WAKATI Ligi Kuu Bara ikianza kutimua vumbi jana, kinara wa mabao msimu uliopita George Mpole anasema hajui hatma yake ya kucheza Tanzania msimu huu ingawa uongozi wa Geita unasisitiza kwamba ni mchezaji wao na ameomba udhuru.
Mpole ambaye yupo kwao Mbeya hakutaja timu ambazo zinahitaji saini yake zaidi ya kuweka wazi kuwa ni za Afrika Kusini na Morocco.
Mpole alimaliza msimu akifunga mabao 17 na Geita Gold ambao wanacheza mechi yao ya kwanza ya ligi kesho Jumatano dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Mpole alisema amemaliza mkataba na waajiri wake wa zamani Geita lakini wao bado wanasisitiza kuwa wataungana na mchezaji huyo jijini Dar es Salaam akitokea mapumziko baada ya kutoka Taifa Stars walipocheza dhidi ya Somalia.
Mpole alisema; “Nipo Mbeya naendelea na mazoezi binafsi bado sijajua nitacheza timu gani msimu ujao na sipo tayari kulizungumzia hilo kwa sasa kwa sababu nimewaachia wasimamizi wangu na mambo yakiwa tayari kila kitu nitakiweka wazi timu nitakayochezea lakini nchi nilizopokea ofa ndio hizo nilizokwambia.
“Hakuna mchezaji ambaye anapenda kukaa nje ya timu nina malengo yangu na ndio maana nipo huku siwezi kufanya mambo kwa kukurupuka nikihofia nitasemwa, muda utaongea dirisha bado halijafungwa hivyo mambo yakienda kama nilivyopanga taarifa zitatoka ni wapi nitacheza msimu ujao lakini kwa sasa naenelea na mazoezi binafsi.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Geita, Costantine Morandi alisema; “Bado ni mchezaji wetu hakuwa pamoja na timu kwasababu ya ruhusa maalum atakuwa pamoja na timu kuanzia kesho suala la kucheza dhidi ya Simba au kutokucheza tunamuachia kocha.”
WAIPANIA SIMBA
Nyota wa timu hiyo nao wameonekana kupania mechi hiyo huku wakiapa kutonesha kidonda cha kufungwa na watani zao Yanga katika mechi ya Ngao ya Jamii mabao 2-1.
Kiungo wa timu hiyo, Godfrey Manyasi alisema kuwa; “Ni mchezo mgumu kwa sababu ni mwanzo wa ligi na timu zote zimejiandaa vizuri na tumeiona Simba ilipocheza na St. George na Yanga, hivyo makocha wameona mbinu za kwenda kuzitumia, mipango yetu ni kuwa na mwendelezo ule ule wa kupambana na kufikia malengo tuliyojiwekea kama msimu uliopita. Usajili mpya umeongeza chachu sana ya upambanaji na kutokwenda Burundi hakujatuathiri kwa sababu maandalizi ni popote.”