Home news KWA HUYU KOCHA MPYA..KILA ‘FAULO’ YA SIMBA NI GOLI…SOKA LAKE NI ‘SUKARI’...

KWA HUYU KOCHA MPYA..KILA ‘FAULO’ YA SIMBA NI GOLI…SOKA LAKE NI ‘SUKARI’ TUPU…


WAKATI mashabiki wa Simba wakihesabu saa kabla ya kushuhudia kocha mkuu mpya wa kikosi chao akitua Msimbazi, mabosi wa klabu hiyo wamekuja na sapraizi ya aina yake ya kuwaletea kocha kutoka Hispania ambaye anasifika kwa soka la kampa kampa tena!

Awali ilielezwa Simba ilikuwa ikiwapigia hesabu makocha kutoka Afrika akiwamo Rolani Mokwane wa Afrika Kusini, lakini dau lake likawafanya wachomoea mapema licha ya kushawishiwa na Kocha wa Al Ahly, Pitso Mosimane, kisha kuhamia kwa Lamine N’Diaye kutoka Senegal.

Jina jingine la tatu lililokuwa likipigiwa hesabu ni Muargentina Miguel Angel aliyeinoa Wydad Casablanca na ilionekana ndiye alikuwa akikaribia kutua Msimbazi, kabla ya mabosi hao kubadili gia angani kutokana na kuvutiwa na maufundi ya Mhispania, Pablo Franco aliyekuwa katika Tatu Bora.

Taarifa zikufikie rasmi kuwa huyu ndiye kocha anayekuja kuinoa Simba kuchukua nafasi ya Didier Gomes aliyeachana nayo saa chache baada ya kung’olewa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa bao la ugenini na Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Pablo aliyekuwa akiinoa klabu ya Ligi Kuu ya Kuwait ya Al-Qadsia anakuja nchini akiwavutia mabosi wa Msimbazi kwa sifa zake zinazolingana kwa kiasi kikubwa na alizokuwa nazo kocha wao wa zamani, Sven Vandenbroeck aliyewafikisha makundi ya CAF msimu uliopita kisha kutimkia FAR Rabat ya Morocco.

Unaambiwa muda wowote kuanzia sasa kocha huyo ambaye majina yake kamili ni Pablo Franco Martín akiwa na umri wa miaka 41 tu atatua nchini kabla Ligi Kuu haijarejea tena baada ya mapumziko ya wiki mbili.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Simba ni kwamba kati ya jana na leo Jumanne, Pablo atatambulishwa na mabingwa hao wa Bara ambao pia ni wawakilishi pekee wa nchi katika michuano ya kimataifa, ikiwa inashiriki mchujo ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba katika kuhakikisha wanakuwa na benchi imara la ufundi, Pablo hatakuja peke yake, ila atakuwa na msaidizi mmoja – mtaalamu wa viungo kuchukua nafasi ya Adel Zrane aliyetemwa sambamba na Gomes na kocha wa makipa, Milton Nienov kutoka Brazili.

“Kila kitu ni kama kimekamilika baada ya Franco (Pablo) kutuma maombi aliingia kwenye makocha watatu bora akiwa na Miguel Angel na Lamine N’Diaye, ila wasifu na gharama zake zilimpa nafasi ya kuwapiku wenzake na sasa anakuja kuinoa Simba,” alisema kiongozi mmoja wa juu.

“Franco (Pablo) alifanya vizuri hata mahojiano na jopo la kutafuta kocha mpya na kila ambacho alitakiwa kukijibu alitoa majibu sahihi. Ndio maana tulimpitisha na sasa tupo katika hatua za mwisho kukamilisha aje nchini na huyo msaidizi wake – kocha wa viungo.”

FUNDI WA PASI NYINGI

Pablo Franco Martin aliyezaliwa Juni 11, 1980 katika mji wa Madrid, Hispania alianza kucheza soka kabla ya kujitosa kwenye ukocha akifundisha timu mbalimbali Hispania kupitia klabu za Real Madrid akiwa msaidizi wa Zinedine Zidane ‘Zizzou’, Getafe katika La Liga, huku akiwa ni mzoefu kwenye soka barani Ulaya, Asia na Mashariki ya Mbali.

