Home Habari za michezo SIMBA QUEENS WAZIDI KUTAKATA LIGI YA WANAWAKE…WAISASAMBUA FOUNTAIN GATE 4G….

SIMBA QUEENS WAZIDI KUTAKATA LIGI YA WANAWAKE…WAISASAMBUA FOUNTAIN GATE 4G….


Fountain Gate Princess imekubali kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Simba Queens katika mchezo wa Ligi kuu ya Wanawake (WPL) kipute kilichofanyika jana katika uwanja wa Fountain Gate Arena Jijini Dodoma.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Fountain walikubali kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Simba mchezo uliofanyika katika uwanja wa Mo Simba Arena.

Mchezo huo ulishuhudiwa na Kocha wa timu za Taifa za Wanawake,Bakari Shime na Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka nchini( TFF) Oscar Milambo.

Ikicheza kwa kujiamini Simba Queens ilianza kupata bao dakika ya pili ya mchezo kupitia kwa mshambuliaji Asha Djafar.

Djafar alifunga bao hilo baada ya mabeki wa Fountain, Crister John na Protasia Mbudya kushindwa kuokoa mpira ambao ulikuwa ukizagaa katika lango la Fountain.

Simba Queens ilijipatia bao la pili dakika ya 24 kupitia kwa Aisha Juma mara baada ya mabeki wa Fountain kudhani ameotea.

Hadi mapumziko Simba Queens walikuwa mbele kwa mabao 2-0.

Kipindi Cha pili kilianza taratibu ambapo Kocha wa Fountain,Juma Masoud aliwatoa,Sarrive Badiambila na Agnes Pallangyo na nafasi zao kuchukuliwa na Mariam Semgomba na Winfrida Gerrald.

Kwa upande wa Simba walimtoa Asha Djafar na nafasi yake kuchukuliwa na Amina Ramadhan.

Mabadiliko hayo yaliipa ahueni Fountain na dakika ya 72 Winfrida almanusura aipatie timu yake bao lakini kipa wa Simba Queen,Gwela Yonah aliokoa na kuwa kona.

Mabadiliko hayo yaliiongezea nguvu Simba ambapo dakika ya 85 mshambuliaji wa Fountain,Mariamu Semgomba alipiga shuti Kali lakini kipa wa Simba aliokoa na kuwa kona.

Dakika ya 84 mshambuliaji hatari wa Simba, Aisha Juma aliipatia timu yake bao la 3 kwa shuti kali.

Juma alifunga bao hilo mara baada ya kupokea pasi kutoka kwa Mchezaji aliyetokea benchi,Amina Ramadhan.

Bao la 4 la Simba liliwekwa kimiani na Jackine Albert mara baada ya mabeki wa Fountain kushindwa kumkaba mfungaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here