Home Habari za michezo RAGE : YANGA WAKO VIZURI …..WANASHINDA KWA AJILI YANGU…HAKUNA KAMA MAYELE…

RAGE : YANGA WAKO VIZURI …..WANASHINDA KWA AJILI YANGU…HAKUNA KAMA MAYELE…


Licha ya Yanga kumtibulia kwenye utabiri wake kwamba timu hiyo ingepasuka mbele ya KMC na Azam, Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage amesisitiza kwamba; “Nitafutwe baada ya Aprili 30, sioni kama Mnyama atamuacha.”

Rage alikaririwa na gazeti la Mwanaspoti kuwa, Yanga isingetoboa kwenye mechi nne zilizokuwa mbele yao, zikiwamo za Simba na Mbeya City na kuitibulia kwenye mbio zao za ubingwa, lakini Yanga imezichapa KMC na Azam na sasa inajiandaa kuivaa Simba.

Rage alipotafutwa jana alisema; “Ni kweli nilisema Yanga isingetoboa, lakini naona kauli yangu imewachochea kupambana kama ilivyofanya juzi kwa Azam, ila siamini kama itabeba ubingwa kwa vile bado ina mechi ngumu mbele yao ikiwamo dhidi ya mnyama.”

“Kama Mtanzania lazima nikiri kwa sasa Yanga ipo vizuri kuliko misimu minne iliyopita na kila mtu anajua hakuna straika mkali kwa sasa kama Fiston Mayele, lakini nitafutwe baada ya Aprili 30, kwani sioni kama Mnyama atamuacha,” alitamba kiongozi huyo wa zamani wa TFF.

Rage aliongeza, kuna watu wanamchukulia sivyo, ila ukweli ni kwamba Yanga na Simba sio maadui bali watani wa jadi na kauli zake huwa ni za kuchombeza utani huo tofauti na wanavyochukulia wengine.

“Yanga wenyewe wananijua ninavyowatia tumbo joto, hata kushinda dhidi ya KMC na Azam imetokana na kutaka kufuta kauli yangu, ila niwaambie wasijiamini sana.”

Yanga ilizitungua KMC na Azam mtawalia kwa mabao 2-0 na Aprili 30 itavaana na Simba katika mechi ya 108 ya Kariakoo Derby kabla ya kucheza na Ruvu Shooting kisha Namungo mechi zitakazochezwa kati ya Mei 4 na 8.

Matokeo ya juzi usiku dhidi ya Azam imeifanya Yanga kujikita kileleni na pointi 51 baada ya mechi 19, ikifunga mabao 33 na kufungwa matano, ikiiacha Simba ikiwa nyuma yao kwa tofauti ya pointi 11 baada ya kushinda ugenini dhidi ya Coastal Union, jijini Tanga.

SOMA NA HII  ACHANA NA ISHU YA BONGO UNAAMBIWA SIMBA IMEFUNIKA AFRIKA NZIMA YAWEKA REKODI HII