Home CAF RAIS CAF AAPIGILIA MSITARI TANZANIA NA UGANDA KUANDAA AFCON 2027…AHAIDI MAMBO HAYA...

RAIS CAF AAPIGILIA MSITARI TANZANIA NA UGANDA KUANDAA AFCON 2027…AHAIDI MAMBO HAYA MAKUBWA….


Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Patrice Motsepe amefichua atakaribisha na kuhimiza mpango wowote utakaowezesha Uganda na Tanzania kuwa mwenyeji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2027.

Motsepe ambaye yuko Uganda kwa ziara ya siku mbili na ameeleza hisia zake kuhusu Afcon 2027 na alisema akiwa rais wa bodi inayoongoza, analazimika kuunga mkono vyama vyote wanachama.

Wazo la kuandaa fainali hiyo lilianzishwa na Spika wa Bunge la Uganda, Anita Among, ambaye alisema tayari wamefanya mazungumzo na Rais Yoweri Museveni kuhusu hilo.

“Tulifanya mazungumzo na Rais [Yoweri Museveni] na tuko tayari kufanya uenyeji pamoja na Tanzania. Tumepata kibali kutoka kwa rais wetu na tutaweza kufanya hivyo,” alisema Among.

“Niliambiwa Uganda na Tanzania ziko tayari kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika 2027 [Afcon] katika nchi hizi mbili nzuri,” alisema Motsepe.

“Kama Rais wa Caf, sina budi kuunga mkono vyama vyote 54 wanachama kwa usawa na niseme binafsi nisingekaribisha tu bali nitahimiza uenyeji wa pamoja kati ya nchi hizi mbili kwa sababu utatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya soka Uganda na Tanzania.

“Kanda hii [Cecafa] haijawahi kuandaa Kombe la Mataifa ya Afrika hapo awali na itakuwa hatua nzuri kwa Uganda na Tanzania, sio tu katika kukuza maendeleo ya soka, pia katika maeneo mengine kama utalii, uwekezaji na kukuza uchumi.”

Wakati huo huo, Rais huyo ambaye ni raia wa Afrika Kusini alifichua sababu za kipaumbele kwa nini yuko Uganda.

“Niko hapa kutoa mchango wa unyenyekevu katika maendeleo ya soka nchini, pia kufanya majadiliano na baadhi ya watu wetu katika sekta binafsi ili kusisitiza wajibu wao katika mchezo huo,” aliongeza.

“Nimefurahi kujifunza kuhusu mchango ambao serikali inatoa katika soka na michezo kwa jumla katika nchi hii.”

Motsepe aliandamana na Rais wa Fufa, Moses Magogo, Rais wa Cecafa, Wallace Karia, Naibu Spika Thomas Tayebwa na Waziri wa Michezo wa Uganda, Denis Obua wakati wa ziara yake Ikulu ya Entebbe kumtembelea Rais Museveni.

SOMA NA HII  SONSO AJIFUNGA MWAKA MMOJA NDANI YA RUVU SHOOTING