Home Habar za Usajili Simba PAMOJA NA KUSABABISHA PENATI KWENYE MECHI ILIYOPOTA…ONYANGO ATULIZA ‘PRESHA’ SIMBA…

PAMOJA NA KUSABABISHA PENATI KWENYE MECHI ILIYOPOTA…ONYANGO ATULIZA ‘PRESHA’ SIMBA…


Beki Joash Onyango ni kama ameshusha presha kwa kocha Pablo Franco ambaye alikuwa na wasiwasi wa kumtumia kwenye mchezo wa Jumapili.

Simba itakuwa mwenyeji wa Union Sportive de la Gendarmerie Nationale kwenye Uwanja wa Mkapa Dar es Salaam katika mchezo wake wa mwisho wa makundi wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Kama itashinda Jumapili, Simba itatinga robo fainali sanjari na mshindi wa mechi ya ASEC Mimosas au Berkane ambazo ziko nafasi ya kwanza na ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo.

Wasiwasi wa kocha Pablo ilikuwa ni kukosekana kwa beki wake raia wa Kenya, Joash Onyango katika mchezo huo muhimu kwa Simba ambayo itakuwa nyumbani.

“Tulifikiri ana kadi tatu za njano, kwamba hataweza kucheza Jumapili,” alisema meneja wa timu hiyo, Patrick Rweyemamu jana akizungumzia kuwepo kwa Oyango kwenye mchezo huo.

Mechi yetu ya mwisho, Onyango alicheza faulo iliyosababisha penalti ambayo kipa Aishi Manula aliicheza ingawa Simba ilifungwa mabao 3-0.

“Kwenye mechi ile tulijua amepewa kadi nyingine ya njano, lakini haikuwa hivyo, refarii alitoa penalti lakini hakumpa Onyango kadi hivyo amesalia na kadi zake mbili za awali, hivyo Jumapili itakuwa ni matakwa ya kocha tu kumtumia,” alisema.

Alisema katika mchezo huo, Simba itamkosa Hassan Dilunga pekee ambaye ni majeruhi, na wachezaji wengine wote watakuwepo kikosini.

Simba itaikabiri Gendarmerie ikiwa na kumbukumbu ya kuvuna pointi moja ilipocheza nayo kwao na kutoka sare ya bao 1-1, matokeo ambayo mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa klabu hiyo, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema yamekuwa na faida kwao.

“Tunaamini nyumbani tutashinda, kila mwana Simba anahitaji ushindi tu Jumapili na si vinginevyo, timu ina ari na hamasa ya kushinda mechi hiyo na kufuzu kucheza robo fainali,” alisema.

Juzi wachezaji na benchi la ufundi la Simba chini ya kocha, Pablo Franco walifanya kikao kizito baada ya wachezaji kuwasili kambini kwao mchana kabla ya kupata chakula cha mchana.

Pablo ndiye aliyeendesha kikao hicho ambapo aliwaeleza nyota wake kwamba katika siku tano za maandalizi ya kuelekea mchezo dhidi ya USGN wanatakiwa kuongeza umakini ili kupata matokeo mazuri.

SOMA NA HII  SIMBA HAKUNA KUPOA KUSEPA LEO JIONI KUWAFUATA AL AHLY

Baada ya hapo wachezaji walieleza wanatakiwa kuichukulia kwa umakini mkubwa mechi hiyo ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na kila mchezaji kupambana vya kutosha kwa nafasi yake kuhakikisha wanashinda na kwenda robo fainali.

Mshambuliaji wa Simba, Benard Morrison baada ya kuwasili kambini alisema; “Jamani tumerudi, tuna kazi kubwa Jumapili lakini ni rahisi kwa kuwa tunaenda kupambana zaidi kuhakikisha tunaingia robo fainali.”

Nyota wa Simba waliokuwa kwenye kikosi cha Stars waliombewa ruhusa ili kujiunga na wenzao katika maandalizi hayo ambao ni Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Mzamiru Yassin, Kibu Denis, Israel Patrick na Jonas Mkude. Pablo aliomba mastaa wake wasiwe kwenye mpango wa Stars chini ya kocha Kim Poulsen kutokana na kuwa na mchezo mgumu mbele yao na kuwa na uchovu kutokana na kutoka safari sambamba na kucheza mechi mfululizo.

Kim alisema kuwa; “Nimewaruhusu jana (juzi) kujiunga na wenzao tayari kwaajili ya mchezo wao na USGN, nawatakia kila la kheri na tunategemea matokeo mazuri kutoka kwao kwasababu ndio wawakilishi pekee kwenye michuano ya kimataifa,” alisema na kuongeza;

“Nilikuwa natambua umuhimu wao kikosini hasa kwenye mechi hii ya mwisho tunayotarajia kucheza kesho (leo) dhidi ya Sudan lakini hakuna njia nyingine, tuna kikosi kipana ambacho naamini kitamalizia pale kilipoishia.”

Naye Mkuu wa Idara ya Habari ya Simba, Ahmed Ally alithibitisha kuwa; “Baada ya kupewa ruhusa wachezaji walijiunga na wenzao kambini na jioni walifanya mazoezi ya pamoja na wenzao chini ya kocha Pablo.”

Katika mechi hiyo, Simba imeruhusiwa na CAF kuingiza mashabiki 35,000 huku viongozi wakisisitiza mashabiki kutumia vyema nafasi hizo kuisapoti timu yao na kutaja viingilio kuwa ni Sh 30,000 VIP A, VIP B ni 20,000, C ni 10,000 na mzunguko ni Sh 3,000.

Katika kundi D ASEC Mimosas inaongoza kwa pointi tisa, huku Simba na RS Berkane zikilingana pointi saba na US ikiwa na pointi tano.