Mshambuliaji wa Simba, Yusufu Mhilu ameeleza kurudi Kagera Sugar msimu ujao, huku akisisitiza kujipanga upya na kuwa kwenye ubora utakaowashangaza wengi.
Mchezaji huyo alijiunga Simba msimu wa 2020/21 akitokea Kagera Sugar kwa mkataba wa miaka mitatu ambao ameutumikia msimu mmoja pekee na klabu hiyo kumtoa kwa mkopo msimu huu baada ya kushindwa kuendana na kasi ya timu hiyo.
Mhilu amesema kuwa ameamua kurudi nyumbani ambako anaamini ataendeleza pale alipoishia baada ya kocha Francis Baraza kukubali kumpokea.
“Nilipewa nafasi ya kutafuta timu ambayo naweza kucheza kwa mkopo. Kulikuwa na timu mbili ya Kabwe Warriors ya Zambia na waajiri wangu wa zamani Kagera Sugar, hivyo nimeamua kurudi nyumbani kutokana na kuelewana maslahi tofauti na Kabwe,” alisema mchezaji huyo.
“Kagera ndiko nilikokulia kisoka na walinipa nafasi ya kuonekana hadi Simba kunisajili, hivyo nina uhakika wa nafasi ya kucheza kwa mara nyingine nikiwa huko na ninaahidi kuitumia ipasavyo ili kurudi kwenye kiwango changu cha mwanzo, sitaki kufanya makosa.”
Alisema anaamini ukubwa wa Simba, uzoefu alioupata na namna timu hiyo ilivyomjenga zaidi, vitakuwa chachu kwake kuvitumia atakapokuwa na Kagera Sugar sambamba na kupambana kuifungia mabao mengi zaidi ya yale ya miaka ya nyuma kabla hajatimkia Simba.