Home Habari za michezo HIVI NDIVYO JINSI PAPARA ILIVYOIGHARIMU SIMBA JUZI…WALICHEZA KIMAZOEA…USGN ANAWEZA KUSHANGAZA DAR..

HIVI NDIVYO JINSI PAPARA ILIVYOIGHARIMU SIMBA JUZI…WALICHEZA KIMAZOEA…USGN ANAWEZA KUSHANGAZA DAR..


Kama ungekuwa unaangalia mechi ya juzi kwa kuvutiwa na kupeleka mipira mbele, ungeweza kusema Simba ilicheza kwa kiwango cha juu dhidi ya wenyeji Asec Mimosas katika mechi ya mzunguko wa pili iliyofanyika Coutonou, Benin.

Na hata takwimu, kwa kiasi fulani zilithibitisha hilo; Simba ilimiliki mpira kwa asilimia 56 dhidi ya 44 za wenyeji, ilipiga pasi 524 dhidi ya 425 za Asec, ilipiga kona nane dhidi ya nne na ilikuwa na pasi za uhakika kwa asilimia 85 dhidi ya asilimia 83, angalau kwa uchache.

Lakini takwimu hizo hazionyeshi uhalisia wa mchezo huo wa mwisho kasoro mmoja wa Kundi B ulioisha kwa wenyeji kushinda kwa mabao 3-0 na hivyo kujiweka kileleni kwa kufikisha pointi tisa, huku Simba na RS Berkane zikifuata kwa pointi saba na USGN ikiburuza mkia kwa kuwa na pointi tano.

Lakini USGN inaweza kusonga mbele kama timu nyingine tatu za kundi hilo iwapo kutakuwa na maajabu katika mechi za mwisho zitakazofanyika Aprili 4.

Kama ilivyocheza katika mechi nyingine za kundi hilo, Simba ilielekeza silaha zake zote mbele, ikicheza kwa jitihada bila ya unadhifu.

Ilianza na Sakho, Meddie Kagere na Lary Bwalya katika safu ya ushambuliaji, kitu kilichoonyesha kuwa kocha Pablo alitaka timu ishambulie zaidi licha ya kwanza ilikuwa ugenini ambako pointi moja ingeisaidia kujiweka vizuri kwa mechi ya mwisho.

Nyuma yao walikuwepo Kibu Dennis, Jonas Mkude, Mzamiru na Mohamed Hussein kusaidia kumiliki mpira wakati timu ikishambulia.

Na kweli, Simba ilianza kwa nguvu na ikaonekana muda mwingi ikijaribu kupitishia mashambulizi upande wa kulia, ambako mbali na Bwalya kutokea upande huo, bado nyuma yake alikuwepo Kibu huku Kapombe akifanya kazi yake ya kusogea mbele kusaidia mashambulizi.

Sehemu ya kiungo haikuonekana kutumia muda wake kusoma hali ya mchezo na kubadili mbinu au sehemu ya kupitishia mpira, bali kuendelea kusukuma mbele mashambulizi kupitia upande wa kulia na mara chache sana kumtafuta Sakho, tena kwa mipira mirefu iliyomkuta akiwa amejitenga na wenzake na hivyo kuwapa Asec mwanya wa kumzunguka na kumzuia asie nde mbele au kumpokonya mipira kirahisi.

Kagere alibakia na kazi ya kujaribu kuwabana mabeki wa Asec ili wapoteze mipira, lakini akawa akiwekwa mtu kati hadi anapoamua kuacha na kuwaruhusu waondoke golini.

Mkude, Mzamiru na Bwalya walijitahidi kutawala kiungo, lakini uwezo wa kuusoma mchezo na kubadili maarifa ulionekana kuwa mdogo na hivyo mipira yao kutokuwa na ufanisi mwishoni.

Matokeo yake, kila waliposhindwa kutekeleza mkakati wao, Asec walirudi kwa nguvu na kasi na kulifikia lango la Simba mapema na wakati mwingine mipira mirefu ilionekana kuwasumbua mabeki wa Simba, Verane akilazimika kwenda chini kunasa mipira.

SOMA NA HII  KILICHOMWONDOA BOCCO SIMBA HIKI HAPA

Kati ya hiyo, mipira miwili mirefu ilisababisha ngome ya Wekundu wa Msimbazi kuwazawadia wenyeji penati mbili, ambazo zingeweza kusababisha kipigo cha jana kuwa kibaya zaidi kama si umahiri wa Aishi Manula kupangua penati mbili.

Zote mbili zilitokana na Simba kuangalia upande mmoja zaidi na mipira mirefu ilipotumwa kutoka sehemu ya kiungo ya Asec kwenye kwa Karim Konate, Stephanie Aziz Ki au Kramo Kouame, ilionekana hakukuwa na njia nyingine zaidi ya kucheza professional foul; kwanza kwa kipa Manula na pili kwa beki Joash Onyango.

Mara nyingi, Asec walionekana kupasiana sana nyuma lakini wakiangalia kwa makini sehemu ambayo wangeweza kupitisha mipira.

Mabao yote mawili yalianzia katikati. Kwanza Toseta Singone aliona uwazi mbele yake na akautumia kwa kuingia na mpira. Baadaye akaupeleka kulia kwa Anicet Ouara aliyemtoka kirahisi Tshabalala na kupiga krosi ya chini kwa mfungaji Kramo Kouame.

Tshabalala hakuwa amesimama kimshazali wakati Ouara akitafakari jinsi ya kumpita, hali ambayo humpa winga urahisi wa kupitishia mpira sehemu ambayo beki hataweza kugeuka kwa haraka. Mkude ndiye aliyeonekana kuwa angeweza kufuta kosa hilo, lakini akabakia kumtazama Ouara hadi alipopiga krosi hiyo ya chini.

Na bao la pili, Toseta Singone alipokea mpira uliobutuliwa na Onyango na badala ya kuupeleka pembeni, safari hii aliupeleka mbele ya eneo la penati kwa Aziz Ki, ambaye aligeuka kwa haraka na kuachia kiki ya mguu wa kushoto iliyomuacha Manula akichupa kiushahidi.

Bao la tatu pia lilitokaa na mabeki kusahau upande wa kulia ambako pasi ndefu ilitumwa, lakini krosi ikaokolewa kabla ya krosi nyingine iliyounganishwa wavuni kwa kichwa na Konate.

Kwa ujumla, umiliki wa mpira si silaha pekee ya kuizidi timu pinzani, bali unadhifu wa matumizi yake. Mipira michache ambayo Asec waliipeleka golini kwa Simba ingeweza kuzaa mabao matano, lakini mipira mingine ambayo Simba waliipeleka langoni kwa Asec haikuwa na tija, labda kiki moja ya Kagere iliyonyakwa na kipa.

Aina ya uchezaji huu wa Simba bila ya kubadili mkakati ni mwendelezo wa mechi ambazo zimekuwa zikiwagharimu mabingwa hao wa soka nchini. Ilicheza hivyo katika mechi zote mbili dhidi ya Kaizer Chiefs na baadaye Galaxy na matokeo yake ikawa ni kuruhusu zaidi ya mabao mawili.

Simba haihitaji papara kwenda mbele, bali kushambulia kwa unadhifu, maarifa na kubadili njia za kupitishia mipira kila inapoonekana kuwa hali ni ngumu.