Home Habari za michezo BOCCO AGONGA MWAMBA MAHAKAMANI…OMBI LAKE LA KUDAI FIDIA YA MAMILIONI LAKATALIWA….

BOCCO AGONGA MWAMBA MAHAKAMANI…OMBI LAKE LA KUDAI FIDIA YA MAMILIONI LAKATALIWA….


Nahodha na mshambuliaji wa Simba, John Bocco ‘Adebayor’ amekwaa kisiki baada ya kesi ya madai fidia kwa kutumiwa picha ya sura yake katika tangazo la kibiashara bila ridhaa yake kukataliwa kusikilizwa na mahakama.

Bocco alifungua kesi dhidi ya kampuni ya Princess Leisure (T) Ltd, inayojishughulisha na biashara ya michezo ya kubashiri, Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza Masjala Ndogo, lakini mahakama hiyo imekataa kuisikiliza na kuitupilia mbali ikieleza haina mamlaka ya kuisikiliza kwa vile mahali ilipofunguliwa si sahihi na kinyume cha masharti ya kisheria.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Wilfredy Dyansobera kufuatia pingamizi alilowekewa Bocco na kampuni hiyo, kupitia wakili wake, Nabir Jumanne, akikubaliana na sababu hiyo moja kuwa imefunguliwa mahali pasipo sahihi, kati ya sababu tatu.

Bocco aliyewakilishwa na wakili Innocent Michael alikuwa akiiomba mahakama hiyo iiamuru kampuni hiyo imlipe fidia pamoja na mrabaha kutokana na mapato iliyoyapata kwa kutumia picha ya sura yake kutangaza huduma na bidhaa zake bila ridhaa yake.

Kwa mujibu wa hati ya madai, Bocco alikuwa akidai kampuni hiyo ilitumia sura yake hiyo katika kutangaza biashara yake katika mtandao wa Instagram kuhusiana na mechi ya Ligi ya Kuu ya NBC, baina ya Simba na Ruvu Shooting.

Alidai Novemba 18, 2021 alikuwa Mwanza akijiandaa na mechi hiyo iliyopangwa kuchezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba ndipo alipoweza kufahamu kulikuwa na tangazo la kibiashara katika mtandao wa Instagram lililosajiliwa kama winprincesstz.

Kabla ya kuanza usikilizwaji kampuni hiyo iliweka pingamizi ikiiomba mahakama hiyo isimsikikize Bocco, ikibainisha hoja tatu ikiwemo hoja ya mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kuisikiliza, ambayo ndiyo pekee ilitosha mahakama kuitupilia mbali kesi hiyo.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote kuhusiana na pingamizi hilo, Jaji Dyansobera katika uamuzi wake alikubaliana na hoja ya wakili Jumanne kuwa kesi hiyo haikupaswa kufunguliwa Mwanza, bali Dar es Salaam, mahali palipo na makazi ya kampuni hiyo mdaiwa na inakoendeshea shughuli zake hizo.

SOMA NA HII  FT: GEITA 1-1 SIMBA SC ....MPOLE AZIDI KUTAKATA...KIBU AWAOKOA NA AIBU YA KIPIGO...YANGA SASA BADO NNE TU....

Jaji Dyansobera alikubaliana na hoja ya utetezi wa wakili wa Bocco, Michael kuwa kuna Mahakama Kuu ya Tanzania moja tu isiyofungwa na mipaka ya kijiografia.

Hata hivyo, aliunga mkono hoja ya wakili wa kampuni ya Princess kwamba shauri hili lilipaswa kufunguliwa mahali yalipo makazi ya mdaiwa na anakoendeshea shughuli zake, au mahali kisa cha madai kilikotokea, ambako ni Dar es Salaam na si Mwanza.