Home KMC FC HITIMANA – YANGA WAKITAKA WATACHUKUA UBINGWA KWA NJIA ZOTE…SENZO ATIA ‘UZITO’ MABADILIKO…

HITIMANA – YANGA WAKITAKA WATACHUKUA UBINGWA KWA NJIA ZOTE…SENZO ATIA ‘UZITO’ MABADILIKO…


FISTON Mayele anatisha nyie acheni tu. Karibu kila timu aliyokutana nayo ameitungua na alianza na Simba kwenye Ngao ya Jamii, akawapiga Azam, Mtibwa, Coastal na nyingine na nyingine. Na usishangae kuona KMC ambao ndio kituo kinachofuata cha Yanga wakisuka mkakati maalum wa kumdhibiti mwamba huyo.

Kocha mkuu wa KMC, Thiery Hitimana amesema anatambua ugumu wa mchezo wao ujao dhidi ya Yanga lakini wanajiandaa vizuri kuhakikisha hawapotezi katika mechi hiyo.

Yanga na KMC zitakutana Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa saa 1:00 usiku.

Hitimana alisema anajua hawako vizuri kwenye safu ya ulinzi lakini ameandaa plani ya kulidhibiti jeshi la Wananchi linaloongozwa na straika wao kinara wa mabao, Mayele.

“Tutacheza kwa tahadhari kubwa sana kwa kujua kama hatuko vizuri kwenye safu ya ulinzi lakini tutapambana, mechi itakuwa ngumu sana kwetu kwa sababu tunacheza na kinara wa Ligi ambaye ana nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa akiutaka kwa njia zote,” alisema Hitimana.

Kwenye mzunguko wa kwanza KMC walifungwa 2-0 na Yanga huku Mayele akitupia moja ya mabao hayo, la pili likifungwa na Feisal Salum.

KMC kwenye mechi yao iliyopita dhidi ya Coastal Union ilifungwa 3-2 kwenye Uwanja wa Azam Complex, wakati Yanga katika mechi iliyyopita ilishinda 1-0 ugenini dhidi ya Geita Gold, shukrani kwa bao la Mayele, ambaye analingana mabao 10 na Reliants Lusajo wa Namungo kileleni mwa chati ya wafungaji wanaoongoza kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu.

KMC inashika nafasi ya tatu katika orodha ya timu zinazofunga mabao mengi ikiwa na mabao 20, nyuma ya vinara Yanga (mabao 29) na Simba na Namungo (mabao 21 kila moja), lakini tatizo kikosi hicho cha Hitimana kinaruhusu mabao mengi (19) yakitofautiana na waliyofunga kwa bao moja tu, jambo linalozidi presha kwao.

TIZI KALI

Baada ya kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya taifa ya Somalia, kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi amewapa wachezaji wake mazoezi makali ya fiziki na mbinu za kutosha kwa ajili ya mechi yao dhidi ya KMC.

SOMA NA HII  KUHUSU BALEKE KUBAKI TZ...TP MAZEMBE WAZIDI KUIKALIA KOONI SIMBA...TIMU ZA ULAYA ZAWEKA OFA...

Nabi amesema walianzia kwenye mazoezi ya nguvu (Gym). “Baada ya mechi wachezaji walikuwa na mapumziko ya siku moja kisha leo (jana), tutaanza kufanya mazoezi mengi ya mbinu zaidi kulingana na mahitaji ya mechi inayofuata,” alisema Nabi na kuongeza;

“Ukiangalia mechi ya KMC ni ngumu kutokana na ubora wa wachezaji, benchi la ufundi kwahiyo tutafanya maandalizi mengi ya mbinu kulingana na wapinzani wetu walivyo.”

MABADILIKO YANGA

Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingisa amesema kuwa mchakato wa mabadiliko unaendelea vizuri na sasa wapo kwenye hatua za mwisho na kufika mwishoni mwa mwezi wa Juni kila kitu kitakuwa tayari.