Harmonize au Teacher Konde; ni staa wa muziki kutoka kiwanda cha Bongo Fleva ambaye ameonesha nia yake ya kushiriki katika mchezo wa Tamasha la Samakiba ambalo ni ‘projekti’ inayoendeshwa na Mfalme wa Bongo Fleva, King Kiba na staa wa soka wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta.
Lengo la Samakiba ambalo hufanyika kila mwaka baada ya kumalizika kwa msimu wa soka ni kuchangia elimu nchini Tanzania.
Harmonize anasema; “Samatta msanii wako namkabia juu kabisa havuki nusu uwanja, halafu nakuwekea mtambaliko kama Sure Boy, nataka uniwekee wanangu, Jonas Mkude, Feisal pale dimbani, kushoto niwekee Chilunda, kulia niwekee Idd Nado.”
Ujumbe huo unamaanisha kwamba Harmonize ameomba nafasi kwenye timu Samatta ambapo atakuwa mpinzani wa King Kiba wakiwa uwanjani.
Kumbuka King Kiba ndiye msanii pekee wa Bongo Fleva aliyewahi kushiriki Ligi Kuu ya Tanznaia Bara akikipiga katika Klabu ya Coastal Union ya jijini Tanga.
Swali wanalojiuliza wengi ni kwamba, je, Harmonize ataweza kumkaba King Kiba huku wote wakiwa wanaendelea na mazoezi ya gym?