Home Habari za michezo MASHINE MPYA YA SIMBA HII HAPA….JAMAA NI KIFAA NA NUSU….BENCHIKHA APITISHA TIKI...

MASHINE MPYA YA SIMBA HII HAPA….JAMAA NI KIFAA NA NUSU….BENCHIKHA APITISHA TIKI NYEKUNDU..

Tetesi za Usajili Simba

SIMBA imemaliza usajili wa ndani na sasa imehamia anga ya kimataifa baada ya usiku wa kuamkia jana kushusha mtu wa kwanza kiraka flani kimyakimya tayari kwa kuboresha kikosi hicho kilichopo kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa sasa visiwani Zanzibar.

Usiku huo mnene ambao waandishi wa gazeti la  Mwanaspoti walikuwepo Uwanja wa Ndege jijini Dar es Salaam ulikuwa unampokea kiraka Michael Charamba raia wa Zimbabwe, anayemudu nafasi tofauti kwa eneo la mbele ambaye inaelezwa ni pendekezo la Kocha Abdelhak Benchikha.

Huyo ni staa wa kwanza wa kigeni kwa Simba kwenye dirisha dogo kushushwa baada ya awali kutambulishwa Saleh Masoud Karabaka kutoka JKU, huku ikielezwa pia imemalizana na Ladeck Chasambi kutoka Mtibwa Sugar na Edwin Balua kutoka TZ Prisons ikiwa ni wachezaji wa ndani.

Charamba aliyeitumikia Chicken Inn ya Zimbabwe anasifika kama kiraka ambaye amekipa kikosi hicho ubora mkubwa kutokana na kumudu kucheza nafasi zaidi ya nne za ushambuliaji, kwani anamudu kucheza kama straika, kiungo mshambuliaji, mshambuliaji namba mbili na winga wa kulia.

Zaidi ya hayo jamaa anajua kufunga kwa mashuti ya mbali makali ambayo yalimpa ubora mkubwa kwenye Ligi Kuu ya Zimbabwe na sasa anahamishia makali hayo Msimbazi.

Jana mara alipotua nchini, Charamba alichukuliwa uwanjani hapo na watu wa Simba kwa ulinzi mkali huku wakizuia asipigwe picha yoyote kisha kuondoka naye haraka.

Inaelezwa leo Charamba aliyezaliwa Aprili 14, 1996 katika mji wa Kwekwek, Zimbabwe baada ya kumalizana na mabosi wa Simba anaweza kuvuka maji kuelekea kisiwani Zanzibar kuungana na kikosi cha timu hiyo tayari kwa kuanza kazi mara moja.

Kocha wa Big Bullets ya Malawi, Mzimbabwe Callisto Pasuwa amemzungumzia Charamba mwenye urefu wa M1.74 na kilo 68 akitumia zaidi mguu wa kulia, akisema Simba kama itamchukua kiraka huyo itakuwa imelamba dume kutokana na jinsi ambavyo anaweza kutumika kwa nafasi tofauti kisha akacheza kwa ubora mkubwa.

Pasuwa ambaye ni mmoja kati ya makocha wakubwa Zimbabwe alisema katika dirisha kubwa la usajili aliwahi kufikiria kumsajili mshambuliaji huyo Big Bullets, lakini alikwama kutokana na bajeti ya usajili.

“Namjua Charamba ni kijana wangu, ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa sana, kitu kinachompa thamani kubwa ni namna ambavyo anaweza kubadilika kwa matumizi tofauti halafu akayafanya kwa ufanisi,” alisema Pasuwa.

“Kama Simba wamempata kwa ajili ya kikosi chao nadhani watakuwa wamepata mchezaji mwenye kipaji kikubwa, hapa katikati niliwahi kumpendekeza wamlete hapa Malawi lakini naona uongozi ulikwama bajeti yake.”

Ujio wa Charamba huenda ukaenda kung’oa baadhi ya mastaa waliopo Simba ambao wamekuwa kwenye rada ya kupigwa panga kwa sababu mbalimbali, akiwamo kiungo mshambuliaji, Clatous Chama aliyesimamishwa kwa utovu wa nidhamu na Moses Phiri aliyedaiwa ameomba kuondoka.

Credit- Mwanaspoti.

SOMA NA HII  CHAMA 'AKOPOLEWA MAWE' NA SHABIKI WA SIMBA...ISHU NZIMA IKO HIVI...