Home news EDO KUMBWEMBE:..MASTAA SIMBA WANAWEZA KUMFUKUZISHA KAZI PABLO…AGUSI JINSI SVEN ALIVYOSEPA…

EDO KUMBWEMBE:..MASTAA SIMBA WANAWEZA KUMFUKUZISHA KAZI PABLO…AGUSI JINSI SVEN ALIVYOSEPA…


MAISHA huwa yanakwenda kasi. Sven Vandenbroeck amechaguliwa kuwa kocha bora wa Ligi Kuu ya Morocco msimu huu. Inashangaza kidogo. Alipoondoka wengi waliridhia. Bahati nzuri kwake ni kwamba pande zote zilikutana katikati.

Kuna ambao hawakuridhishwa na uwezo wa Sven katika njia za kushangaza kidogo. Walikuwa wanadai kwamba kocha ni mbishi. Wapo waliokuwa wanamshutumu kwa kutotumia washambuliaji wawili eneo la mbele. Lakini wapo pia waliokuwa wanamshutumu kwa tabia mbalimbali za nje ya uwanja. Kwamba ni mwanadamu mbishi. Ilipokuja ofa kutoka klabu ya Rabat FS ikaonekana kama vile ilikuwa fursa nzuri kwa kila mtu kwenda upande wake.

Hata hivyo hii ya kutochezesha washambuliaji wawili kuna wakati ilikuwa hoja maarufu miongoni mwa Wanasimba. Ulikuwa ni wakati wa maringo hasa kwa sababu kila mshambuliaji wa Simba alikuwa fiti. Meddie Kagere alikuwa fomu, John Bocco alikuwa fomu na Chris Mugalu alikuwa fomu.

Nyakati zimekwenda na sasa Simba wana kocha mwingine, Pablo Franco Martin. Amekumbana na tatizo la washambuliaji ambalo linaweza kumfukuzisha kazi pia. Wakati washambuliaji hawa hawa wa Simba walikuwa wanataka kumfukuzisha kazi Sven kutokana na ubora wao, washambuliaji hawa hawa wanataka kumfukuzisha kazi Pablo kwa sababu nyingine.

Kwanza kabisa tofauti na nyakati zile, wote hawa kwa sasa hawapo katika fomu. Labda tunaweza kumzungumzia Kagere mwenye mabao matano. Kwa kiwango chake mwenyewe Kagere haya ni mabao machache. Tushamzoea kuona sasa hivi akiburuza washambuliaji wengine wa ndani na nje ya nchi.

Leo Kagere anaburuzwa na Relient Lusajo pamoja na Fiston Mayele. Sio kawaida yake ingawa mambo yanaweza kubadilika. John Bocco yupo katika fomu mbaya na hamsaidii kocha wake. Chris Mugalu alikuwa majeruhi wa muda mrefu lakini hata baada ya kurudi hajaonyesha makali yake.

Majuzi hapa mlinzi wa Mtibwa Sugara, Abdi Banda ingawa alitumia kauli isiyo nzuri lakini alielezea matatizo ya washambuliaji wa Simba. kilichoshangaza ni kwamba siku chache baadaye Pablo aliamua kutoanza na mshambuliaji pale Kagera. Simba walipoteza.

Kwanini Pablo alianza bila ya mshambuliaji? Wapo watu waliompinga lakini wapo watu waliomuunga mkono. Kwanza kabisa Pablo ni kocha wa Kihispaniola. Kina Pep Guardiola huwa wana tabia hizi kwa kile kinachoelezwa ni mbinu zao uwanjani.

Lakini hapo hapo wapo waliomuunga mkono Pablo wakiamini kwamba washambuliaji wenyewe walikuwa wamepoteza makali. Hata hivyo Simba walipoteza pambano hilo kiasi kwamba ikazua mjadala kwa Kamari ya Pablo ambayo haikulipa.

Juzi Simba walikuwa tena uwanjani kucheza na timu kibonde ya Dar City na kulikuwa na nafasi nyingi kwa washambuliaji wa Simba kumuonyesha Pablo kwamba alikosea kutoanza na mshambuliaji kule kanda ya Ziwa. 

