KOCHA Mkuu wa Mbeya City, Mathias Lule, ameitahadharisha Yanga, kuwa isitarajie kupata mteremko katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, watakapokutana Februari 5 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Mbeya City, wapo nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 22 kibindoni huku wakiwa wameshuka uwanjani mara 13 wakiwa juu ya Azam FC kwa pointi moja malengo yao mwakani ni kushiriki michuano ya Shirikisho barani Afrika.
Lule amesema kuwa malengo yao ni kucheza michuano ya Shirikisho mwakani ili kuwapa uzoefu wa michuano ya kimataifa wachezaji wake kama ilivyokuwa kwa Namungo na Biashara ambazo kwa misimu ya karibuni zimeiwakilisha nchi pamoja na Simba.
“Tunapaswa kuwa na muendelezo mzuri katika michezo minne ijayo ili kujiwekea katika mazingira mazuri yakutimiza malengo yetu ambayo yatatimia kama tutapata ushindi kwenye michezo yetu,” alisema Lule.
Mbeya City watakuwa kibaruani Februari 5, kuwakabili vinara Yanga, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, katika muendelezo wa kuzisaka alama tatu ambazo zitawasaidia kusogea juu katika msimamo wa Ligi kuu Tanzania Bara.