Home Makala OSCAR OSCAR: NINA IMANI NA MASHAKA JUU YA KOCHA MPYA SIMBA..UWEZO WAKE...

OSCAR OSCAR: NINA IMANI NA MASHAKA JUU YA KOCHA MPYA SIMBA..UWEZO WAKE UMEPOROMOKA…


NILIKUWA juu ya kitanda nikiperuzi mtandaoni kabla ya kukurupushwa na taarifa ya uteuzi wa kocha mpya wa Simba aitwaye Pablo Franco Martin.

Kati ya majina yote ambayo yangeweza kutangazwa na Simba sikutegemea kukutana na jina la Mhispaniola huyu aliyewahi kuwa mfanyakazi wa Fiorentino Perez pale Santiago Bernabeu katika klabu ya Real Madrid.

Unahitaji kusikia nini zaidi kuhusu Franco ili ukubali ukubwa wa wasifu (CV) wake? Kuanzia kuwa kocha mkuu Getafe kisha kocha msaidizi wa Julien Lopetegui pale Real Madrid, kucheza dhidi ya Barcelona iliyokwenda kutwaa klabu bingwa Ulaya ikiwa na utatu wa Messi, Neymar na Suarez, ‘kumshika koo’ Diego Simeone pale Wanda Metropolitano na mengineyo.

Pablo anaingia katika orodha ya makocha wenye CV kubwa kuwahi kuja nchini. Mbali na timu alizofundisha, Pablo ni msomi mzuri, anamiliki shahada ya sayansi ya michezo (bachelor degree of sports science).

Pia ana shahada ya uzamili (masters) katika uchambuzi wa mpira (football analysis).

Hata kama hukiri mdomoni, kimoyomoyo utakuwa unakubali kwamba Simba wamepata kocha mkubwa.

Lakini hapahapa kabla hatujafika mbali wakati tunajadili ukubwa linaibuka swali kwa kocha. Kocha aliyepata nafasi ya kufanya kazi katika ligi kubwa kama La Liga imekuwaje akaporomoka kiasi cha kuishia Tanzania?

Ninachofahamu kwa binadamu wote ni kwamba, kiu ya binadamu yeyote yule duniani ni kupiga hatua kwenda mbele. Hakuna binadamu anayetaka kurudi nyuma katika maisha. Kutoka kuifundisha klabu kubwa zaidi duniani hadi kudondokea katika mikono ya Simba ni kurudi nyuma. Imekuwaje?

Jibu hapa ni rahisi sana. Kuporomoka uwezo wa kufundisha. Wakati Pablo anapata kazi ya kuifundisha Getafe 2015, Thomas Tuchel alikuwa hana kazi. Unadhani kwanini sasa hivi Tuchel yupo Chelsea na Pablo yupo Simba?

Wakati Tuchel anazidi kupiga hatua kwenda mbele Pablo alikuwa anapiga hatua kurudi nyuma. Ushahidi zaidi unaweza kuupata kwa kutazama muda Pablo aliodumu ndani ya klabu moja. Klabu pekee aliyodumu kwa miaka miwili ni Qadsia ya Kuwait aliyofanya kazi kabla ya Simba. Hii inakuonyesha kwamba alifeli sehemu nyingi ndiyo maana hakuvumiliwa.

SOMA NA HII  ANAITWA KANTE, KIUNGO BORA DUNIANI

Lakini hilo halitoi sababu ya moja kwa moja kwamba atafeli ndani ya Simba. Wapo makocha waliowahi kufeli katika klabu moja lakini wakafanikiwa katika klabu nyingine.

Mfano mzuri ni huyu Tuchel tuliyemtumia kama mfano kabla. Tuchel aliwahi kufeli PSG kabla kuibuka shujaa Chelsea. Unai Emery alifanikiwa Sevilla kabla ya kwenda kufeli PSG na Arsenal, sasa ameibuka shujaa Villarreal na majuzi tu amewapa taji la Europa kwa kuwafunga Manchester United. Kwa hili la kufeli kabla katika klabu alizopita naweza kumtetea Pablo.

Ninachoshindwa kumtetea ni kuhusu suala la uzoefu na soka la Afrika. Ni kweli Pablo amezurura kwenye klabu nyingi barani Ulaya na Asia, lakini katika historia yake Simba inakuwa klabu yake ya kwanza ya Afrika kufanya nayo kazi.

Hapa atakutana na tamaduni mpya na mazingira mapya ya kufanya kazi. Je ataweza kukabiliana na changamoto mpya za soka la Afrika atakazokutana nazo? Ni suala la kusubiri na kuona. Hapa inabidi tuuachie muda ufanye kazi yake.

Nina uhakika katika maisha yake hajawahi kucheza uwanja unaofanana na Namfua (Liti) wa Singida au Kumbukumbu ya Karume (Musoma). Huu ni mfano wa changamoto inayomsubiri katika kibarua chake kipya.

Changamoto nyingine kubwa inayomsubiri ni kutimiza malengo waliyowekeana na Simba. Japo sijachungulia mkataba wa Pablo lakini najua lengo kuu la Simba ni kufika fainali ya Klabu Bingwa barani Afrika.

Hata kocha aliyepita Didier Gomes aliondolewa kwa sababu hiyo. Kiu ya Simba siyo kutwaa taji la Ligi Kuu Bara au Kkombe la Shirikisho la Azam (ASFC). Haya hata Selemani Matola angeweza kuwasaidia kuyapata. Hoja yao ni kutisha katika mashindano ya Bara. Ataweza? Siwezi kusema chochote lakini ninachofahamu kocha pekee hawezi kukusaidia kufanya vizuri katika mashindano makubwa kama ya Klabu Bingwa Afrika.

Unahitaji kocha bora na wachezaji bora. Sidhani kama Simba ina wachezaji hao kwa sasa. Tumsubiri Pablo na muda watatupa majibu.

CREDIT; MWANASPOTI/OSCAR OSCAR