Kagere alijitahidi kumuonyesha Pablo ingawa ilikuwa mechi nyepesi zaidi. hata hivyo Bocco na Mugalu walishindwa kumuonyesha Pablo kwamba alifanya makosa kuwaacha nje kule Kagere. Walikosa mabao ya wazi. Hata kama baadaye Mugalu alifunga lakini mashabiki waliondoka uwanjani wakiwa wanasononeka kwa kile ambacho Bocco na Mugalu walionyesha.

SOMA NA HII  MMEKWISHAA...CHAMA KATUA...SIMBA YAMSAINISHA MIWILI FASTA...BARBARA ASIMAMIA SHOO NZIMA..

Na sasa Pablo amekalia kuti kavu. Nazifahamu vema hivi timu. Simba kupoteza mechi mbili kati ya tatu za mwisho za Ligi ni lazima kocha akalie kuti kavu. Haijalishi kama tatizo ni la kocha au sio lakini lazima akalie kuti kavu.

Simba pia wametoka sare nne katika Ligi. Ni sare ambao zimeambatana na washambuliaji wake kupoteza nafasi nzuri za kufunga lakini pia wamekosa penalti. Matatizo yote haya yana-kwenda kumuangukia Pablo.

Ingawa joto la kufukuzwa kwa Pablo halipo juu lakini ukweli ni kwamba endapo Simba watakosa taji lolote msimu huu na kisha kushindwa kwenda mbali katika michuano ya Shirikisho huenda Pablo atajikuta pabaya. Swali litakuja katika uhalali wa kufukuzwa kwake kama akifukuzwa. Je Simba haitengenezi nafasi? Hapana. Inatengeneza nafasi nyingi tu lakini washambuliaji wake hawazitumii ipasavyo. Yote haya hayataaangaliwa vema klabuni na mwisho wa siku hukumu inaweza kumuangukia Pablo.

Haya yanatokea wakati watani wao wakiwa vizuri. Wana mshambuliaji nambari moja, Fiston Mayele ambaye amekuwa akifunga na kushangilia kwa nyodo. Hata hivyo Mayele anabakia kuwa kama alama tu ya ufungaji lakini kuna watu wengine wanamsaidia kazi na ndio siri ya mafanikio ya Yanga msimu huu.

Fey Toto anafunga, Khalid Aucho anafunga, Jesus Moloko anafunga. Herietier Makambo anafunga japo hajafunga katika Ligi. Simba ina tatizo la washambuliaji wake kutotumia nafasi lakini pia msimu uliopita na mingine michache iliyopita wachezaji wake waligawanya mabao.

Achilia mbali Kagere, Bocco na Mugalu lakini pia Clatous Chama na Luis Miquissone walifunga mabao ya kutosha kutoka katika maeneo mengine. Msimu huu washambuliaji hawafungi na wachezaji wa maeneo mengine hawafungi.

Pambano dhidi ya Kagera, Mzamiru Yassin alikosa bao la wazi. Shomari Kapombe alikosa bao la wazi. Mohammed Hussein Tshabalala naye alikosa bao la wazi. Hapa ndipo unapoona ugumu wa kazi ya Pablo. Wachezaji wanaweza kumfukuzisha kazi. Kwa jinsi ambavyo maisha yanakwenda kasi Msimbazi, Sven alikuwa anataka kufukuzwa kazi kutokana na ubora wa mastaa, lakini ghafla Pablo anataka kufukuzishwa kazi na ubovu wa mastaa wale wale. Ni suala la wao tu kutumia nafasi.

Katika mechi zote ambao Simba imepoteza pointi, achilia mbali ya Yanga, Simba walikuwa wanatawala mpira kwa kiasi kikubwa. Katika mechi zote hizi waliondoka uwanjani na utawala wa mechi kwa asilimia 70 au zaidi. Hata hivyo leo tunazungumzia hatihati ya Pablo kufukuzwa kwa sababu tu wachezaji wake hawatumii nafasi.

Waulize wachambuzi pamoja na watu wa ndani wa Simba ni mbinu zipi ambazo Pablo anafeli nadhani hawawezi kukwambia. Watakachokwambia ni uzingatie matokeo tu bila ya viwango. Hapa ndipo linapokuja suala la ugumu wa kazi ya ukocha.

Makala haya yaliandikwa na Edo Kumwembe na kuchapishwa kwanza kwenye wavuti la Mwanaspoti.