Home Habari za michezo KWA HILI ZA MZAMIRU…KWA KWELI MINNE TENA…JAMAA KAMA KAZALIWA UPYA VILE…SIMBA WAKIMUACHA...

KWA HILI ZA MZAMIRU…KWA KWELI MINNE TENA…JAMAA KAMA KAZALIWA UPYA VILE…SIMBA WAKIMUACHA IMEKULA KWAO…


Na Mohammedi Kuyunga/MwanaSpoti

ULIMWONA Mzamiru Yasin akiitumikia Timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars‚‘dhidi ya Algeria?

Ni katika mchezo ule wa kuwania kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), Juni 8 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam.

Bado ulimwona Mzamiru katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Mbeya City?

Katika michezo hiyo miwili Mzamiru ameupiga mwingi hadi umemwagika. Ingawaje Stars ilipoteza kwa kufungwa 2-0 dhidi ya Algeria lakini Mzamiru alifanya kazi kubwa sana.

Pia, katika mchezo wa ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mbeya City katika uwanja huohuo wa Benjamini Mkapa, kiungo huyo alikichafua kinoma.

Baadhi ya mashabiki wa Simba wamesikika wakitaka kiungo huyo aongezewe mkataba. Tena apewe miaka minne sio miwili kama ilivyozoeleka.

Kauli hii imekuja kipindi hiki Simba mwishoni mwa msimu huku klabu hiyo ikiwa katika harakati za kufanya mabadiliko makubwa kwenye kikosi chake.

Mwanzoni mwa msimu hali ilikuwa tofauti kabisa. Kama kulikuwa na mashabiki wenye shaka na uwezo wa kiungo huyo, basi ni wale wa timu yake ya Simba Sports.

Umeshawahi kuwasikia mashabiki wa klabu hiyo wakimponda kiungo huyo siku za hivi karibuni.

Kama ungewasikia ungeweza kusema mchezaji huyu ni wa ovyo na hafai kabisa kuitumikia timu hiyo yenye masikani yake pale Mtaa wa Msimbazi. Katika kipindi kirefu Mzamiru amekuwa haimbwi vizuri na mashabiki wa timu yake hata pale anapofanya vizuri uwanjani lakini anapokosea tu huwa ni balaa.

Shutuma zote huwa juu yake, hasa inapotokea Simba inapopoteza mchezo na yeye kuwamo kikosini. Sijui kama mchezaji huyu amekuwa akisikia kile anachoambiwa au anavyopondwa na mashabiki wa timu yake pindi alipokuwa akikosea, sijui!

Usajili wake msimu huu

Hivi karibuni ilifikia hatua baadhi ya mashabiki wa Simba wamekuwa wakimpigia hesabu za kuachwa katika usajili wa kujenga kikosi kipya ndani ya Simba kwa ajili ya msimu ujao.

Lakini kama viongozi na mashabiki wa Simba walikuwa na mpango wa kuachana na kiungo huyu, sidhani kama bado wanayo ajenda hiyo baada ya kumwona kiungo huyo katika mchezo wa Stars na Algeria.

Hata katika mchezo ule wa Ligi Kuu dhidi ya Mbeya City. Mzamiru aling’ara utadhani ni mchezaji mgeni anayekuja kutafuta malisho mapya.

Katika mchezo wa Stars na Algeria kila aliyetoka uwanjani aliliimba jina lake pamoja na Stars kupoteza mchezo. Ilifikia baadhi ya mashabiki kujiuliza kwa nini Mzamiru huwa hachezi vile siku zote.

Ikumbukwe kuwa tangu msimu ulipoanza na hatimaye Simba kupoteza mataji yote mawili ya Ligi Kuu na lile la Azam Sports Federation Cup (ASFC) mashabiki wengi wa Simba wamekuwa hawamzunguzii vizuri kiungo huyo.

Kocha wa zamani wa Simba, Pablo Franco Martin hakuwa akimpa nafasi kubwa Mzamiru. Na alipofanya mabadiliko na kumuingiza Mzamiru, wengi waliguna.

Laiti kama Mzamiru angekuwa anasikia au anajua shutuma alizokuwa anapewa angeweza kukata tamaa ya kuitumikia timu hiyo.

