Home Habar za Usajili Simba EDO KUMWEMBE : MORRISON ANAWADANGANYA WATANZANIA…KUCHEZA SIMBA HAKUTOSHI…

EDO KUMWEMBE : MORRISON ANAWADANGANYA WATANZANIA…KUCHEZA SIMBA HAKUTOSHI…


Neymar alishakuwa tajiri kabla hajaenda Ulaya. Mwaka 2012 wakati akicheza klabu ya Santos alishanunua boti ya kifahari (yatch) yenye thamani ya dola 10 milioni. Ni pesa nyingi. Ina maana tayari alishakuwa tajiri kwa kucheza Ligi Kuu ya Brazil.

Hata hivyo, inasemekana mambo mawili yalisababisha aende Ulaya mwaka 2013 huku akisaini klabu ya Barcelona katika uhamisho ambao lilikuwa suala la muda tu kwa sababu lazima Neymar ilikuwa aende kucheza Ulaya.

Kulikuwa na sababu mbili. Wabrazil walimlazimisha akacheze Ulaya. Sababu ya kwanza ni kwamba haijalishi angeonyesha kipaji cha namna gani akiwa Brazil lakini kamwe asingefikiriwa kuwa Mwanasoka Bora wa Dunia kama angeendelea kucheza kwao.

Haijalishi kama angetwaa ubingwa wa Amerika Kusini (Copa Amerika), haijalishi kama angechukua ubingwa wa klabu bingwa kwa mataifa ya Amerika Kusini (Copa Libertadores), haijalishi kama angechukua Kombe la Dunia akiwa na Brazil. Kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia inabidi ucheze Ulaya.

Ni ngumu kutwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia kama hauchezi katika ligi kubwa Ulaya. Ni ngumu pia ukiwa unacheza Amerika Kusini, Afrika, Asia wala kule juu Australia. Inabidi ukaonyeshe kipaji chako Ulaya katika ligi ngumu dhidi ya timu imara.

Sababu nyingine iliyowasukuma Wabrazil wamwambie Neymar akacheze Ulaya ni ukweli kwamba walitaka akomae katika soka la Ulaya kabla ya kuiwakilisha Brazil katika michuano ya Fainali za Kombe la Dunia nchini humo mwaka 2014.

Ndio maana Neymar aliondoka mwaka mmoja kabla ya Kombe la Dunia. Walitaka akatoe ushamba Ulaya na acheze mara kwa mara kabla ya kuwa mchezaji wao muhimu zaidi katika michuano hiyo ambayo ingefanyika nchini kwao.

Nimekumbuka kuhusu Neymar baada ya majuzi kuendelea kumsoma Bernard Morrison ambaye amekuwa akililia kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Ghana wakati huu akicheza soka Afrika Mashariki. Nimecheka kidogo.

Kuna mwandishi mmoja kutoka Ghana huwa anakuja Tanzania kutazama baadhi ya mechi za Simba. Inaonekana kama vile ana kampeni maalumu na rafiki yake Morrison kuhusu staa huyu kuitwa timu ya taifa ya Ghana.

Kuna ukweli mwingi ambao Morrison anausahau. Amekuwa akiwaponda kina Andre Ayew na mdogo wake Jordan Ayew kama vile wapo nyuma yake kisoka naye kupitia hizi mechi dhidi ya Coastal Union anaona kama anastahili.

Mpira una viwango vyake. Kuna Waghana zaidi ya 100 ambao inawezekana kiasili hawafikii kipaji cha Morrison, lakini wanacheza soka katika nchi ambazo ligi zao ni bora kuliko Tanzania. Ghana wanakuchaguaje wakati unacheza Tanzania?

Inaweza kuwa ngekewa kama unacheza nafasi fulani ambayo wana matatizo nayo lakini sio nafasi ya Morrison. Kule Afrika Magharibi makipa wengi wanaocheza ndani ya Afrika au ndani ya nchi zao huwa wanapata bahati ya kuitwa katika vikosi vyao. Kuna makipa wachache wa Afrika wanaotamba nje ya nchi zao au nje ya bara la Afrika.

