Home news PAMOJA NA TIMU KUYUMBA UWANJANI…MANULA, ONYANGO KUIKAMUA SIMBA MAMILIONI..BARBARA ATULIZA HALI..

PAMOJA NA TIMU KUYUMBA UWANJANI…MANULA, ONYANGO KUIKAMUA SIMBA MAMILIONI..BARBARA ATULIZA HALI..


ACHANA na mzigo mzito walionao kwenye Ligi Kuu Bara kwa sasa, mastaa wa Simba, Aishi Manula na Joash Onyango misimamo yao ya kimasilahi huenda ikawatoa jasho vigogo wa Msimbazi siku chache zijazo.

Mastaa hao na wengine wanane, mikataba yao inaelekea ukingoni lakini uongozi wa Simba umesisitiza kwamba mkwanja upo na yeyote ambaye wanamhitaji wa kikosi cha kwanza watapambana naye abaki wakiwemo Aishi na Onyango.

Simba ambayo imepoteza mechi mbili na sare mbili ugenini kwenye ligi, wachezaji wake ambao mikataba imebakia miezi sita wapo kipa, Manula, Hassan Dilunga, Onyango na Rally Bwalya.

Wengine ni kinara wa mabao msimu huu kwenye kikosi cha Simba, Meddie Kagere, Chriss Mugalu, Bernard Morrison, Mzamiru Yassin, Jonas Mkude na Pascal Wawa.

Inafahamika kwamba Simba tayari kuna wachezaji wameanza mazungumzo nao wale wanaomaliza mikataba ukiondoa Morrison na Wawa.

Kipa tegemeo, Manula inaelezwa kwamba ametaka Sh100 milioni kama aliyochukua hapo awali aliposaini mkataba wa miaka mitatu na imekuwa hivyo kutokana na ubora alionao sasa pamoja uwepo wa ofa nyingi mezani kwake kutoka timu mbalimbali kubwa Afrika.

Dilunga wamekubaliana na uongozi anachosubiri ni kusaini mkataba mpya wakati Onyango mwenye bao moja mchakato wake bado umekuwa na mvutano kutokana na kutaka sasa aongezewe mshahara kutoka Sh6 milioni kufika Sh11.5 milioni kwa mwezi.

Onyango amewaeleza Simba katika mkataba mpya atakuwa tayari kumwaga wino kwa dau la kusainia la Sh60 milioni kama thamani ya usajili wake kwa miaka miwili pamoja na kutaka mshahara usiopungua Dola 5,000 zaidi ya Sh10 milioni kwa pesa ya Kibongo.

Uongozi unaendelea kupambana Bwalya, Mugalu, Mkude na wengineo kuona namna gani wanakubaliana kandarasi mpya na kabla ya zile za sasa kufikia ukingoni watakuwa wamemalizana nao.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alisema uongozi una mipango mikubwa juu ya mikataba hiyo na wanalifanya kwa kushirikiana na kocha, Pablo Franco ambaye mashabiki wamekuwa wakimsema vibaya mitandaoni kutokana na kiwango cha timu.

SOMA NA HII  FT: AZAM FC 1-1 SIMBA SC....BOCCO KAWAOKOA TENA..MATUMAINI YA SIMBA YAZIDI KUYEYUKA...YANGA WANATAKA TISA TU...

“Niwahakikishie wapenzi wa Simba wote watulie wasiwe na wasiwasi juu ya uongozi tumejipanga vizuri na bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuwapa mikataba mipya wachezaji wetu muhimu,” alisema Barbara na kuongeza;

“Kikosi chetu kina wachezaji wengi wazuri tena kwa ajili ya malengo ya muda mrefu sidhani kama tunaweza kuwaacha kiurahisi na kabla ya msimu kuisha litakuwa limeenda vizuri hili,” aliongeza Barbara.