Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI YA PILI SAUZI…DYLAN KERR AIPA SIMBA MBINU ZA KUIMALIZA ORLANDO...

KUELEKEA MECHI YA PILI SAUZI…DYLAN KERR AIPA SIMBA MBINU ZA KUIMALIZA ORLANDO MAPEMA…


Aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Dylan Kerr amefunguka kuhusu mchezo wa Mkondo wa Pili Hatua ya Robo Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika kati ya klabu hiyo ya Dar es salaam dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Simba SC itacheza ugenini Uwanja wa Orlando Jumapili (April 24), baada ya kuanzia nyumbani jijini Dar es salaam Uwanja wa Benjamin Mkapa na kupata ushindi wa bao 1-0 Jumapili (April 17).

Kocha huyo ambaye kwa sasa anakinoa kikosi cha Moroka Swallows, amesema Simba SC inaweza kuifunga Orlando nyumbani kwao, endapo watakua na umakini na kutumia mbinu mbadala, tofauti na walizotumia Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili iliyopita.

Amesema tangu alipoanza kazi Swallows amebahatika kukutana na Orlando katika michezo mitano ya Ligi Kuu ya Afrika Kusini ‘PSL’, akishinda mmoja, akitoka sare mara tatu na kupoteza mchezo mmoja.

“Nakumbuka mara mwisho kucheza dhidi ya Orlando nilitumia mfumo wa 4-3-3, tulitengeneza vizuizi vitatu kila pembe, haikuwa rahisi kufika eneo letu, tulifunga njia, kila mpira ambao tulikuwa tukiupata tulihakikisha unakuwa na madhara kwao,” amesema Kocha huyo mzaliwa wa visiwa vya Malta ambaye alipata wasaa wa kucheza soka katika Ligi ya England na kuongeza.

“Haikuwa rahisi kupata alama dhidi yao lakini kasi ilitubeba. Mkishambulia kwa kasi Orlando wanawavurugikiwa,” amesema

Katika mchezo wa Jumapili (April 24), Simba SC italazimika kulinda ushindi wake wa bao 1-0 walioupata Dar es salaam, ama kusaka ushindi zaidi ili kujihakikishia nafasi ya kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Orlando Pirates watalazimika kusaka ushindi wa mabao mawili kwa sifuri ama zaidi, ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo msimu huu 2021/22.

Dylan Kerr alikinoa kikosi cha Simba SC msimu wa 2015-16, kabla ya kutimkia nchini Kenya kujiunga na Gor Mahia ambapo alifanya kazi kwa msimu mmoja wa 2017/18,

Msimu wa 2018-19 alianza kazi Afrika kusini akiwa klabu ya Black Leopards, mwaka 2020 aliajiriwa na Baroka FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini ‘PSL’, kabla ya kurudi tena Black Leopards msimu wa 2020/21.

SOMA NA HII  WAKATI BARBARA AKISEMA HAWATAKI MAKOSA TENA....SIMBA WAMSHUSHA KIUNGO MNIGERIA DAR..

Mwaka 2021 alijiunga na klabu ya Tshakhuma Tsha Madzivhandila, kabla ya kutimkia Moroka Swallows F.C. ambayo anaitumikia hadi sasa.