunatoka kupoteza mechi na Galaxy, tunakuja kucheza ligi na vinara wa wakati huo walikuwa Polisi Tanzania, mchezo huo ulikuwa ni lazima tushinde ili mashabiki waweze kutulia na wachezaji kurejea mchezoni,”

“Wakati huo huo ikumbukwe benchi la ufundi lililoondolewa lilikuwa na mafanikio makubwa, ilinilazimu kuwajenga wachezaji kiakili kwani walikuwa ni wale wale waliokuwa wanafanya kazi kubwa ndani ya misimu minne,”anasema.

MKUDE, KAGERE

Anasema hakutaka kubadili kikosi kwa haraka, kwani angeweza kuigawa timu zaidi, aliamua kukitumia kilekile kilichokuwa kinaanza chini ya Gomes.

“Ndio maana hata kina Ajibu, Mkude, Kagere kuanza kikosi cha kwanza, nilianza nao kwa utaratibu, baadae tukaanza kukaa sawa na sasa anakuja kocha mkuu atakayekuwa na mifumo yake,”anasema huku akisisitiza kwamba si rahisi kwa kipindi kifupi kujaribu mambo mengi kwa wakati mmoja ndio maana kwa sasa Kagere na mastaa wengine Wazawa wamekuwa wakifanya vizuri kwavile ameshawajulia na kila mmoja anajua wajibu wake mbele ya klabu na mashabiki lakini anasisitiza kwamba ujio wa Pablo jana utasaidiana kufanya mambo mengi yaende haraka

ALISHINDWA KULA, KULALA

Hitimana anasema wakati kikosi cha Simba kipo chini yake, alikuwa na presha kubwa ambayo ilimfanya ashindwe kula kwa raha na wakati mwingine kukosa kabisa usingizi.

SOMA NA HII  KWA YANGA NZIMA...HUYU HAPA NDIYE STAA ANAYEMTIA 'TUMBO JOTO' KOCHA WA EL MERREIKH...

Anasema kwake kilikuwa kipindi cha dimbwi la mawazo, akifikiria namna ya kutoka kwenye giza kinene na kuwafanya mashabiki wa Simba kuwa na kicheko.

“Niliwahi kukutana na presha kama hii nikiwa Rayon ya Rwanda na Namungo, ila hii ya Simba ni funga kazi ilikuwa kubwa katika maisha yangu ya soka, tangu nianze kucheza na kufundisha, nilikuwa nashindwa kulala, chakula kilikuwa hakina radha mdomoni,”anasema. 

Kocha huyo ameongeza kwamba Simba ina nafasi ya kufanya vizuri msimu huu licha ya kwamba mashabiki wanapata wasiwasi. Anasema kwamba kikosi hicho kina wachezaji wengi wazoefu wenye uwezo wa kuamua matokeo hivyo changamoto za hapa na pale za mwanzo wa msimu hazipaswi kuwakatisha tamaa mashabiki na kujiona kwamba timu yao ina tatizo kwani bado mechi nyingi na nafasi ya kujipanga ni kubwa. 

Hitimana anaona kwamba tena ni bora kuanzia chini ujue udhaifu wake na jinsi ya kujipanga kuliko uanze na papara na kumaliza vibaya.

Anaongeza kwamba misimu ya hivikaribuni Simba imekuwa ikianza na kasi ya kawaida kwani imekuwa bize na mambo ya kimataifa lakini jinsi msimu unavyochanganya na kufanya maajabu zaidi kuthibitisha umakini na ukongwe wao kwenye kuamua mechi za mashindano.

BIASHARA UNITED

Hitimana anasema alikuja Tanzania kwa mara ya kwanza wakati msimu unaanza kipindi Biashara United, lakini baada ya kudumu nao kwa miezi minne, huku akiwa halipwi mshahara yakamshinda akaamua kurejea kwao.

“Kabla ya kurejea nyumbani, nikatoka Musoma kwenda TFF kupeleka barua ya kudai mshahara wangu, nikakutana na mtu aliyenishauri niombe kazi Namungo FC, nikapewa namba ya viongozi, nikatuma CV yangu, ikakubalika nikapata kazi,”anasema Hitimana na kuongeza kuwa;.

“Nikaanza kazi, nikafanikiwa kuipandisha timu Ligi Kuu Bara, tulianza kwa kishindo kwa kutoa ushindani dhidi ya timu kongwe.

“Msimu uliopita kabla ya kuanza mwingine, niliwaandalia ripoti ikiwemo masuala la usajili na niliwaeleza ikiwezekana tushauriane masuala ya ufundi ila ya uongozi wafanye wenyewe.

“Nikashangaa wakati nipo nyumbani, wanasajili bila kuniambia, nikawa kama shabiki tu, yaani bora wangekuwa wanasajili ila wananiambia ningeona wanaona thamani yangu, ila hawakufanya hivyo, sikujisikia vyema, nikaona ni dalili ya mtu nisiyetakiwa,”anasema.

MTIBWA SUGAR

Hitimana anasema baada ya kumalizana na Namungo alirudi kwao Rwanda na hapo alipokea mawasiliano kutoka kwa viongozi wa Mtibwa Sugar ambao walifikia makubaliano ya kwenda kufanya nao kazi.

“Baada ya kuingia ndani ya timu nilikutana na mambo ya ajabu, ikiwemo kuingiliwa kazi zangu na msaidizi wangu ambaye alikuwa anapewa nguvu na baadhi ya viongozi, mimi nilikuwa kama vile msaidizi wake, alifanya vitu bila kunishirikisha,” anasema Hitimana na kuongeza;

“Binafsi niliona si mazingira sahihi ya kufanya kazi kwani hata msaidizi wangu nilikuwa nikimueleza ambalo anafanya si sawa, lakini hakutaka kubadilika basi nikaamua kuondoka na kurudi kwetu Rwanda, ili kulinda maslahi ya timu.

“Msimu huu ulipoanza viongozi wa Mtibwa Sugar, walinifuata tena na kuniambia wanataka kufanya kazi na mimi tena na watanitumia tiketi ya ndege, wakafanya hivyo na kabla ya kuja wakaniuliza kwa nini niliondoka, nikawaeleza baada ya kuchunguza wakajua ukweli wa jambo hilo, wakawawajibisha wahusika.”anasema. MWISHO.

Credit : Mwanaspoti