Kiungo Mshambuliaji, Salum Abubakar Salum ‘Sure Boy’ tayari ametambulishwa kuwa mchezaji wa Yanga baada ya hivi karibuni kuomba kuvunja mkataba ndani ya Azam FC.
Sure Boy aliyedumu Azam FC kuanzia 2007 hadi 2021, amejiunga na Yanga kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo akisaini mkataba wa miaka miwili.
Baada ya kutua Yanga, Sure Boy ambaye kwa muda mrefu amekuwa akitumia jezi namba nane katika timu anazocheza, Azam na Taifa Stars, ndani ya Yanga amekabidhiwa jezi namba 18.
Jezi hiyo katika kikosi cha Yanga inatajwa kuwa si yenye bahati sana kutokana na wachezaji wengi walioivaa kwa miaka ya karibuni kutokuwa na mwendelezo mzuri wa kiwango.
Akizungumzia ujio wa Sure Boy, Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli, alisema: “Sure Boy amepewa jezi namba 18, na taratibu ndogo zimebaki kukamilisha mambo mengine madogo madogo kwa ajili ya kukamilisha usajili wake.”
Jezi hiyo tangu iachwe na kiungo Frank Domayo aliyeichezea Yanga kuanzia 2012 hadi 2014 ambapo alitimkia Azam FC alipo sasa, waliofuatia wamekuwa hawadumu sana licha ya kutua na makali.
Desemba 2016, Emmanuel Martin baada ya kutua Yanga akitokea JKU ya Zanzibar,alikabidhiwa jezi hiyo, lakini kiwango alichotua nacho, hakikuwa na mwendelezo zaidi ya kushuka hadi anaondoka.
Baadaye jezi hiyo ikakabidhiwa kwa straika Mganda, Juma Balinya aliyecheza kwa takribani miezi sita, kuanzia Julai 1, 2019 hadi Desemba 12, 2019, akafunga bao moja tu ligi kuu, akaondoka.
Haruna Niyonzima wakati anarudi tena Yanga Desemba 2019, alikabidhiwa jezi namba 18, baadaye akabadilishiwa na kupewa namba 8 ambayo sasa imetua kwa Sure Boy baada ya kukuta namba 8 inavaliwa na Khalid Aucho. Pia kuna wakati kiungo Said Juma Makapu aliivaa, lakini baadaye akabadilishiwa na kupewa 22.