Yanga haijamaliza kazi ya kushusha vifaa vipya kwa msimu ujao na baada ya kumaliza usajili wa mshambuliaji Stephane Aziz KI sasa wamehamia msako wa beki mmoja wa pembeni ambaye matajiri wa klabu hiyo GSM wameapa kuleta mtu mwingine wa kazi.
Kuna majina mawili ya mabeki wawili ambao Yanga sasa inapambana nayo wakiwa katika hatua za mwisho kabisa kuamua yupi avae jezi za njano na kijani kwa msimu ujao ambapo klabu hiyo itakuwa ikirejea tena katika mbio za Ligi ya Mabingwa Afrika.
WONLO COULIBALY
Beki wa kwanza ambaye Yanga wanapambana naye ni Wanlo Coulibaly raia wa Ivory Coast ambaye yupo pale jijini Abidjan akiitumikia klabu ya ASEC Mimosas.
Coulibaly yumo katika rada za Yanga baada ya kuwa na msimu mzuri na ASEC akiwa katika kikosi cha kwanza na aliwahi kushuka hapa nchini akicheza mechi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, lakini na ile ya ugenini akikosa mechi moja tu ya hatua hiyo kwa kutumikia kadi ya njano.
Tayari Yanga ilishafanya mazungumzo ya awali na beki huyo anayejua kupiga krosi za mabao na akili kubwa kwa Yanga ni staa huyo atakuja kuunganika kwa haraka na KI ambaye tayari ameshamalizana na klabu hiyo.
JOYCE LOMALISA
Jina lingine ni Joyce Lomalisa raia wa DR Congo ambaye yumo katika listi hiyo na ubora wake wa ‘kumwaga maji’ unawaumiza kichwa mabosi wa Yanga.
Mastaa hao wawili wako katika mazungumzo na Rais mtarajiwa wa Yanga injinia Hersi Said ambaye ni mgombea pekee wa nafasi hiyo katika uchaguzi unaoendelea.
Akili ambayo Yanga inaipiga ni jinsi itafanikiwa akuchukua staa yupi kati ya hao ingawa Coulibaly anaonekana staa ambaye yuko kwenye moto kwa kutoka katika klabu ambayo imecheza hatua ya makundi msimu huu huku Lomalisa akiwa amesotea benchi akiwa na Sagrada Esperança.
Lomalisa mwaka mmoja uliopita alikuwa kwenye moto mkali katika kiwango chake akiitwa mpaka timu ya taifa hilo ingawa hakupata nafasi ya kucheza akiwa benchi.
Kocha wa Yanga Nasreddine Nabi katika ripoti yake inahitaji beki wa kushoto na kama mmoja kati ya Coulibaly na Lomalisa watasaini basi haraka kuna beki mmoja kati ya Yassin Mustapha na David Bryson mmoja huenda akapewa mkono wa kwaheri.
Huenda Yanga ikaamua kubaki na Bryson ambaye bado amesalia na mwaka mmoja wa mkataba wake huku Yassin akiwa katika wakati mgumu kutokana na mkataba wake unafikia tamati mwisho wa msimu huu.