SOMA NA HII  FEI TOTO:HAIKUWA KAZI RAHISI, MAPAMBANO YANAENDELEA

Kocha huyo mwenye wasifu wa maana anajipambanua kupenda soka la kuvutia lenye udambwidambwi mwingi wa pasi nyingi za kwenda mbele na umiliki wa mpira ambao kwa msimu huu Simba umekuwa ukikosekana na kuwatia hasira mashabiki wakiona watani wao Yanga wakiupiga mpira wa aina hiyo katika mechi tano za Ligi Kuu Bara.

Mbali na soka la pasi nyingi, lakini pia ni mtaalamu wa mipira iliyokufa ambapo kwa mashabiki wa Simba wamekosa kuona kwa miaka mingi tangu alipoondoka Dragan Popadic kutoka Yugoslavia (Serbia ya sasa) ambaye aliwafanya wapinzani wa timu yake kuogopa kufanya madhambi au kutoa kona.

KLABU ALIZOPITA

Kama kocha, Pablo alianza kuifanya kazi hiyo 2008 akiinoa Coria kama kocha msaidizi hadi 2009 alipohamia Fuenlabrada akiwa pia ni msaidizi na 2010-2012 alikuwa kocha mkuu wa Santa Eugenia zote za Hispania, kisha 2013-14 alijiunga na Puertoliano na baada ya hapo alienda Getafe B, 2014-15 kabla ya kuwa kocha mkuu katika klabu hiyo 2015 katika La Liga.

Alienda Georgia 2016 kuinoa timu ya Saburtalo Tbilisi kwa mwaka mmoja kabla ya kutimkia China 2017-18 kuifundisha Beijing Sport University akiwa kocha msaidizi.

Msimu wa 2018-2019 alikuwa msaidizi wa Zizzou ndani ya Real Madrid katika La Liga iliyokuwa na mastaa kama Gareth Bale, Karim Benzema, Sergio Ramos, Toni Kroos na wengineo na 2019-2021 alikuwa Kuwait kuinoa Al Qadsia katika Ligi Kuu ya nchi hiyo.

Kati ya 2000 hadi 2005 alifanya kazi kwenye soka la vijana katika klabu za Real Madrid, Rayop Vallecano na Real Valladolid CF zilizowahi kutamba La Liga.

Mbali na kufundisha soka akiwa na Uefa Pro Licence, lakini jamaa pia ni mtalaamu wa kuchambua mchezo kwa kuuangalia (football analysis) akiwa na shahada ya uzamili, pia ni skauti mzuri wa kunasaka vipaji akiwa na taaluma ya utawala, kitu kilichowakuna mabosi wa Msimbazi kumbeba.

Hata hivyo, hana rekodi nzuri ya mataji kama ilivyokuwa kwa Sven, lakini uwezo wake wa kufundisha na hasa soka lililozoeleka Msimbazi imefanya Pablo awe chaguo la kwanza kwa mabosi wa Simba wakiamini kiu yake ya kusaka mafanikio na hasa kufundisha Afrika kutambeba kuisaidia timu yao.

Aliwahi kutwaa ubingwa na timu ya CD Puertoliano katika Ligi Daraja la Nne Hispania (Tercera División). Mwaka 2016 aliifikisha Saburtalo Tbilisi fainali ya play-off kuwania medali ya shaba na kupoteza mbele ya Dinamo Tbilisi baada ya awali timu hizo kumaliza nafasi ya pili na tatu katika Ligi Kuu ya Georgia.

Mwaka juzi akiwa na Qadsia aliiongoza kubeba ubingwa wa Kuwait Super Cup kwa kuinyoa Al Kuwait kwa bao 1-o, likiwa ndilo taji lake kubwa la karibuni.