Tangu aliponyang’anywa mpira na kiungo wa Yanga, Balama Mapinduzi katika mchezo wa sare 2-2 uliopigwa Januari 4, 2020 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na kusababisha bao la kwanza la Yanga, wengi walikosa imani naye.

SOMA NA HII  HUKO SIMBA MAMBO NI BAMBAM....MAKI HATAKI MASIKHARA NA YANGA LEO...DOZI ZAKE KAMILI HIZI HAPA...

Mzamiru akiwa nje kidogo ya dimba alishindwa kuutuliza vizuri mpira mrefu uliotoka kwa mabeki wa Yanga na kumfikia Mapinduzi. Na bado Mzamiru alishindwa kumalizana na Mapinduzi nje ya 18 na kumwacha apige shuti lililomshinda, Aishi Manula na kujaa kimiani.

Bao la Fei Toto pia

Pia, katika mchezo wa nusu fainali ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) wa Mei 28, 2022 pasi ya Mzamiru kwenda kwa Chris Mugalu ilinaswa na kiungo wa Yanga, Khalid Aucho aliyempenyezea mpira huo, Fei ambaye alivuta na kuachia shuti kali lilikuwa bao pekee la ushindi kwa Yanga.

Pasi hiyo ilinaswa wakati viungo wangine wa Simba, Sadio Kanoute na Taddeo Lwanga walikuwa wakiamini timu inapanda, nao walipanda juu na kushindwa kurudi ghafla kumkaba Fei.

Wengi wanaamini Mzamiru angeweza kufanya kitu kingine kwa kubadili uelekeo wa mpira tofauti na alivyofanya.

Pamoja na makosa hayo, lakini Mzamiru ni fundi katika ukabaji na kuziba nafasi. Mara nyingi amekuwa akificha udhaifu wa wachezaji wengi kwa kuwafutia makossa yao.Hata aliyemuita jina la utani la ‘Kiungo Punda‚‘ ni kwasababu alikuwa anaijua kazi yake uwanjani. Ukimwangalia Mzamiru unaweza usimuone uwanjani lakini ni kiungo wa jasho na damu na unaweza kumfananisha na kiungo wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa, Real Madrid na Chelsea, Claude Makelele.

Mzamiru na Makelele mwenye asili ya DR Congo wanalandana kidogo kwenye vimo, Makelele akiwa mrefu kidogo futi 5 na nchi 9.

Mzamiru ni mfupi kidogo kwa Makelele lakini wachezaji wengi wa aina yake ni wagumu sana kuwanyang’anya mipira pindi wanapojishindilia chini. Kama wanakuwa fiti kimazoezi, huweza kutawala eneo la kati vile watakavyo.

Tatizo lake uwanjani

Pamoja na Mzamiru kukaba vizuri na anaweza kuipandisha timu juu lakini tatizo lake kubwa ni kwenye kutoa pasi zisizokuwa na macho.

Ni mara chache amefanikiwa kutoa pasi hizo. Lakini ameshapoteza mipira mingi katika mwelekeo ambao umeleta madhara au kosakosa katika lango la timu yake.

Tatizo linaanzia pale, Mzamiru anapokuwa na mpira akimiliki mpira, mara nyingi huwa anaonekana kuinama na kuangalia chini kama kondoo anayetafuta kitu chini ya ardhi.

Wachezaji wengi huinua macho kabla ya kuupokea mpira na kuangalia mazingira wanapoumiliki huwa wanajua nini wanachotakiwa kukifanya kabla ya kuuondoa katika eneo husika.

Tatizo hilo kwa Mzamiru laiti angeweza kulifanyia kazi, basi maneno mabaya dhidi yake yangepungua au kuisha kabisa.

Mbali na tatizo la kushindwa kupiga pasi za uhakika, Mzamiru anatakiwa ajifunze vilevile kunusa hatari kutokana na maeneo ya katikati ya uwanja anayocheza.

Mzamiru sio mchezaji anayepewa kadi mara kwa mara, lakini anatakiwa ajue kumalizana na mtu kabla hajafikia kuleta madhara kwenye timu.

Pasi fupi na ndefu

Mzamiru wa Stars dhidi ya Algeria na Simba na Mbeya City alikuwa akipiga pasi ndefu na kuinua macho yake. Alikuwa akibadilisha mwelekeo wa mipira. Inawezekana amenza kubadilika na sio kama anapigania mkataba mpya ndani ya Simba.