Home news WAKATI MAYELE AKIZIDI KUTAKATA YANGA…YACOUBA AMTAZAMA WEEE…KISHA AFUNGUKA HAYA…

WAKATI MAYELE AKIZIDI KUTAKATA YANGA…YACOUBA AMTAZAMA WEEE…KISHA AFUNGUKA HAYA…


HABARI ya mjini sasa kwa upande wa soka ni straika wa Yanga, Fiston Mayele ambaye amekuwa mwiba kwa mabeki na makipa wa timu pinzani, kumbe moto huo umemshtua hadi Yacouba Songne ambaye ameukubali mziki huo, ila amepiga mkwara.

Mayele ameibuka shujaa juzi baada ya kuifungia Yanga bao pekee dhidi ya Mbao na kuivusha timu hadi 16 Bora ya michuano ya Shirikisho (ASFC) katika mechi kali iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM KIrumba, jijini Mwanza.

Kumbe Yacouba amekuwa akimfuatilia mwenzake mwenye mabao sita katika Ligi Kuu Bara akishika nafasi ya pili nyuma ya Reliants Lusajo wa Namungo na kusema anafurahishwa na juhudi za Mayele na kukiri hofu aliyonayo kwa namba yake.

Yacouba yupo nje ya uwanja kwa muda kutokana kusumbuliwa na jeraha la goti amefunguka, kwa sasa anaendelea vizuri na ameanza mazoezi ya nguvu, akiweka wazi kuwa muda wowote anaweza kurudi uwanjani kuipigania namba yake.

“Tumesajiliwa Yanga kujenga nyumba moja mazuri yanayofanywa na Mayele ni ya wanayanga wote, nafurahia juhudi zake na nakiri kuwa ni mchezaji bora kwa sasa pamoja na mastaa wengine wanaocheza nao kikosini, kwani peke yake hawezi,” alisema Yacouba na kuongeza;

“Nimemisi vingi tangu niwe nje ya uwanja, hakuna pengo linaloonekana baada ya kukosekana kwangu, kwani timu inafanya vizuri inapata matokeo kwa hakika nina kazi kubwa kuhakikisha narudi kikosini kwani kwa sasa kila mmoja ni bora.”

Akiizungumzia Yanga kwa ujumla, mshambuliaji huyo aliyekuwa kinara wa mabao wa timu hiyo kwa msimu uliopita akifunga nane, alisema anaiona ikiwa na mafanikio makubwa zaidi msimu huu tofauti na misimu minne nyuma waliyokosa mataji.

“Kwa sasa kila mchezaji ana uchu na kiu ya mafanikio kwa timu ndio maana imekuwa ikifanya vizuri, nami kwa vile nimeanza kujifua naamini nitarudi kuongeza nguvu.”

SOMA NA HII  KAMA ULIDHANI KMC IMEANZA KUKATA PUMZI....ILA SAHAU...WAZIPIGIA HONI POINT 6 ZA KANDA YA ZIWA...