KUNA vita kubwa ya ubingwa msimu huu, Yanga ikiwa imepania kuzima ufalme wa Simba na katika kuhakikisha kila kitu kinakaa sawa na morali ya mastaa wao inaendelea kuwa juu, mabosi wameamua kugawa mamilioni ya fedha.
Yanga iliyokuwa uwanjani juzi usiku kucheza mechi ya kirafiki na Mafunzo kwenye Uwanja wa Azam Complex, kupitia matajiri wao GSM wameipiga bao Simba kwa kutumia fedha ndefu katika kutoa posho kwa wachezaji wao kupitia mechi zao.
Katika mechi 18 ilizocheza Yanga hadi sasa, mastaa wa timu hiyo wamevuta mzigo wa maana, kwa mgao uliogusa duru la kwanza iliyojumuisha mechi 12 ilizoshinda na nyingine tatu za duru la pili.
Mechi tatu tu ambazo mastaa hao wa Jangwani hawakuvuna fedha baada ya kulazimishwa sare na Simba, Namungo na Mbeya City,
Habari za ndani kutoka Yanga ni kwamba kila mechi moja mabosi wa Yanga huwapa wachezaji Sh 15milioni na kwa mechi hizo 12 za duru la kwanza walikomba jumla ya Sh 180milioni, japo mechi za kimkakati dhidi ya Azam, Coastal Union, KMC na Mtibwa Sugar, wachezaji walipewa Sh 30milioni kwa kila mchezo.
Katika duru la pili ambalo Yanga imecheza mechi tatu dhidi ya Kagera Sugar, Geita Gold na KMC ambapo mzigo uliongezwa kutoka Sh 15milioni na kuwa Sh 20 milioni, huku ule wa KMC ukipanda hadi Sh 30 Milioni.
Jumla ya fedha zote ukizichanganya hesabu katika mechi 15 ilizoshinda Yanga kati ya 18 ilizocheza hadi sasa zinaonyesha kuwa mastaa wa Yanga wamelamba zaidi ya Sh300 milioni.
Yanga ikiwa hivyo, watetezi wa ligi hiyo, Simba yenyewe nao imekuwa na utamaduni wa kugawa mkwanja kwa mastaa wao kila mechi moja wanayoshinda, ambao ni Sh 20Milioni na katika duru la kwanza ilicheza mechi 15 na kushinda tisa ikiwa na maana wachezaji walivuta Sh 180Milioni.
Katika duru la pili Simba imecheza mechi mbili tu dhidi ya Biashara United na Dodoma Jiji na mastaa wake kuvuna Sh 40Milioni ambazo zikijumlishwa na zile za duru la kwanza maana yake wamekomba Sh 220 milioni hadi sasa.
Huku ikiwa na kiporo kimoja na Polisi Tanzania ambapo kama itashinda itawafanya mifuko yao itune na kufikia Sh 240 Milioni wakiifukuzia Yanga kwa mbali.
Imekuwa ni desturi katika mechi ya Kariakoo Derby, kiwango cha bonasi na posho kuwa juu kulinganisha na mechi nyingine, hivyo kama kina Fiston Mayele na wenzake watafanya kweli kama ilivyokuwa kwenye mechi ya Ngao ya Jamii, basi huenda wakabeba mzigo wa maana.
Katika mechi hiyo ya Ngao, mastaa wa Yanga walipewa zaidi ya Sh 300 milioni, kitu ambacho kwenye pambano lao lijalo la Aprili 30, mambo yanaweza kuongezeka, kwani ndio mechi inayoshikilia hatma ya ubingwa kwa timu hiyo msimu huu.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mazingisa aliwahi kukaririwa akisema; “Siwezi kusema ni kiasi gani, lakini wachezaji huwa wanapata bonasi kwenye kila mchezo ambao wanashinda, kuwapa morali.”