WAKATI Simba SC ikiambulia pointi moja mbele ya US Gendarmerie juzi Jumapili, ilifanya umafia kwa kuzungumza na wakala wa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Victorien Adebayor ili kumsajili.
Adebayor ni kati ya wachezaji tegemeo katika kikosi cha Gendarmarie ambaye katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane msimu huu alifunga mabao mawili.
Katika mchezo huo wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika uliomalizika kwa sare ya 1-1, Adebayor aliwasumbua sana walinzi wa Simba akitumia vizuri mguu wake wa kushoto.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema: “Tayari tumeanza kufanya mazungumzo na wakala wa mshambuliaji Adebayor.
“Tumesikia anacheza hapa kwa mkopo, huyu ni mchezaji wa kucheza timu kubwa kama Simba na siyo kwenda Ulaya.
“Nitajitahidi kumshauri Rais wa Heshima wa Klabu (Mohammed Dewji) avunje benki ili tuipate saini yake.”
Kwa upande wa Adebayor mwenyewe akizungumza juu ya uwezekano wa kutua Simba, alisema: “Hakuna ambaye anaweza kukataa kucheza kwenye klabu kubwa kama Simba.
“Nipo tayari na kama bahati kwangu, kwa sababu Simba ni moja kati ya klabu kubwa Afrika, ni heshima na bahatikwangu kutakiwa na klabu hiyo.”
Adebayor ambaye ni raia wa Nigeria, anacheza US Gendarmarie kwa mkopo akitokea HB Koge ya Denmark. Aliwahi pia kucheza ENPPI ya Misri.
Nyota huyo kwa sasa thamani yake imepanda hadi kufikia dola za marekani 200,000 ambazo ni zaidi ya milioni 468 za Kitanzania.