Home Habari za michezo PABLO KUSEPA SIMBA…? ORLANDO PIRATES WAMWEKEA MEZANI OFA ‘BAB KUBWA’…KUMLIPA MILION 58

PABLO KUSEPA SIMBA…? ORLANDO PIRATES WAMWEKEA MEZANI OFA ‘BAB KUBWA’…KUMLIPA MILION 58


Klabu ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini inaangalia uwezekano wa kumpata Kocha Mkuu wa Klabu ya Simba SC, Pablo Franco, kuwa Kocha Mkuu wa Klabu hiyo Kwa Msimu ujao baada ya kutoridhishwa na Mwenendo wa Kocha aliyepo Klabuni hapo, Mjerumani Josef Zinnbauer.

Inaelezwa kwa nyakati tofauti mabosi wa Orlando wamefanya mazungumzo na Pablo na kuweka ofa yao ikiwemo kumuonyesha nyumba ya kifahari atakayofikia iwapo atakubali kujiunga nao, kuboreshewa mshahara kutoka Dola 14,000 za Kimarekani ambao ni zaidi ya Shilingi Milioni 32 za Kitanzania anaolipwa Simba hadi Dola 25,000 za Kimarekani ambao ni zaidi ya Shilingi Milioni 58 za Kitanzania kwa mwezi.

Hadi sasa Pablo bado hajafanya uamuzi kama atimke Msimbazi au la na huenda lolote linaweza kutokea kulingana na Ofa ilivyo.

Hata hivyo kwa siku za hivi karibuni, Pablo na uongozi wa Simba waliingia katika mtafaruku, ambapo kwa mujibu wa chombo kimoja cha habari, iliripotiwa kwamba Pablo haridhishwi na mazingira ya kufanyia kazi.

Katika taarifa ya chombo hivyo, Pablo alishindwa kufanya mazoezi na timu wakati ilipokuwa Moshi kujiandaa na mechi dhidi ya Polis Tanzania kwa kile alichodai kuwa uwanja wa mazoezi hauna hadhi anayoitaka.

Kulingana na taarifa ya chombo hicho cha habari, Kiongozi wa juu wa Simba alimpigia simu Pablo kutaka kujua hilo, lakini hakupokea, ndipo alipopigiwa meneja wa timu, Patrick Rweyemamu ambapo aliagizwa na kiongozi huyo kumpa simu Pablo lakini pia alikataa kuongea.

Baada ya tukio hilo, Kiongozi huyu alimpigia simu Kocha Msaidizi Suleiman Matola ambapo alipewa maagizo ya kusimamaia mazoezi ya timu, hali ambayo ilimlazimu baadaye sana Pablo kujiunga nao kishingo upande.

Mara baada ya timu kurudi Dar es Salaam, Pablo aliitwa na mabosi zake, ambapo katika hali isiyotarajiwa alinukuliwa akisema kuwa kama hawawezani naye wampe barua ya kusitisha mkataba , kisha wakutane naye akiwa na timu nyingie kwenye Nusu fainal ya kombe la shirikisho, ambapo walikuja kutolewa na Orlando Pirates ya Afrika kusini.

SOMA NA HII  SABABU ZA MO DEWJI KUMKATAA CHAMA SIMBA...HIZI HAPA

Hata hivyo, duru za ndani zinasema kuwa , Orlando walianza kumshawishi Pablo kabla ya mechi yao ya kwanza iliyofanyika Dar es Salaam, na walifanya hivyo pia kwenye mechi ya pili Afrika Kusini.

Itakumbukwa kuwa, Pablo alijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu, akichukua nafasi ya aliyekuwa kocha mkuu, Didier Gomes ambaye aliondoka mara baada ya kushindwa kuifikisha timu hiyo kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.