KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ameonyesha kuwa hataki kufanya mchezo katika suala la kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, hii ni baada ya kuwaambia mastaa wake kuhakikisha wanakuwa na mawazo ya pointi tatu tu, katika mchezo wao ujao dhidi ya KMC.
Kuelekea mchezo huo dhidi ya KMC utakaochezwa Jumamosi ijayo, kikosi cha Yanga juzi Jumatano kilirejea kambini kwa ajili ya kuanza maandalizi, huku sehemu kubwa ya wachezaji waliokuwa majeruhi nao wakiwa wameanza rasmi programu za pamoja na wenzao.
Yanga ambao mpaka sasa ndiyo vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi zao 45 walizokusanya katika michezo 17, wanatarajia kuvaana na KMC Machi 19 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, huku wakiwa na kumbukumbu ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Oktoba 19, mwaka jana.
Kocha Nabi alisema: “Kila mtu anajua uwezo wa KMC, hii ni miongoni mwa timu bora kwenye ligi kuu na ni wazi tunatarajia mchezo mgumu dhidi yao, hasa kutokana na ukweli kuwa sehemu kubwa ya kikosi chao kina wachezaji wazoefu.
“Lakini licha ya ushindani tunaotarajia kukumbana nao ni lazima tuhakikishe tunashinda mchezo huu, ni lazima mawazo yetu yawe juu ya pointi tatu na si matokeo ya aina nyingine na wachezaji wangu wanajua hilo.”