Home Habari za michezo MKUDE AFUNGUKA A-Z MAISHA YAKE YAKUITUMIKIA SIMBA NA PANDA SHUKA ZAKE…AGUSIA SUALA...

MKUDE AFUNGUKA A-Z MAISHA YAKE YAKUITUMIKIA SIMBA NA PANDA SHUKA ZAKE…AGUSIA SUALA LA KULEWA …AMTAJA MORRISON..


Jonas Gerad Mkude au unaweza kumuita Nungunungu, ni moja kati ya wachezaji walioitumikia Simba SC kwa muda mrefu zaidi, takriban miaka 12.

Akisimulia historia ya maisha yake kupitia Simba APP, Mkude anasema alianza kuitumikia Simba B baada ya kuonekana kwenye mashindano ya under 20.

“Matola (Seleman) pamoja na meneja Patrick Rwemamu ndiyo waliniona na kuweza kufanya kila lililotakiwa kufanywa kufanikisha mimi kufika Simba,” anasema Mkude.

Mkunde ambaye amezaliwa mwaka 1992, anasema kipaji chake kilianza tangu akiwa mdogo akiwa anasoma shule ya Msingi Hananasifu Kinondoni hadi baadaye alipokuja kuonekana kupitia michuano ya under 20 kupitia timu yake ya Hananasifu Combine.

“Nilivuruga sana pale kati, kipindi hicho kocha Matola na Rwemamu ndiyo walinifuata baada kurudi Dar kutoka Arusha kule tulipocheza hiyo michuano nakajiunga na Simba B,” anasema Mkude.

Akizungumzia kudumu miaka mingi ndani ya kikosi hicho cha Simba SC, Mkude alisema nidhamu na kujituma na Mungu mwenyewe ndiye aliyepanga.

“Nimshukuru Mungu kunijalia mpaka leo kuwepo. Nimekutana na changamoto nyingi sana. Mimi ni binadamu, shukran kwa mashabiki wa Simba. Kipaji pekee hakiwezi kukufikisha kama hapa nilipo,” anasema Mkude.

Mkude alipoulizwa kuhusu suala la Bernard Morison kumtaja kwamba ndiye mchezaji aliyecheza muda mrefu katika tamasha la Simba Day kwamba kama walipanga au la Mkude akasema hawakupanga.

“Sikuwahi kukaa naye kupanga. Alizungumza mwenyewe nadhani kwa kuwa yeye ni mchezaji mkongwe, kapitia changamoto nyingi anafahamu kukaa kwenye timu hizi kubwa kwa muda mrefu sio kazi rafisi.”

Kiungo huyo mkabaji anasema, ndani ya miaka hiyo aliyodumu Simba amepitia changamoto hususan katika miaka miwili iliyopita.

“Hiki kipindi nimekutana na changamoto, niliteleza na kukosea. Nilifungiwa kama mara mbili lakini ni changamoto tu za kibinadamu. Tumezifuta na sasa maisha yanaendelea japo wengine bado wanabaki tu kusema Mkude mtovu wa nidhamu,” anasema Mkude.

Kuhusu suala la kunywa pombe, Mkude alikiri kuwa anakunywa lakini akasema sio kwa kiasi cha kupitiliza kama ambavyo baadhi ya watu wanazusha.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA NYUMA GAZETI LA SPOTI XTRA JUMANNE

“Mimi na kunywa lakini nakunywa kwenye wakati gani? Athari ya kitu ni pale unapokizidisha. Nilishawahi kuingia uwanjani nikiwa nimelewa? Nilishawahi kunywa hadi nikavua nguo? Nilishalewa nikakutwa nimelala nimezima? Hakuna,” anahoji Mkude.

Mkude anasema baadhi ya watu hupenda kumzungumzia yeye kwa mambo ambayo hayana ukweli na kusahau yeye nje ya mpira ana maisha yake binafsi, ana watoto na familia.

Alipoulizwa na mtangazaji wa Simba APP Ahmed Ally kwamba kuna kipindi alikosa ubingwa akiwa amejiunga na Simba kwa takriban miaka mitano, Mkude anasema kipindi hicho aliumia sana lakini aliendelea kupambana maana aliamini mafanikio yapo njiani.

“Niliumia lakini nilikuwa najua kuna kitu kizuri kinakuja. Tulipambana kama timu na kufanikiwa kuanza kupata mafanikio” anasema Mkude.