SOMA NA HII  KUHUSU ISHU YA KUUNGANA NA GSM YANGA....MANJI KAVUNJA UKIMYA...JIBU LAKE HILI HAPA...

Rafiki yangu Morrison ananichekesha. Nimepitia orodha ya Waghana wanaocheza timu ya taifa nje ya watoto wa Abeid Pele nimekutana na watu wanaocheza Ligi Kuu za Ujerumani, Ubelgiji, Ufaransa, England na kwingineko. Alitaka aitwe kwa sababu gani? Ulazima huo unatoka wapi?

Mchezaji anaweza kuwa na kipaji cha kawaida, lakini kama anacheza katika ligi kubwa basi anastahili kupata nafasi. Anacheza katika ushindani mwingi kila wikiendi. Huo ndio ukweli wa kawaida kwa makocha wanaofundisha timu za taifa.

Rafiki yangu Morrison alie kwa kujilaumu mwenyewe tu. Kipaji chake kipo wazi na wala hakustahili kuwa hapa. Kwa namna alivyo au anavyocheza alistahili kuwa huko Ulaya miaka mingi iliyopita, lakini ameendekeza kuwa mchekeshaji zaidi ya kuwa mwanasoka.

Sio kwa bahati mbaya kwamba yuko hapa. Sio yeye tu. Kuna wanasoka wengi maridhawa wa kigeni katika ligi yetu ambao sio kwa bahati mbaya wapo hapa. Kuna ambao wapo hapa kwa sababu umri umewapita isipokuwa wanamudu tu kucheza hapa, kuna ambao ni walevi tunawajua hawawezi kucheza ligi ‘serious’ zenye ushindani.

Kuna wale wenye utovu wa nidhamu akiwepo yeye mwenyewe. Sio kwa bahati mbaya kwamba tunao wanasoka wengi wa kigeni mahiri na wanamudu kucheza Tanzania kwa sababu ya mfumo wa soka letu. Wasingeweza kucheza nje na kutamba.

Morrison anafahamu fika kitu gani cha kufanya ili aweze kuitwa timu ya taifa ya Ghana. Anajua kwamba anawadanganya Watanzania kwamba anaonewa lakini ukweli anaujua moyoni. Kucheza Simba au Yanga katika mechi za CAF hakutoshi kukufanya uitwe timu za taifa za Ghana, Cameroon, Ivory Coast, Mali au Senegal. Ndio maana miaka nenda rudi tupo na Serge Wawa Pascal na wala halalamiki.

Kuna mahala ambapo alipaswa kujipima kweli kweli kiasi cha kuhalalisha kuitwa timu ya taifa ya Ghana. Ikumbukwe kuwa hata Simba yenyewe hajaikamata vya kutosha kuweza kuhalalisha kuitwa katika timu ya taifa ya Ghana.

Ukiwataja wachezaji watatu muhimu kwa Simba kwa sasa yeye hayupo. Inakuwaje analilia kuichezea Ghana? Analeta udanganyifu kwa sababu anajua kwamba mashabiki wetu huwa wanapenda kuambiwa vitu wanavyotaka kusikia.

Hata hawa rafiki zetu Zambia kuna nyakati ambazo mchezaji wao alikuwa akija Tanzania kuwa wanagoma kukuita katika timu ya taifa. Davis Mwape alipokuja Yanga wakaacha kumuita timu ya taifa. Sielewi kwanini wamebadili msimamo wao kwa Clatous Chama na Rally Bwalya. Labda kwa sababu Simba inafika mbali katika michuano ya kimataifa.

Makala haya yaliandikwa na Edo Kumwembe na kuchapishwa kwanza kwenye wavuti la Mwanaspoti